WAZANZIBARI NA USINGIZI WA ‘AS-HABUL-KAHAFI’

Written by  //  01/01/2013  //  Makala/Tahariri  //  7 Comments

KAHF

Kisa cha watu wa pangoni, yaani kwa lugha ya kiarabu ‘ashaabul-kahfi’, ni miongoni mwa visa vikongwe katika historia ya dini na maisha ya mwanadamu. Kisa hiki ambacho ni moja ya visa vingi vinavyoonesha utukufu na uwezo mkubwa wa Mola wetu Muumba, Allah subhaanahu wataala, si maarufu katika uislamu tu, bali hata katika dini na jamii nyengine duniani.
Kwa muhtasari, kisa hiki kinawahusu watu wasiopungua saba, na mbwa wao, waliokimbia mateso ya utawala kandamizi katika nchi yao. Katika kimbia kimbia yao hiyo, walifika pahala wakaingia kwenye pango kujipumzisha. Hapo Mola mtukufu aliwalaza usingizi mrefu zaidi kuliko usingizi wowote aliowahi kulazwa mwanadamu na mola wake, ukitoa maiti waliokwishatangulia mbele ya haki.Watu hawa waliamka baada ya kulala kwa miaka inayosadikiwa kutimu 300 na ushei. Ambapo, walipoamka walikuwa wageni katika ardhi yao waliyozaliwa na kukulia humo. Allah akbar!

Nimelazimika kukikumbuka kisa hiki kikongwe kwa kukinasibisha na maisha halisi wanayoishi wazanzibari wakiwa chini ya himaya ya Muungano. Himaya, kwa maana wakiwa chini ya uangalizi na udhibiti wa Muungano huo ambao kwa kughafilika na kulala kwao kwingi wamejikutia au watajikutia wakiamka mbali na zama za siku walizolala.Pia wameamka au wataamka wakiwa wageni katika nchi yao kama walivyokuwa ‘as-haabul-kahfi’.

Ikiwa imepita miaka 48 sasa ya Muungano, huku Zanzibar ikizidi kupoteza himaya yake na kila kitu chake, kuna kila dalili kwamba sehemu kubwa ya wahusika wa kuitetea nchi hii kuwa bado hawajaamka. Wamelala pangoni bila kujitambuwa.
Wazanzibari tumelala usingizi mnene, mzito, uliojaa mkoromo, korozo, na ndoto za mwasande(mwanamke anaemjia mwanamme ndotoni kimapenzi), tena katika bustani za Adeni. Wakati sisi tukistarehe na mwasande, wenzetu hawalali, wanakusanya kila kilicho chetu. Na yule mbwa wetu tuliemchukuwa kule pangoni, katupiwa fupa ambalo hugunya, akichoka nae hulala. Hata habweki, maskini.

Na kwa usingizi huu, tumepoteza utambulisho wetu, utaifa, mila na desturi zetu, na kila kitu. Kwa kulala kwetu huko kusikokwisha, tukipumbazwa na ndoto za mwasande, huku tukiamini mbwa wetu yupo kutulinda, bila kutanabahi hasara inayotukabili. Kumbe vile tunarudi nyuma kiamendelo huku washirika wetu wakikimbia kwa kasi ya ajabu. Kasi ambayo hata siku tukiamka, tutalala tena kwa kukata tamaa kwa walivyotuacha duni na umbali walioko wao.

Kwa sababu ya usingizi wetu mzito, Wazanzinbari ambao kiasili ni magwiji, wazawa na wamiliki halisi wa lugha ya KISWAHILI duniani, leo wanasomeshwa Kiswahili na watu wa bara. Pamoja na kasumba zinazoenezwa na wenzetu wa Kenya na Tanganyika kuwaambia wageni na kuandika vitabuni kuwa Kiswahili hakina wenyewe, ukweli unabaki kuwa wenyewe hasa ni Wazanzibari ambao hawazaliwi na lugha nyengine yoyote ukiacha Kiswahili, seuze wao wanauzungumza Kiswahili kama lugha yao ya tatu au ya nne.

Hata hivyo, sishangai sana kuwasikia wenzetu wa bara na Kenya wakisema Kiswahili hakina wenyewe. Ni kweli kiasi fulani maana kama wapo kweli Waswahili, wangesema, wangejibu, au hata kujitetea kwa njia moja au nyengine. Lakini tupo, tumelala, watu wanajivunia Kiswahili chetu na kujipatia utajiri mkubwa na shahada za juu za Elimu huku sisi tukizidi kutokwa na ‘dovuo’(madenda) kwa usingizi mzito uliotuvaa.

Ni jambo la aibu na fedheha kuona Wizara ya Elimu Zanzibar, ikiwapiga chenga wataalamu wa Kiswahili waliopo taasisi ya Kiswahili na lugha za kigeni (SUZA), na kukimbilia waandishi wa bara kuwatungia vitabu vya kufundishia Kiswahili Zanzibar. Iweje wenzetu wa bara, japo wana shahada kubwa za Kiswahili, lakini ukweli wao sio waswahili, wawe ndio mabingwa wa kutuandikia sisi vitabu vya Kiswahili? Haya sio yale ya ‘kuku kupanda basikeli na bata kuvaa raizoni’?
Ukweli tunaheshimu sana taaluma ya wenzetu na kila mtu, lakini ikumbukwe kwamba zamani vitabu vyetu vya Kiswahili ndivyo vilivyovikitumika Afrika mashariki nzima na duniani kufundishia Kiswahili. Na vilikuwa vizuri na vyenye kufunza Kiswahili cha kikweli.Lakini ukiviangalia vitabu vya Kiswahili tunavyoandikiwa bara na kamusi, ni ‘korogo-vyogo’ tu!
Sambamba na haya, kuna ombwe la vilio juu ya Kiswahili kinavyoharibiwa na wenzetu wa Kenya na Bara. Tena kwa bahati mbaya,kinaharibiwa na wale wanaoitangazia dunia kuwa wao ndio wajuzi wa Kiswahili. Ama kweli, penye vipofu, chongo huwa mfalme. Wakati sisi tumelala, wao wanajichumia na kututungia maneno yasiyokuwa na nyuma wala mbele.

Isitoshe mengi yao maneno hayo, kwa mila na desturi zetu ni matusi ya laana, lakini kwa vile hii si lugha yao hawalijui hilo.Je, tunategemea nini iwapo wao hawatajuwa mipaka, miko na itikadi ya lugha hii ambayo wenyewe wameisahau chini ya vitanda vyao walivyolalia usingizi mzito wa watu wa pangoni?

Kuna wenzetu wa bara na Kenya wametajirika kwa kufundisha Kiswahili nje ya nchi na kuandika vitabu vya Kiswahili. Japo vingi ya vitabu vyao hivyo na hasa kamusi, ni vyenye kiwango duni, lakini madamu hakuna chengine, wao ndio watatambulika. Sisi wazanzibari tupo, hatuandiki, hatuziombi kazi hizo hata zikitangazwa kiasi gani. Letu dharau nyingi tu, tukitajiwa kufundisha Kiswahili.Utasikia ‘ah! Kiswahili kitu gani? Tunawaachia wenzetu wakifaidika bure!
Leo hii kumkuta Mzanzibari anaefundisha Kiswahili nje ya nchi ni nadra. Na sijui hata kama yupo. Na kama wapo, ni mmoja kwa mia. Kiswahili kina wakenya na wabara tu kule Marekani, Uingereza, na kila pahala ni Mkenya, Mbara tu. Zanzibar tumelala, huku tukisondogewa na dume la ng’ombe lililokata kamba liitwalo Muungano bila huruma na wala hatufanyi jitihada ya kujitetea.

Pamoja na yote haya, suali hili linachangiwa na viongozi, taasisi zetu za elimu, na wasomi wa Kizanzibari waliopo. Ambao, wao ni nguvu kazi kubwa na wanaopaswa kusimama na kukikingia kifua Kiswahili, kukitetea na kukirejeashea hadhi yake.

Bahati mbaya hakuna msomi anaeandika tena hapa petu. Ukitoa wale wachache waliowakiandika hadithi na mashairi siku hizo, hakuna mwengine. Na bahati mbaya hawa pia vitabu vyao haviingizwi katika silabasi ya bara kwa madai Kiswahili chao ni kigumu, hakimo katika kamusi zao.
Lakini yote haya ni kwa sababu hapana Kiongozi anaelipa kipaumbele suali hili. Ndio maana ukaona hata ile TAKILUKI pale SUZA, imedorora. Haichapishi, haiandiki kitu, inasubiri tuandikiwe kamusi na vitabu kutoka bara. Kamusi zenye maneno ya kikabila, mengi yakiwa ya matusi, yasiyoingia akilini, tuwafundishe watoto wetu. Kule Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA), japo wametoa kamusi lakini ni la lugha moja tu, halikidhi haja. Pia wanaonekana kufunikwa sana na wenzao wa kule bara.

Kwa kweli, ipo haja kwa Serikali, viongozi, wasomi, na taasisi husika Zanzibar kulivalia njuga suali hili. Kwani Zanzibar kama Zanzibar, tumeshapoteza vingi katika Muungano, na ni vigumu kuvirudisha tena. Basi na hili la Kiswahili kuna dalili ya kukipoteza. Kiswahili, lugha ya mama na baba zetu. Lugha ya wahenga wetu, utu wetu, na utambulisho wetu? Hatuoni hata kimeme, tunakiacha kikifaidisha watu wengine. Bado tumelala tu.
Tuamkeni Wazanzibari, tujiandikie vitabu vyetu, kamusi zetu. Kamusi zinazosawiri muktadha wa mazingira na tamaduni zetu. Vitabu, vyenye kuandika Kiswahili chetu na sio chao. Hili tunaweza na halihitaji, tume ya Warioba kamwe. Hivi hatuoni aibu, hata Kiswahili tufundishwe na bara? Tuamke, Inatosha, kwani ‘Mwana mtambuwa shibae, hashibiwi’.

About the Author

View all posts by

7 Comments on "WAZANZIBARI NA USINGIZI WA ‘AS-HABUL-KAHAFI’"

  1. Makame Ame 01/01/2013 at 7:28 mu ·

    Angalizo kwa faida ya ahli-l-ilm:

    “….Watu hawa waliamka baada ya kulala kwa miaka inayosadikiwa kutimu 300 na ushei. Ambapo, walipoamka walikuwa wageni katika ardhi yao waliyozaliwa na kukulia humo. Allah akbar!

    Ni miaka 300 Thalathamia (Shamsia – ya Jua) ambayo ni sawa na miaka 309 thathamia na tisa (Qamaria – ya mwezi). Hiyo ndiyo tafisri ya 25 ya suratu-l-kahf. Yaanu ukichukuwa hesabu tarehe ya leo kwa hijri (Qamaria) na Gregorian (Shamsia) itachukua miaka mingine 300 (Shamsia) sawa na 309 (Qamaria) tarhe hiyo ikutane tena.

    Kwa mfano leo ni tarehe 1 January 2013 sawa na 19 Safar 1434 ni mpaka 1 January 2313 tarehe hizi zitakutana tena hjri ikiwa 19 Safar 1743.

    Hiki ni kijiilmu kidogo nilichokipata nilipokuwa nikisoma ilmu ya taarikh na tafseer. InshaaLlah waliozama zaidi kwenye bahri hii watatufunza zaidi.

    MwenyeziMngu atupe barka za Ashabu-l-Kahf, watu wakubwa mbele ya MwenyeziMngu.

  2. siri 01/01/2013 at 9:58 mu ·

    Hili ni moja kati ya makosa makubwa ya SMZ kuwadhararu walimu baada ya mapinduzi wakawa wanawapa mishahara mbuzi huku wakisema anayetaka asomeshe asotaka aondoke.
    Mwalimu wangu alisha kusomesha form 6 pale Lumumba ili akagombee Uwakilishi wa CCM kwani alisema huko ndiko kwenye Maslahi yake. Walimu wengi walikimbia dhiki iliyotetwa na Mungano wakakimbilia dunia nzima. Cha ajabu wengine walikimbilia maskuli ya Binafsi ya bara ambapo walipokelewa vizuri na majumba kupewa!! sisi tukabaki kufeli kwa kukosa walimu bila serikali kujali. leo nchi zote zenye maendeleo kama UK uwalimu nisawa na daktari ni kazi zenye mishahara mizuri.
    SMZ ipo na siasa za chuki na ubaguzi hawjui kama tunazama na tutazama wote pamoja na wao!! wasidhani kuwasomesha watoto wao nje ndio wao wamewahii laaa . kumsomesha mtoto ulaya ni kumtoa sadaka kwa makafiri kwani ndio sababu yako kukatikiwa na kheri atakuwa kafiri kuliko makafiri !!! utakufa hata dua hutoipata milele kaburini. Watoto kupotea ulaya ni jambo linalotumaliza kuliko njaaa. Hakuna kheri huku kwa watoto seuze watoto wawakubwa wanaopelekwa boading hufanya watakalo kwani hakuna kugombwa.

  3. Kishanshudas 01/01/2013 at 11:06 mu ·

    Kwa mara ya mwanzo nataka kuchangia mada hizi za Stonetown. Kusema kweli uliyoyasema Stonetown ni mambo ya maana sana. Lakini kwa Wazanzibari na wachangiaji wengi hili watalidharau kwani macho yao yanaangalia upande mmoja tu; jazba na chuki. Ingekuwa makala hii inashabikia chuki ungeiona imeenda ‘viral’ kwa sekunde sita tu. Lakini kwa vile ni ya Ukumbusho hakuna anaejali. Ndio sis wazanzibari tulivyo.

    Hivi sasa tumeghafilika tunapigania Muungano bila kujua tunalotaka. Maana tulikubliana hatuutaki, alipokuja warioba tukasema wa Mkataba. Fujo tu, hatuna moja tulitakalo sisi ni waja wa tabu tu. Tumeshika kuubwa la Muungano, wakati haya madogo kama aliyoyazungumza Stonetown, ni muhimu mno pia na hayahitaji vikao, ni maamuzi tu na shindikizo letu kwa Serikali. Hatufanyi pia.

    Endelea kuuelimisha Stonetown, bila shaka watatokea wenye akili wakufahamu. Si lazima uandike kusifu CUF na kutukana Muungano, mada kama hizi pia ni muhimu hata ikiwa hatupendi kuzisoma na kuzifanyia kazi.

    Kishanshuda

  4. HALIKUNIKI 01/01/2013 at 10:21 um ·

    Mwandishi umeona mbali,hata kiswahili pia jamaa zetu wa Tanganyika eti
    wao ndio wamekuwa walimu wetu,wakati ulimwengu mzima wanajuwa kuwa
    ukitaka kiswahili safi basi Zanzibar ndio makao yake makuu.

    Lakini ili jamaa zetu wahodhi kila kitu basi na hata kiswahili wanajifanya wao
    ndio magwiji na kuweza kututungia maneno ambayo hata aibu kusema.

    Kuna wakati niliwahi kusikia ya kwamba lilitungwa neno la kiswahili wakati
    ule Mh. Ali Hassan Mwinyi, ndie alikuwamwenyekiti wa baraza la kiswahili na
    kulipinga neno hilo.

    Kwa kifupi walitunga neno ili kukipa kile chombo kidogo cha kuchongea
    penseli na kukipa jina la kifirio, ambapo kwa kwetu ni matusi makubwa ndipo
    mzee Mwinyi nasikia alilikataa hili.

    Kwa kifupi WAZANZIBARI tuamkeni na tuweze kuondokana na kunyang`anywa
    hata lugha yetu.

  5. salum almaawily 02/01/2013 at 5:44 mu ·

    As aleikhum wana mzalendo
    Katika suala hili mimi natoa rai kwa SUZA, kushirkiana na vyuo vya kigeni katika exchane programs za walimu wa Kiswahili ili waweze kupata exposure walimu wetu.Pia kufuatilia vitabu vya watunzi wa zamani kidogo mfano Mzee Gora Haji na wengine ili kazi zao zijulikane. Sisi wazazi ni muhimu kuwajengea utamaduni wa kujisomea hadithi fupi fupi watoto wadogo kwani hapo ndipo penye chimbuko la mtoto kuweza angalau kutofautisha kati ya L na R na misamiati ya kiswahili chetu khalisi.

  6. Makame Ame 02/01/2013 at 7:10 mu ·

    Kwani Kiswahili ni cha Wazanzibari au Waswahili? Ikiwa ni cha Waswahili basi Lahija zote za Kiswahili zina haki nayo, hiyo ikiingiza lahija ya kimvita, Kitanga, Kipemba, kibagamoyo, Kilindi, Kitumbatu, Kikojani, Kimakunduchi, KiPaje, kiNungwi, Kimjini na wengineo walio WASWAHILI.

    Bahati lahija ya Kimjini (Zanzibar) ilifanywa ndiyo standard na Waingereza…au tuseme ndio kigezo chema. Lakini ubaya wa mambo hicho kimjini sasa kimekuwa kimezikwa na ubara. Kwa mfano si ajabu kumsikia mtoto akisema salasini badala ya thalathini. Hili ni sababu ya kukosa tarbia (malezi) njema ya lugha.

    hilo ndilo la kwanza. Pili, lugha yenyewe imetekwa nyara na watu wasio Waswahili na kukifanya ni chao kwa vile kina status ya utaifa na kukubalika ulimwenguni. Si ajabu siku hizi kusikia mtu anasema kamtu kale na kaladygay na kanini na kanini.

    Hii imepelekea kuwa lugha ya Kiswahili imekuwa ngumu hata kwa Waswahili. Hili mimi nalikumbuka nilipokuwa niko shuleni mimi mwenyewe sikwambii sasa kukiwa na maneno ya kiajabuajabu.

    Kwa hili rai ya kukisimamia Kiswahili na Waswahili ni muhimu. Lakini tupo?

  7. kitumbua 02/01/2013 at 12:17 um ·

    Ni kweli jamani, tumejipwetekeza sana kwa hawa watanganyika, hivi kweli kila kitu ni wao tu sisi hatuwezi! Ni dhana potevu, bado tunaweza endapo tutakuwa tayari wazanzibari. Tunaweza kuandika kamusi yetu yenye lugha fasaha inayoendana na mila na desturi zetu wazanzibari bila ya kutegemea wao tanganyika. Tutakua na Kamusi yetu ya Zanzibar na Kamusi yao ya Tanganyika.

Comments are now closed for this article.