GOYA LA MZALENDO: ‘MUUNGANO UNA FAIDA ZANZIBAR’

Written by  //  23/12/2012  //  Makala/Tahariri  //  22 Comments

Katika harakati zangu za hapa na pale nimefikia pahala nikaona ipo haja ya kuanzisha jamvi la hoja tete hapa Mzalendoni lijulikanalo kama ‘Goya la mzalendo’. Katika jamvi hili nitakuwa nikizungumza mada tete na zenye mushkla katika jamii ili kuweza kupata taswira halisi ya fikira za wasomaji juu ya mada hizo nitazoziabiri kwa upana katika kijamvi hiki. Naishukuru mzalendo kwa kunipa kijikataa cha kuchapishia makala hizi. Shukran.

Wiki hii ‘Goya la mzalendo’ litaabiri na kutathmini kwa mapana faida za Muungano kwa Zanzibar na hasara za kuukata kwake iwapo wazanzibari wataamua kufanya hivyo. Mada hii inakuja mahali muafaka ambapo siku za hivi makaribuni tu tutaweza kuupata msimamo wa jumla wa maoni ya watu wa Zanzibar juu ya Muungano upi wanaoutaka.

Wakati kijungu hiki kikikaribia kuepuliwa baada ya kupwaga kwa muda sasa, kuna kila dalili kuwa Wazanzibari walio wengi hawaridhishwi na muundo wa Muungano uliopo, na wengine wengi wanasema kuwa hawautaki kabisa kabisa, yaani kwa jina maarufu watu hawa huitwa ‘Tuachiwe tupumuwe’.

Mungu ndie kadiri, tujaalie ije iwe hivyo. Yaani wenzetu wa bara waseme ‘haya tunawaachia Mupumuwe’, nyie kwenu, na sie kwetu’. Hali hii bila shaka kwa sasa itaonekana ya faraja sana lakini tukiangalia kwa upana kuna athari kubwa kuliko faida ya kuachwa ‘tukapumuwa’. Nasema kwa kiasi kikubwa, Muungano una faida nyingi kwa Zanzibar. Na kila lenye faida nyingi na hasara haiwi ndogo kimaumbile. Kama hujui waulize wafanya biashara juu ya hili.

Moja ya faida kubwa ya Muungano kwa Zanzibar ni vile kuachiwa tukajenga magorofa kule bara na kuumiliki uchumi wa kule ambao kwa asilimia kubwa umo mikononi mwa Wazanzibari. Hii ni faida kubwa ya Muungano kwani Wazanzibari wamenufaika sana kibiashara kule kuliko hata walivyokuwa kwao visiwani. Sasa kabla ya ‘kupumuwa’ wanapaswa hili walitazame upya kwanza.

Faida nyengine ni ile hali ya kuchanganya damu na wenzetu wa bara na kuunga udugu. Leo hii kwa sababu ya Muungano Mzanzibar kaowa Tabora, Shinyanga na kila pahala. Na kawaida unapofunga ndoa unajenga udugu wa kudumu baina ya kaya hizo. Hii nayo tusiipuuze hata kidogo ni moja kati ya faida kubwa kwa sasa.

Kwa upande mwengine Muungano, umechangia kwa kiasi kikubwa kuiweka salama Zanzibar. Tukumbuke kuwa Mapinduzi ya mwaka 1964, yaliyomuondoa Sultani, ysingeiacha Zanzibar salama. Zanzibar baada ya Mapinduzi ilikuwa na maadui wengi, kiasi kama si Muungano ingepinduliwa mara kwa mara na kukabiliwa na matatizo makubwa ya uvunjifu wa amani. Kwa sasa Zanzibar haiwezi kupinduliwa kwani si nchi yenye mamlaka kamili. Rejea kesi ya 1997 ya viongozi wa juu wa CUF walioshtakiwa kwa uhaini.

Zanzibar ina nafasi kubwa ya ushiriki katika vyombo vya kutunga sheria. Kama utaangalia kwa utulivu zaidi utaona kuwa ni Wazanzibari tu wanaopata kuingia baraza la Wawaikilishi na Bungeni, wakati bara wanapata haki moja tu ya hayo. Muungano umeijengea mazingira mazuri Zanzibar ya kujiamulia mambo yake na kujiletea maendelea kwni wana uwakilishi mkubwa katika vyombo vya sheria kuliko hata bara. Dogo hili?

Tugeukie Michezo na burudani. Ushiriki wa Zanzibar katika michezo kama mpira wa miguu umeipatia faid kubwa Zanzibar kuliko bara. Kwani hakuna mcheazji yoyote duniani anaechezea timu mbili za Taifa ukitoa Mzanzibari. Mfano mzuri ni akina Nadir, Agrrey, Mcha nwachezaji wetu wengi wa Timu ya Taifa, yaani heroes. Wote wanachezea timu mbili za Taifa na kuimba nyimbo mbili tafauti za Taifa. Hii ni historia katika dunia, haijapata kutokea isipokuwa kwetu chini ya Muungano huu.

Isitoshe, kutokana na Muungano Mzanzibari na Mbara kwa pamoja wanauwezo wa kuingia nchi zote mbili bila vikwazo wala pingamizi. Ingekuwa si Muungano suali hili lingehitaji ghrama na vitambulisho kadhaa kwa Raia wa nchi moja kuweza kusafiri kwenda sehemu nyengine ya nchi.

Kwa hivyo pamoja na kuwepo kwa kasoro ndogo ndogo katika Muungano kama vile kuchaguliwa Rais Dodoma (ni kasoro ndogo tu), kutozwa ushuru mara mbili bandarini bara, kupata mgao mdogo wa fedha, kutokuwa na dhamana ya wizara nyeti na Muhimu kwa Zanzibar ni mambo madogo tu hayo. Lakini hasara ya utokuwepo kwa Muungano ni kubwa zaidi.
Zanzibar nje ya Muungano, haiwezi kusimama bila Ubaguzi kama alivyosema Baba wa Taifa, Nyerere. Nje ya Muungano wazanzibari wangebaguana tu, kukawa na huyu ‘Mpemba, na huyu ni Muunguja, kwani dhambi ya Ubaguzi ni sawa na kula nyama ya mtu’. Tungebaguana tu. Pia Sultani angerudi tena visiwani kama si Muungano. Kwa hivyo haya ni mambo ambayo mzanzibari lazima ayafikirie kabla ya kutaka aachwe apumuwe ‘Majuto ni mjukuu’.
Nakunja jamvi, na goya langu!

About the Author

View all posts by

22 Comments on "GOYA LA MZALENDO: ‘MUUNGANO UNA FAIDA ZANZIBAR’"

  1. Abdul 23/12/2012 at 7:40 mu ·

    kwani zanzibar kabla ya mapinduzi kulikuwa hakuna amani wewe wacha pumba fujo na ubaguzi ni sera ya ccm na nyerere wao juzi tu walimtukana mansuri edi riyami na wakairuhu kina borafia hutukanwa na kuregeza sauti hadi wanaume wakasisimkwa wewe kama una sera zako za sulwani khofu kwani eti tumejenga khorofa wao hujenga kanisa kila hatuwa 5 unagema nini

  2. siri 23/12/2012 at 8:53 mu ·

    Mwandishi mimi naona unafanya KEJELI kwa haya unayo yasema. lakini hapa sio mahali paa kejeli, utakuja jibiwa jawabu mbaya. Faida ya MUUNGANO sawa na chowa kwenye mchele kila mtu anajua hili. Taifa haliimariki kwa kujenga majumba ya ugenini… taifa lina imarika kwa kuwajenga watu wake.. leo watoto wetu wanakosa elimu, wanakosa matibabu, wanakosa kazi hakuna wanabaki kula unga !!! maofisi ya serikali yamejaa wenzetu tuu. Kuowa wazanzibari tumeowa dunia nzima lakini hii isiwe sababu ya kupoteaza nchi yetu.
    Tutizame maslahi ya UMMA na sio maslahi ya wachache.. TUACHIWE TUPUMUWEEE.

  3. Awami 23/12/2012 at 10:58 mu ·

    Hivi Muandishi anaishi ulimwengu upi ?sitotaka kueleza mengi kwa machache tu nitaanza kwa kutowa mfano wa hai usio wetu hapa Nyumbani kisha nitaunganisha na mwenendo wa hapa Nyumbani Ukingalia Uchumi wa United Kingdom wahindi wamehodhi sehemu kubwa ya Uchumi huo wahindi wanamduka makubwa majumba mengi Uk hata kuliko hao waengereza wenywe na wao hawa hawakungana na isitoshe mapenzi kati ya watu wa nchi mbili hizi si bora kati yetu na Tanganyika ,ukija kwa wafrika Angalia wa Wagambia wameowa wanawake wa kizungu katika kila nchi wanishi na wamezaa nao hivi wana Mungano baina ya Nchi zao hapa Germany Kuna waGhana wameowa tokea mika ya Ubaguzi wa kweli na hadi leo wapo kuna Mungano gani baina yao sasa Ukija Zanzibar hata Watanganyika nao wanfaidika Makanisa yanatiririka Kila kukicha kama vile Uyoga alhamdulilahi wameletwa wengi na wengi wao wamepata angalau kuelimika na Ustarabu wa kizanzibar lisitoshe hilo angalia wanawake wengi kutoka bara wamefaidika pia na kuja kuuza maungo yao leo hii ukiangalia tu zina kama vile uneteleza ,makanisa mengi mapya yamefunguliwa kwa kufanya kazi ya kusambaza madawa ya kulevya na kuleta vruka njia >waTanganyika wanajivunia Zanzibar .

  4. salali 23/12/2012 at 1:02 um ·

    Hawo wenye kula nyama za binaadam ni watu kutoka bara Tanganyika na Nyerere alikuwa na maana ya hukohuko kwao tuko na usibitisho ya hayo ,yule kijana (Dogo) aliyekutwa muhimbili na kichwa cha mtu anakifonza na wengine wanauwawa kwa imani za kishirikina (Albino),Jee hapo tutasema Tanzania ni nchi ya Amani?..Niaibu kubwa afadhali nchi iwe na vita kuliko kumkata binaadam mwenzako viungo kwa imani ya ushirikina atii watapata utajiri,Niafadhali wa Zanzibari waukatae huu muungano kwani iko siku wanawenza kujifunza kutoka bara hizo imani za kishirikina na kuja kutuuwa sisi ndugizawo huku kwa imani ya kupata Utajiri.

  5. mwanafunzi 23/12/2012 at 1:21 um ·

    Mtoa mada wazanzibari wa leo hatutaki ututajie faida za muungano kuwa ni mbatata, kuoana, kujenga nyumba, kwani hayo yanapatikana popote ilimradi tu unafedha za kutosha. Ikiwa utaangalia jinsi biashara inavyoendeshwa duniani unatakiwa uyaelewe hayo.

    Faida ulizozitaja utawadanganya wanamaskani lakini si wana mzalendo au wazanzibari walio wengi.

    Mzanzibar sio kaachiwa kujenga magorofa bure amewekeza assets ambazo hazihamishiki na biashara inayoendeshwa wanalipa kodi na kuendeleza uchumi wa Tanganyika.

    Uchanganyaji wa damu si faida ya muungano kwani jambo hilo lilikuwapo kabla ya muungano na litaendelea hata kama hakuna muungano cha msingi ni (mapenzi ya wapendanao wawili).

    Kama ni suala la usalama kwa nini tulimuondoa mkoloni na ulinzi ulikuwa wa hali ya juu. Dunia leo imebadilika na kuna nchi zina watu elfu kumi tu duniani, soma historia, ingia kwenye mitandano, soma kwa njia mbali mbali usibakie na kasumba zako hizo ambazo zimepitwa na wakati, hii ni karne ya 21.

    Wazanzibari wengi wanadhulumiwa ndani ya huo muungano unaoutaja, mashekhe wangapi wameuliwa, kuwekwa ndani, au kuihama Zanzibar? Maalim seif na wenzake waliwekwa ndandi kwa miaka ndani ya muungano huu, UAMSHO wako wapi sasa?

    Ni kweli Wazanzibari wengi wanaingia katika vyombo vya kutunga sheria (BLW na Bunge) lakini maamuzi yote yanapitishwa na watanganyika, Wazanzibari walijikomboa ili wawe huru na wajiamulie wenyewe sio wawe wengi katika vyombo hivi.

    Michezo, burudani, uhuru wa kutembea ni utumbo mtupu. Wazanzibari hata bila ya muungano hayo yanapatikana tukiwa na viongozi makini.

    Suala la ubaguzi halijawahi kuondoka katika Zanzibar na Muungano unalipalilia hilo. Huyo baba yako wa taifa ndie aliyelipanda na kulitilia maji na mbolea. Upemba na Uunguja haujawahi kuondoka katika tawala zote (Baba yako wa taifa, Jumbe, Abdulwakili, Komandoo, Karume na hivi sasa Borafya na wenzake, kisonge na kachorora) ushahidi wa haya soma makala na vijarida mbalimbali kama kweli unaijua Zanzibar utayapata tu haya.

    Wazanzibari hatuwezi kumlazimisha mtu kuungana na sisi ilhali tukijua anatudhulumu, kwani Mwenyezi anasema “MSIKUBALI KUDHULUMU WALA KUDHULUMIWA”.

  6. Mrfroasty (Ufundi) 23/12/2012 at 1:53 um ·

    Nilipoona mwandishi amejikita kwa kueleza kwa mapana na marefu faida za muungano, niliona leo nitapata mapya ambayo sijawahi kuyasikia.Ukiwa mtu kama mimi ‘open-minded’ nilijua pengine zipo lakini akili yangu imedumaa nikawa sizioni!

    Nikaendelea kusoma makala hii, nikawa dissappointed baada ya kuona faida zote za wazanzibari wachache kuneemeka na biashara ya soko la bara na kuhamia kule, hili si jipya nimeshalisikia mara kadhaa.Kwa ufupi faida na ziwe nyingi na kuwe hakuna hata kasoro moja, bado hoja itabakia pale pale kama wazanzibari walio wengi hawataki tena muungano…..so be it!so called democracy ?

    Mwisho:
    Mwandishi haonekani kama ni mtu aliefanya utafiti wa kutosha kwa maneno yake ya mwisho kuwa wazanzibari watabaguana baina ya Unguja na Pemba.Niulize swali moja, uliwahi kufanya utafiti jinsi gani Unguja na Pemba zilivyochanganya damu ?

    Kwa muono wangu, watu wa Unguja na Pemba ni wamoja.Kumeletwa hitilafu za hapa na pale na huyo baba ako wa taifa (Allah amlaze mahala anapostahiki – motoni…ameen).Sioni hoja ya kusema faida kubwa ni Taganyika kuchanganya damu na Zanzibar, halafu ukasema Unguja na Pemba zitabaguana.Ushahidi wako ni kuwa Nyerere kasema…you can do better than that!

    Tusichanganyane akili hizo faida zote ulizozitaja ni pumba tupu, hivyo vitunguu na mbatata tunauziwa huku Zanzibar na wala si lazima tununue kutoka Taganyika…..so is the electricity (u forgot to mention it i guess :D )! Labda ingelikuwa Tanganyika pekee duniani ndio inayolima vitunguu na mbatata ndio ungekuja kutueleza hilo.

    Wasalaam,

  7. Ghalib 23/12/2012 at 2:13 um ·

    Duh

    Miaka 48 ya muungano nilizani na mimi nitaletewa paper 100 za faida za muungano, kumbe maneno hayajai hata paper moja.

    Kumbe kunahitajika kongamano au makongamano kuwaelimisha watu kama hawa mwandishi, hapo @Awami akie nitangulia ametoa mifano tosha ya muungano na faida za muugano na kutokuwa na muungano.

    Kwanza ufahamu mwandishi miaka 48 ya muungano sio kidogo , suala la uraia na umiliki mali na uwekezaji, hilo ni suala na uhamiaji, zipo sheria za kimataifa.

    Kwa vile muungano wetu umedumu miaka 48 serikali mbili hizi zitalazimika kutoa fursa kwa wananchi wote wa pande mbili mtu kuwamua wapi anataka kuishi.

    Pili au zinaweza kuamua kuwapa watu ukaazi hasa wale ambao wahamiaji, kwa wale watakuwa na vigezo vya uwekezaji kama walio weza kumiliki ardhi na nyumba watapewa ukaazi au uraia ,kwa wale wasio kuwa na vigezo vya ukaazi basi kutakuwa na taratibu mpya za kuishi katika nchi hizi mbili.

    Kwa wale ambao walio zaa watoto wao pia watakuja kupewa fursa watoto hao hapo baadae wakifika umri wa miaka 18 kuamua wapi anataka kuishi kama kazaliwa bara mama zanzibar yeye ndio mwenyewe maamuzi, au mtoto kupewa uraia alipo zaliwa, huo utakuwa utaratibu wa uhamiaji jinsi ya kuweka vigezo.

    Hasara za muuungano ni kubwa sana zaidi ya ulio andika, kaka tutaziongoea basi tunaweza kupata kurasa zaidi ya hamsini. ukilinganisha na faida zako.

    Kumbuka sis tunada nchi, nchi ina samani kubwa zaidi ya hayo unayoongea, ndani ya nchi ujue kuna viumbe, kuna utamaduni, kuna dini ,rasilimali na mengine neo, huoni ya kwamba ziko zaidi ya hayo unayo ongea /

    Rudi tena katika reseach zako .

  8. SHAMUHUNA 23/12/2012 at 2:53 um ·

    @Pambanua na Mr froasty (Ufundi)

    Nadhani mmesoma mkiwa na majibu yenu tayari!yaani namaanisha kile kilichopo kichwani mwenu ndio hichohicho! hamtaki kusikia kingine.Mwandishi yeye ameyaona hayo na akatolea mifano hai kabisa,nilitaraji na nyinyi mtajibu kwa hoja mjarrabu badala ya kutukana na kubwabwaja.Tatizo lenu ni mawazo mgando mliyonayo,yaani hamtaki kusikia kingine chochote!na hamtaki kufikiri tofauti na mlivyoelekezwa!Kuna watu wanafikiri kwa niaba yenu mnawaamini kuliko chochote,angalieni msiingie kwenye shirki.Matokeo yake hakuna cha maana mlichofanya kwenye maoni ya katiba mpya zaidi ya kung’ang’ania Muungano wa mkataba!Shame on you.Tulitaka watu wadai Znz huru na sio mkataba

    Pili mwandishi amesema ukumbi wake ni endelevu hivyo kama mlikuwa hamna cha kuchangia kwa mada hii,mngesubiri mada zijazo na wahakikishia ataandika yale yatakayowafurahisha!Kwani mimi namfahamu mwandishi na msimamo wake tangu mtandao huu unaanzishwa.Haya maoni alioandika si kwamba yana toka moyoni.Yale ya moyoni mwake yatakuja kwenye makala zake zinazofuata.Mtampenda maana atapita mlemle walimopita CUF,Maalim na UAMSHO!!!!
    @Uongozi
    Naomba maoni yenye matusi na kuudhi na yenye kuvunjia watu heshima yafungiwe!Nilitaraji maoni ya Pambanua yasingetokea au yangefutwa kabisa.kitendo cha kuyaacha ni udhaifu kwa uongozi wa mtandao.Hii ni sehemu ya heshima!

  9. bahussein 23/12/2012 at 2:56 um ·

    Ndugu mwandishi ungelipima kwa kutazama kabla ya muungano Zanzibar
    ilikuwa vipi, na baada ya muungano Zanzibar iko vipi,hapo ndio utajuwa kuwa
    muungano una faida au hasara.

    Huko wafanyabiashara kuhamia bara na kujenga huko ndio unayaona mambo
    makubwa ya mafanikio, kwani kabla ya hapo wafanyabiashara walikuwa hawapo
    Zanzibar au walikuwa wakiendeshwa na nani?.

    Kwa kifupi ndugu ulioileta hiyo mada ujuwe kwamba kama hao ndugu wamekwenda
    kufanya biashara baada ya uchumi wa Zanzibar kubanwa na huo muungano
    wenyewe, na kama hizo biashara zingelifanywa hapa kwetu basi mapato mengi
    yangelipatikana na hayo majumba ya ghorofa usemayo basi yangeliiletea mandhari
    nzuri kisiwa chetu hichi, kwa kifupi hiyo kujenga huko ni hasara ilioje na mapato yote
    ya hao wafanyabiashara hayaingii mikononi mwetu.

    Vilevile mbona hukuongea faida za makanisa na mapub tunayojengewa au hapo
    huyaoni?.

  10. pambanua 23/12/2012 at 3:55 um ·

    @shamuhuna

    wewe na huyo muandishi ni sawasawa hamna lolote, we unafikiri kuna jipya aliloliandika humo? kama hizo ni faida zimeshatajwa zamani kama mngekuwa mna jipya wewe na yeye mungeleta mpya zisizokuwa hizo, sasa kwa kuwa nimeona ni mpuuzi ndio maana nikampa maneno yake asituletee upuuzi humu.

    wewe shamuhuna huniwezi kwa chochote kitaaluma labda ujinga huo utanishinda mimi sio mfuasi wa chama chochote cha siasa kwa taarifa yako na sina kadi yoyote ingawa nawachukia ccm kuliko nimchukiavyo firauni na nina sababu zangu kufanya hivyo.

    sasa yeye akiandika mawazo ya cuf au uamsho mimi hayaniumizi kichwa wala kunifurahisha nasema tena tutakacho sisi ni Zanzibar yenye mamlaka, mimi sasa hivi niko duniani huku nasoma, nimekutana na watu wanaotoka EAST EUROPE nasoma nao, wao walikuwa chini ya USSR kwa muda mrefu tunabadilishana mawazo nawaona jinsi wanavyofaidi uhuru na utaifa sio mbatata na vitunguu. UTAIFA UNA LADHA YA PEKEE DUNIANI NA UKIUKOSA NI SAWA SAWA NA UTUMWA NA NDIO MAANA SISI WAZANZIBARI LEO HATUJIJUI.

    NAAMINI WEWE HUJAWAHI KWENDA HATA KENYA NA NDIO MAANA HUJUI CHOCHOTE KUHUSU FAIDA YA KUWA DOLA HURU WAULIZENI WALIOSAFIRI KWA WATU WATAKUWAMBIENI.

    ETI MNASEMA FAIDA YA BIASHARA, KUTEMBEA BARA, KUJENGA MAJUMBA,, HIZO NI AKILI PUMBA. MWAKA JANA NILIFANYA EXCHANGE STUDY NIKAENDA JAMUHURI YA CHINA, CHINA PAMOJA NA UKUBWA WA NCHI, RAIA WENGI, KUZALISHA MALI KWA WINGI,,LAKINI BADO WANATEGEMEA BRAZIL. THAILAND NA VIETNAM KWA BIDHAA NYINGI HASA ZA CHAKULA,, LAKINI PIA CHINA KUNA WATU WA MATAIFA YOTE WAMEWEKEZA NA WANAFANYA BIASHARA TENA KUBWA KUMZIDI BAKHRESA TANGANYIKA NA HAWANA MUUNGANO WOWOTE.

    FUMBUENI MACHO WAJINGA NYIE, TEMBEENI MUONE MJIFUNZE DUNIA YA LEO HAIHITAKI MUUNGANO KUISHI SEHEMU AU KUFANYA BIASHARA. GLOBALIZATION IMEMALIZA KILA KITU ,,KINACHOFANYA KAZI NI CAPITAL, KNOWLEDGE, TACHNOLOGY, COMMUNICATION SKILLS AND SERVICES UKIWA NA VITU HIVI UNAISHI POPOTE, UNAFANYA KAZI POPOTE, UNAFANYA BIASHARA POPOTE DUNIANI.

    HAKUHITAJI MUUNGANO

  11. brenda 23/12/2012 at 5:30 um ·

    Nyooote maneno yenu ni mazuri

  12. brenda 23/12/2012 at 5:35 um ·

    Nyooote maneno yenu ni mazuri lakini waulizeni na wabara, wao wamepata maendeleo gani tokea kuungana na zanzibar? yaoneni sasa maendeleo yote ni kwao na sisi labda mapembe , nakuombeni tena.. tembeleeni gazeti la Fullshangweblog.com la Tanganyika muone wenzetu wanavyozitafuna pesa za Muungano, nyie eti mmeoa, mbona hampewi posho kidogo mkadumisha udugu na urafiki wenu?, na hayo majumba yenu mliojenga na kulipia kodi mbona hata walinzi hampewi ?kila siku risasi,…….muandishi na wachangiaji tusipasuaneni kifua,

  13. Kishanshudas 23/12/2012 at 9:54 um ·

    @Wachangiaji wote ukitoa Shamuhuna

    Ingekuwa makala ya mwandishi huyu munaemwita @stonetown, ingekuwa ni nyavu au kimia nyote mpaka Froasty angenasa ndani ya nyavu hiyo akawa wa bure kuuzwa mnadani. Nyote mmekuwa kama masamaki tu, mmewekewa chambo kidduuchu mkameza. Tumieni akili ndugu zangu nyie mmechoka kimawazo. Mwandishi kama mmesoma makala yake ameeiita ‘GOYA’ maana ya goya mnalijua nyie? Yaani ni kama porojo baada ya shibe tu na mara nyingi ni maneno yenye kukejeli linalosemwa au kukebehi kitu.Hilo ndio GOYA. Hilo moja

    La pili, hio heading mwandihi ameweka inverted commas’ kwamba si maneno yake. Hapo ameonesha kukejeli hizo harakati ziitwazo ni faida. Hilo hamkuliona, bila shaka bibi zenu walikuwa hawawasimulii VITENDAWILI.Pole zenu.

    La tatu, Hamkuweza kuisoma ‘tone’ ya maandishi kwa upungufu wenu wa maarifa ya kihakiki. Sauti ya maandishi hi inaonesha kila dalili kukejeli yote hayo yanayoitwa ‘Mafaida ya Muungano’. Na hili hamkuliona, hakucheza hata KOBOLE utotoni kwenu basi hata KIFICHO FICHO na FOLITI?

    Pole zenu na jazba zenu

    • Mrfroasty (Ufundi) 25/12/2012 at 3:12 um ·

      Nikubali neno goya ndio kwa mara ya kwanza nalisikia kwenye makala hii, nina khofu kuwa sukutaka kufuatilia maana yake nikiogopa kuwa ni kati ya yale maneno ya kutungwa kutoka upande wa pili kama vile tovuti!

  14. nuramo 23/12/2012 at 10:03 um ·

    Pambanua Well spoken,mi sina la kusema ila Najua Mwandishi wa hii mada anajua kila kitu na nia yake si kusema Faida kama faida bali Faida kwa Kukejeli ili apate watu kuanzisha Ligi.Kwa mfano Hasara za kulipa Ushuru mara mbili ni ndogo kuliko alizozitaja Naelewa Fika kuwa anaongea kwa kutania Ila
    Huu si wakati wa kufanya Mzaha nami niongeze yangu kidogo:
    Seychelles ni 150 tiny islands vilivyopo kama 1500 Km na Bara la Africa,cha kushangaza visiwa hivi ni Second richest country in Africa after Equatorial Guinea ,lakini kwa muda mrefu vilikuwa ni vya mwanzo Hakuna South-Africa wala Nigeria wala Egypt,Watu wengi watashangaa lakini kwa ufupi Seychelles remains the richest territory in Africa in terms of GDP per capita (US$9,440.095 at real exchange rates and US$17,560.062 at PPP 2008 estimate) http://siteresources.worldbank.org/ICPINT/Resources/ICPreportprelim.pdf

  15. Msemaji mkuu 23/12/2012 at 10:23 um ·

    Mimi sioni kitu cha watu kulumbana kwa matusi na jazba hapa. Muandishi kaanza kwa kujieleza wazi kwamba hili ni GOYA. Maana ya goya ninavyoelewa mimi ni masikhara au utani. Sasa kila hoja aliyotoa muandishi katika mada yake ni maskhara na utani tu wa kutaka kuwachemsha watu.

    Nina uhakika muandishi mwenyewe hakubaliani na 80% ya hoja zake mwenyewe alizozitoa na kuzieleza ila kafanya hivyo ili kuona je watu watasema nini juu ya agenda hizi?

    Mimi sitaki kujihusisha na mjadala huu kwa sababu kila mtu anaelewa ukweli wa mambo ulivyo. Na aliekuwa bado hajaelewa ni kwamba hataki kuelewa, na kujaribu tena kumuelewesha ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa.

  16. Al khanjary 24/12/2012 at 4:01 mu ·

    Salam Alaykum Wanaukumbiiiii.

    Kwanza ningependa kumshukuru Allah Subhanahuu wa Taala kwa kutupa nafasi ya kuchangiya hili ‘GOYA’ la Ndugu Stonetown(Kiongozi).

    Jengine ni jambo ambalo lililonitia huzuni kuona uwezo wa Wazanzibari wenzangu kuwa wafinyu wa kufahamu lugha yao ambayo ni moja ya jambo la kujivunia.Mwandishi amesakamwa kwa jazba na matusi kutokana na ufinyi wa ufahamu wa wachangiaji wengi ila ni wachache tu ndio waliyoifahamu mada na mantiki ya uandishi wa mada yenyewe.

    Iweje leo Waswahili wenye kuzungumza lugha moja na ndio lugha yao asilia nayo ni kiswahili wanafasihiwa lugha yao na kuongezewa maneno yasiyo na mtiririko wa kiswahili na kuhakikiwa lugha yao kutoka kwa watu wenye asili ya lugha za kikabila zilizokithiri ya khamsini khalafu wakaiita lugha hiyo eti”Kiswahili fasaha”………Haya Muungano huo!

    Ewe Mola wetu tupia jicho lako kwa Taifa letu la Zanzibar na asili yetu inayopotea na vizazi vyetu pia.
    Amiin.

  17. pambanua 24/12/2012 at 10:40 mu ·

    wewe lete goya siku 260 lema atapewa millioni 85 za mshahara ma marupurupu mengine sasa wewe lete goya za kijinga,,watu wanatafuna nchi kwa kwenda mbele.

  18. dk.m 24/12/2012 at 11:57 mu ·

    Usipokua mstahamilivu hapa, utajutia ulichokiandika…. Niliwahi kuisoma makala hii kabla ya comment hata moja ila sikutarajia kama mwandishi anaweza kueleweka vibaya na kupata maneno makali kiasi hiki. By the way, nampa pole sana. Na kilichopelekea yote hayo, ni baadhi ya wachangiaji kutojua ni nini Goya.

  19. Mzambarauni Takao 24/12/2012 at 8:21 um ·

    Pole Ndugu Stonetown .Na khasa kwa kuujuwa msimamo na uzalendo wako. Nilipomaliza kuisoma tu makala yako nikatanabahi ya kuwa unatumia kinachoitwa kwa lugha ya Kiingereza ”satire”. Maana yake kukemea, kukebehi maovu kwa njia za kejeli za kimafumbo-mafumbo ya kinyumenyume.

    Satire hutumika unapotaka kukosowa kwa mlango wa nyuma. Maa shadidi l’asaf wengi walimuelewa vibaya ndugu yetu Stonetown.
    Ndugu Stonetown usivunjike moyo endelea kuchangia katika mkondo wa kuikomboa Zanzibar. Inshaa’Allah tutafika na tutapumua.

  20. Mrfroasty (Ufundi) 25/12/2012 at 3:08 um ·

    @Pambanua,

    Tafadhali tupunguzie matusi, shukurani kwa ushirikiano.

    Kwa niaba ya uongozi

  21. aslam 27/12/2012 at 4:55 mu ·

    Salamu wazanzibar, kwa kweli mtoa mada hakuelezea hasa faida. zaidi ya hasara kujenga bara ni faida nani kukwambia Mtu awache kujenga kwao ajenge bara ni faida wataalamu wa uchumi duniani kote wanakipinga kitu hiki , juzi tu kuna kampuni ya kichina imenunua kampuni ya mafuta Canada mbona umedhuka mzozo mkubwa hata wakuu wa majeshi marekani wakailani Canada kwa kuwaruhusu wachina ; kwani Kabla ya muungano watu hatuoani na wa bara fanya uchunguzi utajuwa na kwa kumalizia nakuuliza hiyo dar es salam imejengwa na nani je wakati huo muungano je ulikuwapo utapata jibu, Mie nahisi ijuwe historia ya yanganyika na zanzibar Kabla ya uhuru , ikesha ulete faida ya muungano , Mimi siuiti muungano Bali ni mavamizi , ukisema faida za mavamizi hapo nitakuelewa lakini kwa muungano hakuna kwanza kitu muungano hakuna kisheria , kama utataka niingie kisheria muungano haramu haujafikiwa na wananchi kwa hiyo it’s faida za mavamizi sio muungano , kwa hivyo ita faida za mavamizi ,

Comments are now closed for this article.