Sera zimeua malengo ya uhuru, mapinduzi

Written by  //  02/03/2017  //  Makala/Tahariri  //  Maoni 4

nyerere_with_karume

Na Juma Duni Haji

MARA tu baada ya uhuru wa Tanganyika 1961 na Mapinduzi ya Zanzibar 1964 viongozi waligeuka manabii. Wakaacha wananchi wawe kama mbilikimo wa majaribio ya siasa. Taifa lilianza na siasa ya ujamaa na kujitegemea kupitia Azimio la Arusha, ambalo lilishindwa na kuja kuuliwa na Azimio la Zanzibar.

Azimio la Zanzibar la mwaka 1991, liliacha viongozi kujitajirisha na kuigeuza rushwa ni takrima. Ilikuwa wakati matajiri wakubwa walipojibuka na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kugombea nafasi za ubunge na nyadhifa nyingine za kisiasa. Baadhi yao wakawa wafadhili wa chama.

Taratibu, ikaonekana miiko na maadili ya uongozi ikafifia. Wakati uhuru ulitafutwa ili watu kujitawala, miaka 55 baadaye, hali inaonesha utegemezi wa misaada na mikopo ndio ada. Bei kubwa za vyakula sokoni, matibabu na elimu duni, uhaba wa chakula, mahitaji ya haki za msingi kwa binadamu, ni ushahidi wa wazi wa kiwango cha umasikini.

Taifa lilianzia na TANU/ASP kabla ya kuja CCM vilipoungana mwaka 1977. Mwaka 1967 serikali iliwapeleka watu maporini kwa nguvu katika walichokiita kujenga vijiji vya ujamaa na kujitegemea. Takriban vijiji vyote vimekufa na havitajwi katika sherehe za uhuru au inapoelezwa nchi imepata maendeleo.

Palikuwa na zawadi maalum kwa kijiji bora. Hapa viongozi wa nchi walitumia umma kujaribu itikadi yao. Waliwafanya mbilikimo, ujamaa vijijini na azimio la Iringa la siasa ni kilimo. Katika kutekeleza sera hiyo, wengi waliliwa na simba.

Waliomiliki vitu au mifugo michache walinyang’anywa kwa kuitwa manyang’au au mabepari uchwara. Mali na majumba ya jamii ya Wahindi vikataifishwa, mwishowe wakauziana wakubwa chini ya usugu wa wahafidhina wa Serikali ya awamu ya tatu, na askari wake wa mwamvuli.

Ikabuniwa sera ya elimu ya kujitegemea iliyozaa jeshi la Wamachinga. Pakaja UPE au ‘Usome Pasipo Elimu’ kama wanavyofanya mradi wa shule za msingi (MMEM) na sekondari (MMES). Matokeo ya majaribio hayo yanaonekana sasa miaka 15 hadi 20 baada ya uharibifu. Leo wengine wanatiwa hatiani eti kwa nini watoto wa mkoa au wilaya nzima wanafeli. Lazima awepo mnyonge wa kulaumiwa.

Miaka ya awali kulikuwa na mipango ya muda mrefu na mfupi ya miaka mitano mitano na ya mwaka mmoja mmoja. Kila miaka mitano tulijipima kwa vigezo vya makadirio ya kila mwaka mmoja. Tukafika mahala tukaiacha na kupata ushauri wa Benki ya Dunia na kuanza na mpango wa kurekebisha uchumi ulioitwa Structural Adjustment Program (SAP). Mipango hii ililenga nchi zilizokuwa masikini zaidi.

Baada ya miaka kupita na kutoonekana mafanikio, wakubwa wakaleta mpango wa kufufua uchumi ambao uliposhindwa, ukaja mpango ulioitwa Annual Rolling plan uliohusishwa na mkutano mkuu wa wafadhili na nchi zinazofadhiliwa jijini Paris, kwa jina maarufu la “Paris Club.”

Mipango yote ilishindwa kusaidia kubadilisha maisha ya Watanzania. Mwishowe majina ya mipango yenyewe yakabadilishwa; badala ya kuiita “mipango ya uchumi” tukaanza kuiita Mipango ya Kuondoa Umasikini. Kumbe watawala walishajua umasikini waliouandaa unahitaji kuwekewa mpango wa kuuondoa. Walipojua kwamba ni silaha nzuri ya kuitumia kuendelea kutawala, wakaubadilisha jina na kuuita mpango mkakati wa kupunguza umasikini. Na mwishowe ukaletwa Mkukuta na Mkurabita, majina yasiyoeleweka hasa maudhui yake.

Rais Jakaya Kikwete akaleta nyongeza yake ya “Mabilioni ya Kikwete” ambayo ni fedha zilizomwagwa kila mkoa na kuliwa na wenye meno huku wenye moyo wakiendelea kunuka umasikini. Kabla ya Kikwete kumaliza muda wake, akaleta Kilimo Kwanza, pasina kuzingatia kuwa siasa ni kilimo ya miaka ya 1970 ilishashindwa miongo miwili nyuma.

Katika kuendelea kutengeneza umasikini zaidi, akaja na mpango ulioitwa “mafanikio makubwa sasa (BRN)” wakiiga programu ya serikali ya Malaysia. Ili kujaribu kuonesha kama wananchi na hasa wakulima wanasaidiwa na serikali, yakaingizwa matrekta mageni kutoka India, ambayo hayakuweza kusaidia.

Pamoja na yote hayo, jamii kubwa imezidi ujinga, umasikini, maradhi yaliyosindikizwa na janga la ukimwi na kipindupindu kinachotokea wakati wa kiangazi kwa kunywa maji yenye uchafu. Tunapaswa kuona aibu kwa kushindwa kwa miaka 55 kupanga jinsi ya kupata maji kwa mji mkuu wa nchi. Mji Mkuu wa nchi watu kuishi kwa maji ya visima vinavyochimbwa kwenye mitaro ya vyoo ni aibu ilioje?

Matokeo ni jeshi la machinga linalopambana na askari wa jiji kujitafutia mlo mmoja kwa siku; Jeshi la watoto wa mitaani wasio malezi ya wazazi na kuzaa jeshi la majambazi; Jeshi la kinadada wenye kuuza heshima zao bila kujali ukimwi.

Jeshi la mayatima wenye kuzaa mayatima wenye kuzaa mayatima kwa sababu waliachwa mayatima kutokana na wazazi wao waliofariki kwa ukimwi; na hatimae kubaki masikini, wenye maradhi na ujinga unaolazimisha kubaki wavaa mitumba huku wakishindwa kumiliki hata mlo mmoja kwa siku.

Miaka ya awali ya 1970 na 1980 Watanzania walifika mahala wakakosa hata nguo za kuvaa. Kule mikoa ya kusini walikuwa wakivaa viroba vya magunia ya mbolea. Wakati huo kupata mahitaji ya lazima kama sabuni na vifaa vya matumizi ya nyumbani sharti uwe na kitambulisho maalum.
Vyama vya ushirika vya wananchi vilivyokuwa vimefanikiwa sana, vikavurugwa na kuvunjwa na kufanywa idara za TANU/CCM.

Baada ya viongozi kukosa la kufanya, wakaibuka na operesheni ya kuhujumu uchumi. Wananchi wakanyang’anywa mali zao, wengine wakawekwa kizuizini kinyume cha sheria. Hofu iliwajaa wananchi mpaka baadhi yao wakatupa mali zao misituni. Sheria ya kuhujumu uchumi ikapelekwa na kupitishwa bungeni baada ya hujuma dhidi ya wananchi kufanyika.

Kwa kiburi, CCM na serikali zake zikabaki hazina jibu. Pamoja na hali hiyo bado wakajigamba hawatageuka jiwe (hawatabadilika). CCM ikageuka jiwe na ikakubali kushauriwa na mashirika ya kimataifa ya fedha, ikaanza kuuza kila kitu (kwa kisingizio cha ubinafsishaji) huku wakiendelea kujigamba siasa safi ni ya ujamaa na kujitegemea.

Wakaanza kuuza kampuni za madini za umma kwa bei ya chini, wasijali maslahi ya Watanzania wanaoishi jirani. Wakaendelea na kuuza vipande vya ardhi vyenye madini. Wakafikia kiwango kuuza mchanga na kuupeleka Ulaya. Wakauza kwa bei ya kutupa mashirika yaliyoshindwa. Wakaendelea kuuza mpaka yale yasiyoshindwa. Pamoja na jitihada kubwa za Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, kutaka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) isiuzwe, ikauzwa bei ya kutupa ya kuua uchumi wa nchi mwishowe wakawa watetezi wakubwa wa ubepari ambao awali waliuita ni unyama.

Wakaita “Ubinafsishaji kuwa ni sera ya taifa kumbe ni ugenishaji,” hali ikawa mbaya kufikia rais kufungua ofisi ya kampuni yake ndani ya Ikulu na wengine wakitetea kuwa ni sawa. Hadi sasa bado takriban asilimia 35 ya bajeti inategemea misaada na mikopo. Azimio la Iringa la siasa ni kilimo limeshindikana kutekelezwa kama lilivyoshindwa Azimio la Arusha na kila kipindi cha miaka mitatu au minne kunatokea janga la njaa na kuomba msaada wa chakula.

Mwaka huu tumekataa njaa kama kwamba ni mara ya kwanza tatizo hilo kutokea. 1974 ilipotokea njaa kubwa Mwalimu Nyerere alitangaza sera ya mpito ya kilimo cha kufa na kupona. Leo miaka 55 baadae bado tunapata majanga ya njaa na wananchi kula mzizi kwa kukosa akiba ya chakula. Mfumo wa utawala wetu ni kwamba haufanyi makosa.

Kuhusu Mtunzi

View all posts by

Maoni 4 katika "Sera zimeua malengo ya uhuru, mapinduzi"

 1. zamko 03/03/2017 kwa 10:24 mu ·

  @ BABU JUMA DUNI Rehma na Amani ya Allah Iwe Juu yako.

  Heko kwa Kipande kikali sana ulichokitoa hapo Natamani Nikubebe Mgongoni kwa Ulivonikumbusha UTUMBO na MAKOSA YA SERIKALI YA CCM na Makosa haya yamegeuka Maradhi ya Kuambukiza na Kutapakaa Kule Zanzibar hasa baada ya Muungano wa TANU na ASP.

  Kinachonishangaza Watanganyika Walio Wengi Sana ( Tena Wengine Wanajiita Wasanii) Miaka hio yote 55 bado Wanaiona CCM ndio Chama Na Serikali Yake Ndio Inayoongoza Vizuri kwa Amani.

  Watanzania Wanaliwa Mali zao na Mfumo Wa Ufalme Wa Kimla kwakuhubiriwa Amani na Utulivu. Kwakuongeza tuu nikwamba Ule Mpango wa Kilimo na Uagizwaji wa Matractor Uliofanywa. Matrector Yote Yalikabidhiwa MATAWI YA CCM.

  NA CCM WALIPOKABIDHIWA MATRACTOR YA KILIMO Wakaanza kuuza huduma kwa Mwana CCM tuu- Ikiwa Wewe sio Mwana CCM hata kama unalima ekari ngapi na na unataka usaidiwe kwa malipo basi Tractor Linakupita na kwenda Kumlimia Karda wa CCM. Haya nimeyaona kule Pemba walipouziwa Matractor Mabovu Kutoka Tanganyika na Masheha kuyahodhi kama mali zao.

  Tusipobadilika CC Wananchi Tukaidai Haki Yetu kwa Nguvu za Umma naamini CCM Itaendelea kutunyonya mpaka siku yakutiwa kaburini-

 2. mzeekondo 03/03/2017 kwa 1:53 um ·

  Naungana na @ Zamko hapo juu katika kukushukuru sana Mh. Juma Duni kwa maandiko matakatifu haya tuliyowekewa hapa kwa hisani ya Mfroasty (ufundi}. kwa wenye umri mdogo wanaweza wakaelewa vifungu fulani fulani tu,lakini kwa sisi watu wazima hizo kumbukumbu zote ulizoziweka hapa bado ziko vichwani, ingawa wengine tulikwisha sahau wewe umetuamsha na kututahadharisha kuwa hapa hakuna jipya huu ni mlolongo wa siasa za ujamaa na kutegemea watu wanyonge miaka nenda miaka rudi.

  Nchi hii imepitia majaribio ya kutosha katika kutafuta nisichokijua,niliwahi kunena kuwa hata huyu JPM mtawala wa leo wa Tanganyika, hana wala hatokuwa na jipya,anarudia yale yote yaliyokwisha kufanywa na kufeli na kina Sokoine,Mrema,Kawawa,Nyerere nk.

  kujitutumua ndio kauli thabiti ya siasa zetu,Inshaalah salama.

  Hongera mzee Duni.

 3. SHAKUSH 04/03/2017 kwa 4:30 mu ·

  Ahsante mzee Kondo kwa kuchangiya. Shkamoo.

 4. mzeekondo 04/03/2017 kwa 10:16 um ·

  @Shakush

  Nakuitikia na kurudisha mzee mwenzangu,ni matumaini yangu ya siku zote kuwa unaendelea vyema katika afya,kipato,sala pamoja na shughuli zote za aila yako pamoja na wale wote mlioshibana.tusiwasahau pia wale wote ambao bado tuna hitilafiana nao, katika kuombeana mema ili sote tuwe pamoja katika kheri na amani ya kudumu.

  Ama zaidi ya haya itakuwa nasema uongo, kama nitaendelea kuhuruju, basi ni lazima au wajibu niweke kalamu pembeni kwa sasa,Inshaalah tutawasiliana zaidi siku zijazo.

  “UUNGWANA SI KAULI BALI NI NIA.”

  Nakushukuru,hicho kipande hapo juu nakuachia zawadi tu.

Comments are now closed for this article.