Wakati ndio unaosema na kuamua

Written by  //  12/07/2012  //  Makala/Tahariri  //  Maoni 1

Na Juma Mohammed

Nyota njema huonekana alfajiri, ukiona alfajiri imeingia upeo wa macho yako huoni nyota ni kiwingi kitupu kimetanda kaa ukijuwa kuwa mambo kwako sio mazuri kajipange upya kimkakati. Kinyume na matarajio ya walio wengi, Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeanza kazi kwa wananchi wengi kujitokeza kutoa maoni yao kwa amani, utulivu na ustaarabu mkubwa kwa upande wa Zanzibar.

Nimebahatika kwenda katika mikutano kadhaa ya Tume hiyo, watu ni watulivu na kwa hili lazima niwapongeze wananchi kwa uugwana wao maana siku zote muungwana ni vitendo.

Jambo moja ambalo nimejifunza wakazi wa vijijini wamekuwa na uelewa mkubwa wa mambo, pengine kuwashinda hata wale walioko maeneo ya mijini, wanajenga hoja katika maoni yao na kutoa mifano hai.

Wakati huu wananchi wakiwajibika kwenye Tume kutoa maoni yao,hatutegemei kuzuka watu au kikundi cha watu kikawa kinaifuata Tume kila inapokwenda, hii sio sahihi, wewe kama ni mkazi wa Fujoni subiri zamu ya eneo lako itafika, ikiwa eneo lako Tume imeshapita umetoa maoni hakuna kuwabughudhi wengine.

Kama walivyoonesha uungwana watu wa Kusini Unguja, tunataraji maeneo mengine kuendelea kuiga mfano wa ukomavu wa demokrasia maana katiba inayokusudiwa kuandikwa ikiwa itaridhishwa na umma ni yetu sote sio ya viongozi wala vyama vya siasa,wasomi au matajiri.

Ilivyokuwa katiba ya nchi katika nchi yoyote ya kidemokrasia, ni mali ya wananchi wenyewe na hivyo ni wananchi pekee ndiyo wenye haki ya kubadili katiba ya nchi yao, haipendezi kutokea watu wakijigeuza mawakala wa kuwafunza watu nini cha kusema katika Tume,kila mmoja na mawazo yake.

Ni hivyo basi, katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mali ya Watanzania na si vinginevyo, ni wananchi wenyewe kwa umoja wao ndio pekee wenye haki ya kuibadili katiba ya nchi yao hivyo kutofautiana kimtazamo sio dhambi.

Yafaa kukumbuka kuwa Katiba inayokusudiwa kuandikwa Tanzania ni ya nchi kamwe si ya chama tawala cha CCM, CUF, CHADEMA,NCCR MAGEUZI,UDP,TLP, AFP nakadhalika, hivyo si sahihi suala la mabadiliko ya katiba likavaliwa njuga kwa kuifuata Tume ya Katiba kila iendako hata kama si mkazi wa eneo husika.

Vijiji ambavyo watu wake wametoa maoni, wamelitaja suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambapo wengine wakitaka Mabadiliko ya muundo uwe wa mkataba , wapo waliotaka muundo wa sasa wa Serikali mbili kuendelea,wapo waliotaka Serikali tatu,wapo wanaotaka Serikali moja.

Kuwepo kwa maoni na mitazamo tofauti kumetupa nguvu sisi wengine ambao awali tulidhani tuwapweke,kumbe tunawenzetu ambao imesadif mawazo yetu kama yao ingawa si kwa maeneo yote,lakini tumo tunaelea jahazi moja.

Hapa nikakumbuka kauli mbiu sio ile ya Uamsho ya “Tuachwe Tupumuwe” ni ya timu pendwa ya soka Uingereza Liverpool ambayo kauli mbiu yao ni “You will never work alone” Kamwe hutatembea peke yako.

Wakati ule nilifikiri kuwa yote yaliyo azizi au bora kwa mwanadamu ni matendo yake aliyotenda zamani nikasema sisi wengine hatujakula chumvi nyingi kwani hatukutenda lolote kwa ujana wetu,nilijihisi kuwa masikini,lakini fikra hizi sasa zimeanza kubadilika maana ubora wa mtu unaweza kuwa katika wakati ujao tutakaposhuhudia mabadiliko katika Muungano wetu.

Ilivyokuwa maisha yangu bado mapya na matumaini yakisheheni kila uchao sitaweza kubakia katika ukale ingawaje tunaaminishwa kwa msemo kwamba yakale dhahabu,lakini yafaa kutambua kuwa si kila ya zamani ni dhahabu.

Kawaida jambo la bahati mara nyingi hukawia, kwa maana yengine bahati haina miadi kama tufanyavyo binadamu, kwa miaka mingi wananchi tulingoja bahati ya kuandika katiba mpya, sasa bahati imetokea na kwa kuwa tulikuwa na shauku ya jambo lenyewe hatutazembea wala kuipoteza hidaya hii kwani kila jambo la kheri linakwenda kwa kheri.

Mara zote wakati ndio unaosema na kuamua ni kama maji kupwa na kujaa, huwezi kuyazuia wale waliotegemea kuzuka kwa makamio yasiyokuwa na tija wamebaki vinywa wazi maana kila mmoja anapewa haki ya kutoa mawazo yake na jambo la kupongeza hakuna anayebeza mawazo ya mwengine,si Wajumbe wa Tume wala watoa maoni wengine.

Katika baadhi ya mikutano hiyo wapo waliotaka katiba mpya iweke kifungu cha wananchi kuwawajibisha Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ikiwa wapigakura wataona uwakilishi wao kwenye vyombo hivyo hauna tija waweze ama kumsimamisha kazi au hata kumfukuza.

Wapo waliotaka kiwepo kifungu kinachotambua zamu za Urais katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakiwa na maana kama kipindi hichi Rais katoka upande mmoja wa Muungano,kipindi kinachofuata atoke upande mwengine.

Ama kweli kama kusemwa ni mauti sisi wengine tushasomewa hitima maneno hayo yamo katika wimbo wa Dua la Kuku ulioimbwa na Spice Modern Taarab ikiwa jibu la wimbo wa fimbo ya Mungu ulioimbwa na Kundi la Taarab la Zanzibar One.

Hatushindwi kushona tanga wala kuiunga heza maana unahodha ni kazi yetu hakuna moja litakalotushinda ndio maana tumekuwa tukieleza bayana misimamo yetu katika suala zima la kupata katiba mpya, hatusubiri maoni ya kupewa kwenye bahasha tukayafanya ya kwetu maana Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa aliwahi kusema “Binadamu wote hatuwezi kufikiri sawa” basi na katika hili la muundo wa Muungano lazima kutakuwa na mawazo tofauti.

Hatutaweza kuwa kama Kinyozi aliyekuwa akilia yeye na mnyolewaji maana yule anayenyolewa yawezekana akawa anaumia,lakini huyo mnyoaji je kakumbwa na nini wakiulizwa ndio kwanza unazidisha kilio!

Hizi sio karne za ujinga au ukifuu tundu na wala sio zama za mtu kujifanya mbabe au mzalendo zaidi kupita mwenzake,kujifanya Senior Citizen, karne hii ya 21 ni ya watu kutendeana wema hisani na upendo,ni karne ya majadiliano katika kufikia maafikiano(consensus).

Kuwa kwangu muumin wa Muungano wa mkataba sio dhambi kwa Mwenyezi Mungu wala Serikali maana mamlaka ya uendeshaji nchi ipo mikononi mwa wananchi wenyewe, haijuzu kuzuka watu walikozuka kuanza kunyoosheana vidole, ushabiki wa vyama ni wa kupita tu ni sawa na wa mpira wa miguu, ziko wapi Cosmopolitan, Malindi, Taifa ya Jang’ombe, Muembe Ladu,Ujamaa, Nyota Nyekundu,Pani Africa na nyenginezo?

Vyama vya siasa ni kama ndege anayetua tawini,lazima aruke washahiri wengi wamelisema hilo nami nalirejea kwa muktadha wa mambo ya msingi katika nchi hayategemea ushabiki wa kisiasa,yanahitaji umoja na mshikamano zaidi maana tunaweza kuishi bila vyama vya siasa,lakini hatuwezi kuishi bila nchi.

Siku za hivi karibuni kulijitokeza wanasiasa waliovaa majoho ya Ujaji kwa kutoa hukumu kwa raia wenziwao wenye kutofautiana nao kimawazo. Utawasikia “huyu sio mwenzetu” Hapo tena wanabishana wenyewe kwani wewe humjui yule si fulani yule ni Hizbu tangu zamani(Hizbu ni kilichokuwa Chama cha Zanzibar Nationalist Party-ZNP kabla ya Mapinduzi).

Badala ya kujadili hoja iliyotolewa wao wanajadili watu kwa kuwanasibisha na vyama vya zamani ambayo haviwezi kuibuka juu katika bahari mpya ya siasa za kileo zenye kuhitaji umakini na weledi katika uwanja wake sio kuendesha siasa kwa mazoea ya kurithi maana waswahili wanarithi kila kitu.

Katika hili la kuwa muumini wa Muungano wa mkataba nisingelipenda kuwa mtazamaji wakati wananchi wenzangu wakijitokeza hadharani,lakini hatujawafunga mdomo waumini wa aina nyengine ya muundo wa Muungano nao kujimwaga kiwanjani kwa msingi ule ule wa ushawishi wa hoja na sio kejeli,vijembe au jazba.

Siku za nyuma niliwahi kusema kuwa kama muundo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ungelikuwa ni jahazi basi jahazi hilo limeshafika ufukweni ikiwa na abiria waliosafiri kwa muda wa miaka 48 je,abiria hao watabadili tanga kukabili upepo wa kusi au watakwenda na tanga bovu na foromali chakavu?

Kitandawili hicho kitaaguliwa katika kura ya maoni hapo baadaye wakati rasimu ya katiba itakapopigiwa kura na wananchi, wanaikubali au la.

Njia hii ya kura ndio sahihi kuliko zote kwani Mwenyezi Mungu ameuzidisha wepesi wa kubadili mambo kwa kumpa fikra mwanadamu kubuni kitu kura ambacho mara nyingi wapigaji kura wanatumia kijipande cha karatasi kufanya maamuzi.

Wataalam wa mambo ya siasa wanasema kwamba umuhimu wa kura unawafanya viongozi waliomo madarakani kuheshimu kazi na kuwaheshimu wananchi wenzao kwani iwapo watawatendea mabaya itapofika siku za kupiga kura bila shaka watawanyima kura hivyo madaraka yatawatoka.

Mara nyingi njia ya kura huleta heshima katika nchi baina ya watawala na watawaliwa hivyo tunategemea sana siku ya siku kura ya maoni kuamua kama tuwe na Katiba mpya au iliyopo iendelee ama inaweza kutuletea heshima au kutuvunjia heshima mbele ya walimwengu.

Jambo la muhimu ni kila mtu kuwa huru kutoa maoni yake bila jazba wala soni, ikiwa huwezi kutoa maoni yako ni bora kukaa kimya kuliko kutumiwa na wewe ukatumika maana siku zote wananchi walikuwa wakilalamika hatushirikishwi sasa mpira upo kwetu hakuna kutia kwapani wala kwa Yanga.

Kuhusu Mtunzi

View all posts by

Maoni yamefungwa.