ZEC mpya ijiamini
Written by Ashakh (Kiongozi) // 31/12/2012 // Habari // 3 Comments

Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar wakiwa kwenye picha ya pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Sharif ameelezea matarajio yake kuwa tume mpya ya uchaguzi itakayoundwa Zanzibar itafanya kazi kwa kujiamini zaidi ili kukidhi matakwa ya wananchi.
Amesema iwapo Tume ya uchaguzi itafanya kazi kwa kujiamini na kuacha kufuata matakwa ya wanasiasa, itajenga imani kwa wananchi juu ya uwezekano wa kuwepo kwa chaguzi huru na za haki.
Maalim Seif ameeleza hayo leo nyumbani kwake Mbweni Zanzibar, wakati akizungumza na wajumbe wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC waliofika kwa ajili ya kumkabidhi ripoti ya utendaji wa tume hiyo kwa kipindi cha miaka mitano, pamoja na kumuaga baada ya kumaliza muda wao wa utumishi ndani ya tume hiyo.
Amesema kazi iliyofanywa na tume hiyo ni nzuri, lakini tume inayokuja inapaswa kujifunza kutokana na tume hiyo ili kufanya kazi zake kwa kufuata misingi ya sheria na kuongeza ufanisi wa Tume.
Ameelezea haja kwa tume hiyo kuanzisha mfuko wake, ili mapato ya tume yaingie moja kwa moja katika mfuko huo na kupunguza usumbufu wakati tume inapohitaji fedha kwa ajili ya matumizi yake ya kawaida.
Hata hivyo Maalim Seif amesema tume hiyo inayomaliza muda wake mwishoni mwa mwezi huu, inaondoka huku ikiwacha viporo ambavyo tume inayokuja inapaswa kuvipa umuhimu wa kipekee.
Miongoni mwa mambo ambayo hayakuweza kutekelezwa na tume hiyo ni pamoja na kushindwa kulifanyia uhakiki daftari la kudumu la wapiga kura kwa vipindi viwili tofauti, jambo ambalo liliahidiwa na tume hiyo kufanyika kila ifikapo mwezi wa Oktoba.
Kamishna wa Tume hiyo bw. Ayoub Bakar Hamad amesema tatizo hilo lilitokana na ukosefu wa fedha za kuendeshea kazi hiyo, na kwamba kwa sasa Shirika la Umoja wa Mataifa la UNDP tayari limekubali kutoa fedha kwa ajili ya kuendeleza kazi hiyo.
Amesema iwapo fedha hizo zitapatikana kwa wakati mapema mwezi ujao, tume ijayo itakuwa na uwezo wa kufanya uhakiki mara mbili kwa mwaka, ili kufidia muda uliopita.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume hiyo Bw. Khatib Mwinyichande amesema jihihada za makusudi zinapaswa kuchukuliwa katika kuimarisha demokrasia ya uchaguzi Zanzibar.
Amesema Tume inayokuja inaweza kufanya kazi zake vizuri zaidi iwapo wanasiasa watatoa ushirikiano wa kutosha kwa tume hiyo sambamba na kukubali kufuata sheria zilizowekwa.
“Naomba wanasiasa musioneane haya, shaurianeni na kubalini kukosoana, na kubwa zaidi ni kukubali kufuata sheria”, alishauri Mwinyichande na kuongeza,
“Wanasiasa pia munayo nafasi kubwa ya kuisaidia tume kwa kuipa maelekezo yanayostahiki, na kufanya hivyo kunaweza kuipa nyenzo bora za kufanyika kazi”, aliongeza.
Nae mkurugenzi wa Tume hiyo Bw. Salum Kassim Ali, ameahidi kuzifanyia kazi changamoto zilizojitokeza katika chaguzi zilizopita, ili kuweka mazingira bora zaidi katika chaguzi zijazo.
Habari na Hassan Hamad. Picha na Salmin Said, OMKR Zanzibar



3 Comments on "ZEC mpya ijiamini"
Mwinchande maneno hayo ilikuwa uwambie viongozi wa ccm maana ndio wanaowaburuzeni, wazanzibar wanajua kwamba changuzi zote mmekuwa mukichakachua na kutoa ushindi wa 51% kwa ccm muda wote huo kitu ambacho hata watoto wadogo wanajua ni uongo.
1. ZEC imefanya kazi nzuri?!!!, Ikiwa wapo wameshawekwa vizuka, mayatima na walemavu kwa kupinga unyang’anyi, na bado wakafanyiwa ujambazi mbele ya tume.
2. WABEPARI wanaogopa msijeshika UISLAMU wenu na ndio kila mkipoteza imani nao hujaribu kuja na style ya kukudanganyeni kama hiyo ya kumaliza muda na kuletwa wababaishaji wengine.
3. Wabepari ndio huweka Raisi/KIBARAKA wamtakae (ikiwa raia wanamtaka au la) na hizo chaguzi ni geresha wasiojua tu.
Kama una comment zozote za kutaka zimfike Maalim, basi wasilisha moja kwa moja kwenye Blog yake:
www.http://mkr1znz.wordpress.com/