URAIS MUUNGANO 2015- NI ZAMU YA ZANZIBAR
Written by Stonetown (Kiongozi) // 24/12/2012 // Makala/Tahariri // 13 Comments
Miaka mitatu kutoka sasa, Tanzania itafanya uchaguzi wake mkuu utaohitimisha miaka kumi ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete. Tanzania kama nchi nyengine duniani, inafata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Katika mfumo wa vyama vingi, na iwapo kuna demokrasia ya kweli, basi ni matarajio yetu kuwa chama chchote kitakachoshinda kitapewa haki yake na ridhaa ya kuongoza nchi.
Lakini pamoja na hayo, suali la uwiano wa Ugombea wa kiti cha Urais kwa pande mbili za Muungano, limekuwa likipuuzwa sana kuanikwa katika mijadala mbalimbali nchini. Suali la makubaliano ya mapokelezano ya wadhifa huu mkuu wa nchi baina ya sehemu mbili za Muungano, haujawekwa sawa na ni moja kati ya changamoto kongwe zinazoungana na mkururo wa kero za Muungano hapa nchini.
Tangu tuungane, ni miaka takribani 49 sasa. Wakati Zanzibar ikiwa na marais saba tangu 1964, Jamhuri ya Muungano ndio inatimiza nusu tu ya wale waliokwisha tawala Zanzibar, ikiwa na marais wane tu hadi sasa. Mara baada ya Muungano, Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalim Julius Nyerere, alishika hatamu ya kuiongoza Jamhuri hadi pale ‘alipong’atuka’ madarakani kwa hiari yake mwaka 1984/85.
Katika kipindi hichi cha miaka 20, Mwalimu hakuwahi kueleza wala kufafanua lolote kuhusu mpokezano wa madaraka kwa zamu baina ya nchi zetu hizi mbili. Naamini alifanya hivi sio kwa kutojua umuhimu wa kitendo hicho muhimu. Kitendo ambacho kingeashiria usawa mkubwa na haki inayosimamiwa na Muungano wetu. Mwalimu hakulijadili hili kwa sababu alijua wazi kufanya hivyo kungeviza ajenda yake binafsi ya kuimeza Zanzibar ndani ya matumbo ya Tanganyika na kuiondoa kabisa katika ramani ya dunia. Hili ndio lililokuwa lengo lake, bila shaka.
Mungu akikupangia nakama, huna ujuzi wala ujanja. Kwani hayati Sheikh Abeid Karume, ambae ndie aliyekuwa Rais pekee wa Zanzibar aliekuwa akithubutu kumhoji na kumjibu Mwalimu lolote, lakini lakuvunda halina ubani, Sheikh Karume alikufa mapema mno. Tena wakati huo anakufa, bahati mbaya zaidi, ilikuwa Muungano huu haujawa na sura mbaya iliyo wazi wazi kama sasa, japo kiwingu cha dalili hizo mbaya kilianza kuonekana kwa mbali. Sheikh Karume akauwawa, na sababu ya kifo chake, ikafikichwa fikichwa, kisijulikane cha ukweli hadi leo.Ni begeje tu. Na kwanini, watu washuhulike na hili wakati, kufa kwa panzi ni neema ya kunguru? Aliekufa ndio kafa!
Rais Jumbe, alijaribu kwa sana kuhoji hali kama hii. Lakini alichelewa mno.Na kwa jinsi Mwalimu alivyokuwa amejipanga kikazi kiulinzi na kiusalama, juhudi za Sheikh Jumbe zikawaka na moto. Zikaunguwa na kusakatuka kama kijungu cha dagaa tonge, kilichosahauliwa na mpishi aliekwenda kujisuka akisahau kuwa moto hauna sumile. Sheikh Jumbe akang’oka kama Mbuyu uliopigwa halbadiri ya mbayana. Akakunguzuka na mashina yake yote! Njia nyeupe!
Baada ya majaribio haya mawili ya kujitokeza kwa Wazanzibari waliowakijifanya hawaogopi kumuhoji Nyerere, kilichofata ni mpango wa kudhibiti nani awe Rais wa Zanzibar. Ikawa Rais anaewekwa huku kwetu si katika yoyote anaeweza kuuhoji wala kuujadili Muungano, ‘imma faimma’ Nyerere awe hai, au awe ameshakufa. Na hili likafanikiwa. Bahati nzuri tu ‘Mtu si mbwa’. Hawa unaowaona walihoji kidogo wakaitwa ‘samaki’ na wavyele wao, ni matokezeo tu. Kwani haki haizami na dhulma haidumu.
Viongozi wetu wa Zanzibar, ni watu waliopangwa maalum kufuata utaratibu waliopangiwa na wakubwa zao kule bara. Na kwa maana hii hakuna aliyewahi tena kuhoji kuhusu mgawano wa nafasi ya Urais wa Muungano. Ambapo, penye Uungwana na haki ndani ya Muungano huo, bila shaka tulikuwa tupokelezane zamu. Hata kama tuko katika mfumo wa vyama vingi kiasi gani.
Kwa upande wa CCM bara, hili walikuwa walione pia. Hasa wao wakiwa kama chama chenya nguvu na chenye kushika hatamu. Ipo haja, tena bila kuzozana, kuipa nafasi Zanzibar kuongoza katika Jamhuri ya Muungano, tena katika wadhifa wa Urais, jambo ambalo linaonekana kuwa zaidi ya ndoto ya ‘Alinacha’ kwa sasa.
Suali la kumpa Mzanzibari Urais wa Muungano ni ndoto ya Alinacha kwa sababu nyingi. Kwanza tuchukulie chama cha CCM kiwe na matumaini makubwa ya kushinda. Ukweli ni kwamba CCM na Muungano ni mtu na mama yake mzazi. Nasema ni mama kwa sababu hutokea watoto wasio baba kabisa, wala watu wengine, lakini hakuna mtoto asie na mama. Na mapenzi ya mama kwa motto hayana kifano chake. Na tunategemea vivyo hivyo kwa mtoto na mama yake. Kama haya ni kweli, na dhamira ya Muungano ni ile ile ya kuelekea nchi moja. Tena wakati ambao Wazanzibari wanahitaji ‘kupumuwa’ kwa nguvu zote. Hili ni gumu.
Isitoshe, ukiwauliza zamu ya Zanzibar lini, wanakujibu kuwa Mwinyi alikuwepo hapa. Hivi Mwinyi ni Mzanzibari? Kwa kigenzo kipi? Na haya naawe huyo Mzanzibari kama ataamuwa kujinadi hivyo, lakini sula linabaki kuwa Marais wawili sasa, yaani miaka 20, Urais uko bara. Kuna ubaya tena gani wakitupa tena kumi, kama kweli tuna nia njema?Hapa panahitajika tuwe wakweli wadadisi kidogo juu ya hili.
Ama kwa upande wa CHADEMA, naona wazo hili si mahala pake hata kidogo. Ingawa CCM na chadema lao moja, na ndio ukaona CHADEMA iliibuka tu kutoka katika ombwe, na kuja kuwa chama chenye nguvu hata kuliko CUF kule bara ambayo ilikuwa inaimarika vizuri siku hadi siku. Lengo, ni kuiondoa na kuizima nyota ya CUF kule wakiamini kuwa, kuanguka kwa CUF bara ni mafanikio makubwa ya kuzima nguvu ya wazanzibari kutaka kujitawala na ‘kupumuwa’. Na hili wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Kuna kila dalili kuwa CHADEMA, hawana mpango na Zanzibar zaidi ya kuimaliza zaidi. Na kama hili linasomeka hivyo katika ajenda zao za siri, hawana mpango wa kumpa Mzanzibari nafasi yoyote ile hata ya Ubunge sembuse Urais. Na hii ni kwa sababu moja kuu: CHADEMA ni wabaya zaidi kuliko CCM, kwani ubaya wao haujifichi. Isitoshe, mfungamano wao mkubwa na kanisa ambalo kwa kiasi kikubwa ndio linaloipa kiburi CHADEMA, unaifanya hali ya uwezekano wa Zanzibar wa kuwa na nafasi kubwa kama hio katika Muungano kuwa ya tembo kupenya tundu ya sindano.
Pamoja na hayo, tusikate tamaa. Ipo haja kwa kila mmoja wetu wakiwemo viongozi kuhoji nafasi ya Zanzibar katika uongozi wa juu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Ijapokuwa tunaonekana kukubaliana na kuridhika kabisa na kitazonge, na changa la macho la kupewa kwetu Umakamo wa Rais. Nafasi ambayo haina athari yoyote kwa taifa zaidi ya kufunguwa vikao, kujulia wagonjwa na kuhutubia mikutano ya mazingira na Ukimwi.
Pia tumeridhika na suala la Rais wetu kuwa Waziri katika Jamhuri ya Muungano, jambo ambalo haliingia akilini kabisa. Maana naamini wazi Makamo wa Rais bara, kiitifaki ni mkubwa zaidi kuliko Waziri, ambae pia ni Rais akiwa Zanzibar. Huu ni mchezo wa kitoto au wa kuku lala, tustiane majivu ya macho. Ukweli tunatakiwa tusitosheke na hapo. Tuhoji, tudai, na tutoe kauli moja, ‘Mara hii Urais wa Muungano, ni Zamu ya Zanzibar’. Tuwatazame na pumzi zao!
Natoa hoja



13 Comments on "URAIS MUUNGANO 2015- NI ZAMU YA ZANZIBAR"
kwa hili waTanganyika na CCM yao watahiyari wavunje Muungano kuliko kutawaliwa na waZanzibari.
Wao wameowa hawajaolewa…wake zao kina Sheni na Shamhuna wameridhia hili.
Ni wazo zuru watu kudai haki yao popote pale wanapoona wanadhulumiwa. Suala hili pamoja na mengine ambayo tunaona wenzetu wanatudhulumu ni mambo ambayo yalitakiwa yapangwe na kupangika tangu April 1964 wakati tunaungana ili kuwe na usawa unaoonyesha nchi mbili huru zimeungana. Na utekelezaji wa haki hiyo uwe unaangaliwa kwa macho mawili ili kuona haki inatendeka.
Lakini kwa namna mambo yalivyokwenda tokea mwanzo hayakuwa hivyo kabisa. Ni Nyerere kupanga na kutekeleza mambo anavyotaka yeye kwa nia ya kuhakikiha Zanzibar anaidhibiti kwa kila hali mpaka kuifanya ni kijiwilaya cha Tanganyika. Na hayo yote yakitenteka Wazanzibari wamelala usingizi hakuna anae hoji wala kudadisi mpaka leo tumefika hapa. Sababu ya Nyerere kujifanya yeye ndie mkubwa na kuwaadhibu watu wanaohoji haki ya Zanzibar ni kwamba makosa yalifanywa na Karume tangu alipounganisha bila ya kuwashirikisha wenzake ili kupata ridhaa na ushauri wa kisheria.
Sasa, dhana kubwa iliopo tokeo wakati huo mpaka hivi sasa, nikwamba viongozi wetu wa Zanzibar wanahisi kuweko kwao madarakani, kote Zanzibar na serikali ya muungano, ni kwa hisani kubwa ya Watanganyika na sio Wazanzibari waliyowaweka. Kwa hiyo wako tayari kutii amri zozote kutoka Tanganyika, ikiwa ni pamoja na kutokua na nguvu ya kuhoji dhulma zozote inayotendewa Zanzibar na Tanganyika.
Kwa mtazamo huo mimi naona hata tukapewa nafasi ya uraisi kwa kipindi cha 2015/2020, au rais wa Zanzibar kuwa makamo wa raisi kama tunavyodai, hapatopatikana faida yoyote kwa Zanzibar kwa sababu ni wazi kwamba mawazo yao yote yatakua ni kuitendea wema Tanganyika ili awamu ya pili Watanganyika wamuone anafaa kuendelea kwa sababu anatekeleza maslahi yao.
Nasema hivyo kwa sababu tunao msururu mkubwa wa Wazanzibari walioko kwenye serikali ya muungano – Bilali, Suluhu, Nahodha, Khatibu, Sheni na kundi la Wabunge lakini hawana ubavu wa kusimamia maslahi ya Zanzibar. Je ni kitu gani kinachowafanya watu wafikirie kwamba raisi wa muungano akitoka Zanzibar Wazanzibari watapata haki zao katika muungano?
Kwa mawazo yangu mimi njia peke yake ni kuachiwa tupumue.
mie kwa muona wangu hapa naona hata huo Urais wa Jamhuri wa muungano tuachane nao sisi ni nchi kwanza baada ya hapo ndio tujadili huo uraisi wa muunagano kwani tukidai huo tutaonakana kuwa tunaupenda muungano wa kufumaniana kwani hao waliofungisha hii ndio hawapo tena duniani..
znz kwanza inshallah
@kamanda Sadaqta maneno yako100%. Tunautakia nini huu urais wa Tanzania? Si ndio kuonyesha bado tunaung’ang’ania na kuuhitajia huo muungano.
Alipokuwa Mwinyi Rais wa Tanzania, Zanzibar ilinufaika nini? Walionufaika ni Bara kukombolewa na Mzee Rukhsa kibiashara na kiuchumi baada ya kubanwa miaka na Nyerere.
Zanzibar huru,sovereign itakuwa na Raisi wake period.
Watanganyika wacha wamchaguwe Raisi Mbara-Mwitu wamtakae.
Watuachie vyetu tumpumue.
Well said Kamanda,sioni haja ya mzanzibari yoyote kupiga kura ya kuchagua Rais wa Muungano huu uliopo,hatutaki ,akiwa Mzanzibari akiwa Mtanganyika ikiwa Rais wa ZNZ anachaguliwa Bara na hana faida na WZNZ atakuwa na faida Wa Muungano,Tuangalie mbele urais ubunge yote ni maslahi binafsi sioni hata haja ya kuitwa moja kati ya kero cause halina faida na Wananchi ila individual tu.Kero ni Zanzibar kuwa huru kwanza kupigia kura Muungano ni sawa na Chichidodo,which hates shits but feed from the maggots which grow in the toilet.i.e kupigia kura ni kukubali hali tuliyonayo na jitihada zote ni sawa na kelele tu
Well Mimi naona kila kinachowezekanwa kudaiwa tusikae kimya. Kila kona lazima tuangaze tutoe hoja na madai yetu
Mie sina interest na hili kwani tatizo sio kupewa mzanzibari bali ni kupewa alochaguliwa na wanachi kwa mfano tuseme apewe Bilal , sasa sie wazanzibari ndio kweli itakua tumefaidika? kama mtu ana maneno basi waache wampe Lipumba au Seif Sharif waone mbona they will never dare on that.
Hapo umesema Star, Zanzibar hainufaiki na viongozi wake kwa sababu sio chaguo lao ni chaguo la dodoma. Ikiwa Rais anaechaguliwa na wazanzibari ndie anaepewa uraisi basi angewaheshimu wale waliomchagua lakini anajua hata mkamkataa nyote wakati watanganyika wanamtaka atakuwa raisi tu, na wengine ndio maana wakathubutu kusema kura yake na ya mkewe tu zinatosha kumuweka madarakani.
Jamani suluhu hapa nikuwakama viongozi wetu na kuwambia sie twacaguwa Rais wtu wa zanzibar tu kama watanganyika watachaguwa watanganyika kama wanavyochagua mtanganyika sie nakura ya watanganyika basi kama zanzibar ni nchi tuhamasishane kwa hilo
kwani kupiga kura kunawapa kiburi cha kuzidi kutunyonya
mzalendo sasa kwenye android http://www.appsgeyser.com/getwidget/mzalendo/
Msipoteze mda wenu wana mzalendo hata kama Wanamwezi watachagua Rais basi atakua kama kina Sheni na Seif IDDI.
Ni mizombi iso kua na mfano na hawana Uzalendo wala hawa kuzaliwa Zanzibar na Hata kama atachaguliwa Rais mwenye Asili ya Zanzibar basi watanganyika wata mchagua mtu kama borafya aiumize Zanzibar Zaidi kwa manufaa ya matumbo yao.
Kwani kuna Ulazimu gani wa Muungano usio kua na mapangilio wala nidhamu?
Cha kupiganiwa ni kura ya Maoni kuulizwa wa Zanzibari juu swala la Muungano na sio kuchaguliwa kuwa Rais wa Muungano.
tukae tukijuwa kuwa binadamu hamuna kitu , roho ni mali ya Allah na anaweza kushukuwa wakati wowote apendapo mwenyewe, tulikuwa nae Mh Idrissa abdullwakili leo hatuko nae.
Jee viongozi wetu wanapo tembelea makaburi ya wenziwao ,jee hupata hisia kuwa kifo kitamkuta kila mtu wakati wwte ulo M/mungu apendapo?
http://othmanmapara.blogspot.ie/2012/12/dk-bilal-aendelea-na-ziara-ya.html
hatuna haja ya uraisi wa muungano tunahitaji dola yetu huru, na hata hapo ikiwa haiwezekani ikabidi waka-compromise mambo ya muungano basi raisi AWE DR. AMANI KARUME.