WITO WANGU KWA MASHEIKH WA ZANZIBAR!!

Written by  //  27/12/2016  //  Habari  //  Maoni 13

Mr Wisdom

WITO WANGU KWA MASHEIKH WA ZANZIBAR!!

Assalam alaikum,
Nachukuwa nafasi hii kumshukuru Allah kwa kutuwezesha Kuwa waumini na kutupa tawfiiq ya Kuwa vipenzi wa dhati wa Mtume Muhammad (s).

Pia nachukuwa fursa hii kumpongeza rasmi Mufti wa Zanzibar sheikh Swaleh Kaabi na uongozi wake katika kushughulikia suala la Kijana aliyemtusi Kipenzi cha Dunia hii Mtume Muhammad (s).

Lakini naona nitowe WITO muhimu kwa masheikh wote wa Zanzibar na wa Afrika ya Mashariki kuujuwa wakati na matatizo ya jamii tunayoishi karne hizi na hasa katika suala la kuukashifu Uislamu, Mtume na vitu vitukufu vya Uislamu!

Vijana wengi zaidi Leo kinyume na karne zilizopita wameweza kusafiri kwenda kwenye nchi za Kiarabu na nchi za Ulaya na wameona mengi yanayojiri kwenye nchi hizo na kukumbana na mitihani au shida na raha kama ilivyo katika maisha.

Vijana wengi wanaokwenda Uarabuni wanasikitishwa na namna wanavyo tendewa na waisilamu wenzao na wanapokuja huku Ulaya huyasema hayo wanayotendewa kinyume na matakwa yao hadharani au kwenye mitandao ya kijamii, jambo ambalo watu wengi linawapa wasi wasi juu ya uwezekano wa Uislamu Kuwa ni Dini sahihi (ewe Allah tuthibitishe katika Dini yako) Amin!!

Huku Ulaya Vijana wengi hukirimiwa Chini ya mwanvuli wa haki za kibinaadamu na kanuni zisizobaguwa watu kwa kabila, rangi au dini kwa kiasi kikubwa ingawa udhaifu huonekana hapa na kule hata hapa Ulaya Lakini kwa sura iliyo rasmi Ubaguzi au chuki za kisiasa na kikabila kama zinavyojitokeza kwenye mataifa ya Kiislamu Ulaya hakuna sana, kwa mtazamo wa akili changa na ya ujana Vijana wengi wanaweza kughilibika kuukosowa Uislamu na hasa pale wanapo watazama watu wanavyowatendea hapo Mashariki ya kati na wanapoona picha sahihi ya kuuwana kwa miaka mingi kati ya waisilamu!!!

Majuzi hivi alionyeshwa kwenye TV ya Kimarekani Kijana Hussain ambaye ni kutoka Afghanistan, alipoulizwa kwa nini katoka kwenye Uislamu kajibu Kuwa tangu alipozaliwa mpaka Leo hajashuhudia amani wala upendo katika nchi yake kati ya hata watu wanaosali msikiti mmoja!! Anasema baba yake aliuliwa na waisilamu na sio makafiri kwa hiyo kuna haja gani yeye kujinasibisha na Dini yenye kuuwa wafuasi wake???

Pia huko Sweeden kuna msichana wa Kisomali ambaye amertadi sababu zake ni Kuwa Uislamu hauna Upendo na watu wake Huko Somalia wanauwana tangu alipozaliwa hadi Leo hii na anasema anamshukuru Yesu kwa kumkombowa na Dini yenye kuwafanya wafuasi wake wawe maaduwi wao kwa wao na wenye kuuwana wao kwa wao!!!

Hii ndio hali ya karne tunayoishi enyi Masheikh mnaokuwa tayari kumhukumu mtu anayedaiwa kurtadi kwa kumkata kichwa bila ya kuyatafiti matatizo yake na mazingira yake, ipo haja ya kuundwa kwa Jopo la Masheikh kushughulikia suala hili haraka iwezekanavyo!!

Hii ni hatari kubwa Masheikh kama hatukufanya wajibu wetu kuna uwezekano wa Kuwa na watu wengi kama Abdullah wengine ambao wako Chini kwa Chini wakiogopa kujitokeza.

Maombi yangu kwenu ni kutayarisha Jopo maalum la wataalamu watakaokuwa na dhamana ya kuwaita watu kama Dr Abdullah na naomba kwa baruwa hii tuanze na huyu huyu Dr. Abdullah aitwe mbele ya Maulamaa na Wataalamu aulizwe live nini hasa matatizo yake katika Uislamu au ni kitu gani hasa kinachomfanya awe na shaka na Uislamu?

Naomba Dr. Abdullah aulizwe hayo mbele za masheikh bila ya vitisho na kwa hekima kubwa kwa sababu Uislamu haujapatapo kuogopa kujibu hoja za makafiri wala wapinzani wake.

Basi ni wajibu sisi kutambuwa nini hasa kimewasibu Vijana wetu na kujaribu kujibu matatizo yao au masuala yao si hivyo huenda tukawakosa Vijana wengi na hasa kutokana na Dunia Kuwa ndogo na kuweza kupata habari za kila pembe za Dunia kwa urahisi!

Leo hii na katika Karne hii kuna watumwa wanauzwa na kufugwa huko Yemen, Mauritania, Mali na Sudan na hii sio siri tena kwa sasa Ulimwenguni, Vijana wanauliza kama huu ni Uislamu (nina hakika si Uislamu wa Mtume Muhammad huo) jee Allah kweli ataruhusu watu kuuzwa na kununuliwa kama Badia au kachori??

Lakini masheikh tumeinyamazia batil kwa muda mrefu mpaka Vijana wameelewa Kuwa haya ni batil baada ya kuambiwa hayo na maaduwi wa Uislamu, sasa kwa Kuwa tumeinyamazia haki na tukakaa kimya kwa sababu mambo hayo yanatendwa na Iran, au Saudia, au Yemen au Oman au Misri, kwa kuogopa Masheikh wa nchi hizo ambao nao wamekaa kimya au kuogopa kutopewa misaada na nchi hizo, naamini tutaendelea kulipa gharama kubwa kwa kutokea watu kama hawa Watakao mtukana Kipenzi chetu hadharani au kwa kufanya kampeni za siri za kuwatowa watu kwenye Uislamu na haki.

Naomba tuachie sharia ichukuwe mkondo wake kama TAARIFA YA MUFTI WA Zanzibar ilivyosema, Lakini masheikh tujitayarishe na kujibu hoja za Vijana ambazo huzipata amma kutoka kwenye mitandao, au kwa kukatana na mitihani ya nchi za Kiarabu na za Ulaya au kutokana na wasi wasi wa shetani.

Tunamuomba Allah ainusuru Zanzibar na watu wake na azilinde nchi zote za Kiislamu na mitihani ya vijana wake, Amin!!!

Kuhusu Mtunzi

View all posts by

Maoni 13 katika "WITO WANGU KWA MASHEIKH WA ZANZIBAR!!"

 1. Abdul Zakinthos 27/12/2016 kwa 6:49 um ·

  @Kiongozi Nashkuru kulikumbushia hili ila nitaongeza kitu,

  Huyu Abdalla alikuwa UK zamani tu , kwa bahati mi sijapata kukutana nae ila nilisikia story zake miaka 3 iliyopita akiutokana uislam, wakati akiwa Zanzibar, pale Block no 6 Michenzani, watu wakishindana nae kwa hasira kila usiku lakini hakuna aliemshinda kwa hoja maana hutumia matusi makubwa makubwa watu hukasirika.

  Pia watu walimuona msomi katoka UK kaletwa na Dr.,Sheni awe daktari pale mnazimmoja, sas akawa anatumia kigezo hicho eti yeye ni mtaalam hata Huko UK hataki kufanya kazi ni mtaalam na anajua maradhi na pia binaadamu hatokani na MUNGU na akiwafahamisha watu kwa njia ya kitaalamu ku prove his points.

  Huyu jamaa haamini dini wala Mungu si ya kiislam wala ya kikristo ni ATHEIST kwa mujibu wa mwenyewe.

  So hata asemeshwe na nani haamini huyu ila nasi tunaamini kuwa UK AU ULAYA ndio kwenye elimu kwa hiyo ukitoka ulaya unaonekana msomi wa Zanzibar nzima kumbe uongo mtupu

  Elimu ya UK ni biashara tu na hili wengi wataliunga mkono waliosoma UK au Ulaya nyengine.

 2. Abdul Zakinthos 27/12/2016 kwa 6:57 um ·

  Kuhusu vijana wanaokwenda Ulaya niongezee:

  Zamani Ugiriki alikuwapo kijana mmoja akiitwa Sheria,huyu jamaa si mlevi na ni muislam wa kuzaliwa na pia amekwenda chuoni kujua japo Kul huwallah..

  Kwa bahati mbaya alipotoka Africa alipitia njia zetu hizi za miguu Lebanon-Turkey – Greece.
  Akapata mtihani pale na wenzake kama 2, wakawa hawana pa kukaa wakaangukia kukaa kanisani chini ya Priest akiwapa kula,pesa na malazi.

  Alipopata kuingia Greece, alianza kuutokana uislam, ila pia alikwenda mbali zaidi, hata kuwatokana wazee wake kwa nini walimzaa Muislam, akisema kuwa eti waislam alipopata shida hawakumsaidia na alikuwa nchi ya kiislam.

  sasa watu hawa waogopeni maana hawafahamishiki,Allah ashapiga mihuri kwenye nyoyo zao.

  Kuna mmoja nae namhifadhi jina tulikuwa nae Greece nae kijana wa Kizanzibari, alikuwa akitokana vile vile, alipopata mtihani wa kukaa ndani alipotoka, sijaweza kuamini alibadilika akawa mtu mwema mwenye kuufuata uislam..

  Najua Abdula atarudi zake UK kwa kuwa nadhani ana uraia wa UK

 3. kwaomtu 27/12/2016 kwa 8:20 um ·

  Mimi nafikiri nyote mnakosea, kuishi ulaya, Somalia na kwengineko, ni sehemu tu Allah amejaalia tuweko. Kuna watu huishi ulaya na raha zote hizo hurudi Somalia kufuatia jihadi. Kila mtu na mtihani aliojaaliwa nao.

  Nafikiri Asha na wengine hoja ulioileta si mbaya ila tusiwatizame wenye majina ya kiislamu tukasema wanayoyafanya wao ndio uislamu. Nakumbuka wakati mmoja nipo New zealand kuna rafiki yangu kutoka Norway alinifuata akaniambia amependezewa na tabia zetu sisi Waislam na akataka kusilimu. Nikamwambia sawa umependezewa na tabia zetu ila je Uislamu umeshausoma? Akanijibu atausoma, nikamwambia usiingie hadi usome taratibu zake ujue nini unatakiwa kufanya na nini unatakiwa kuacha.

  Akaniomba nimsomeshe nikamkatalia nikamwambia mimi nikikusomesha utaniona nakushajihisha uingie, kwa vile unaakili zako soma mwenyewe na nilimkatalia hadi nilipoona ananikera sana nikamjibu sasa nakupa mtihani ukiuweza basi na Uislamu ushauweza. Alipokubali hayo moja nilimwambia ukubali tukienda kusali Alfajiri na wewe njoo utizame tu, nikamuuliza kuhusu girl friend akaniambia hana hadi nilipomuhisi kweli kashausoma na ameshaukubali ndipo nikamtamkisha shahada. Alistaajabu alifikiri kunahitajika registration itakayochukua mda kidogo.

  Hivi ameoa Muislam Mnorway mwenzake na tunawasiliana mara kwa mara na ananishangaa kwa nini nilikua nampiga chenga, nikwambia hii dini ni voluntary hulazimishwi ila ukiingia basi uingie wote.

  Ashak hata Mtume Muhammad S.A.W aliambiwa awaambie Mabedui kua Hawakuamini bali walisilimu tu, Kua Muislam na Muumin ni vitu tofauti. Tusome dini tuijue tusivunjwe moyo na matendo ya watu wengine.

  • Abdul Zakinthos 27/12/2016 kwa 9:03 um ·

   Nadhani hujafahamu hiyo mada, Mi nimefahamu uzuri ila labda hujabahatika kukutana na watu wa aina hii au hujakutwa na matatizo yaliyowakuta watu wengine katika pirika za maisha nikukumbushe tu Hadithi moja ya Mtume S.A.W alisema

   ” Ogopeni vitu viwili (2) Umasikini na maradhi,kwani vitu viwili hivi,humpelekea mtu kukufuru”

   Sasa ndugu zetu wengine wakipata tu misuko suko basi hupelekea kukufuru, na wengine wanaponeemeshwa zaidi pia hupelekea kukufuru..

   Hivi vijana wangapi wanaondoka nyumbani wakiwa na tabia nzuri lakini wakifika Ulaya kwa kuwa kuna uhuru wakufanya watakavyo wanaharibika? Ni kweli Tabia inachangia lakini pia na mazingira kwa mfano:

   Unapoanza kazi ukakuta bosi wako na wafanyakazi wengine wakati wa break wote hupitiliza muda wa break zao, si dhani wewe siku zote utakua unachukua break muda ule ule nawewe utafuata Culture ile ile.

   Ndio maana tukasema inachangia hii ulaya kwani watu wanajisikia wapo huru na wapo mbali k umbe Allah anawaona.

 4. Mrfroasty (Ufundi) 27/12/2016 kwa 8:21 um ·

  Asalaamaleykum,

  Mie nichangie kwenye suala zima la vijana waliohajir nchi za ulaya, niseme kimoja tuu hii haina uhusiano na nchi au mahali mtu anapoishi iwe ulaya, afrika au arabuni.Hii inaambatana zaidi na tabia na hulka ya mtu husika kufurutu ada.

  Binafsi husikia watu wakijifanya acting nyingi, wengine kujifanya wanachanganya kiswahili, mara vijineno vya kiengereza vinavurumishiwa ndani ya kiswahili basi ilimradi ulimbukeni umewazonga.Hizi zote zinafanana kwa namna moja au nyengine na hio ya kukashifu dini , zote hizi ni hizo hizo furutu-ada zinazofanywa na vijana.

  Kwangu binafsi huko kwenda nje maulaya, ni sawa na kutafuta vijisababu vya kuficha uchafu……haina uhusiano kabisa na kwenda ulaya.Wengi wanaishi ulaya tokea dahali na ukikutana nao hamna aliesahau kiswahili wala kukashifu uislamu…..tumsalie mtu jamaa! Hapa naona kama mstari umevukwa!

  • Abdul Zakinthos 27/12/2016 kwa 9:08 um ·

   Naona hapa umenifanya ni cheke, sasa mbona wewe umechanganya hicho kiswahili na kizungu? kumbe na wewe umo?

   Basi mi nadhani kuchanganya lugha nii kujifanya bali ni mazingira yanachangia ,wa mfano unapoishi nchi za ulaya unapokutana na mswahili mwenzako akikuuliza saa tu basi unachanganya saa nne utasema sa kumi au haikutokezei hii? kwa maana ule ubongo wako unakua hauja fanya kazi ya haraka kujibu kama tunavojibu kiswahili.

   mi nadhani ni mazingira unayokaa hasa ukiwa labda umeoa mke anaongea lugha nyengine au sehemu unapokaa labda hamna mkusanyiko wa watu wa jamii yako pia yanachangia plus na tabia.

   Tusilaumu kuhusu Lugha ,hata tunajadili maadili nadhani …

 5. Ghalib 27/12/2016 kwa 8:59 um ·

  Mimi sikubaliani kwamba kusoma sana kunaweza kumfanya mtu asiamini Mungu, hasa kwa ma doctor, kwa sababu wanacho amini ni nature ya mwanadamu, wakati ni nguvu za Muumba mwenyewe, katika Qur-an imeelezea history nzima ya mwanadamu alivyo ubwa na anavyo umbwa hivi sasa, kwa maana hii elimu imetoka katika Qur an , wana science walicho fanya ni kuchunguza hii miujiza ya Allah ,ni siri yake Allah.

  Kama mutafuatilia wale ambao wajiitao wana science, wavumbuzi wa mambo huko magharib, wanaposoma Qur an hujikuta kuwa kila walicho fanya tayari Allah amesha kieleza, yeye ni m juzi zaidi, na hapo huishia katika uislamu.

  Mtu kama Abdallah sidhani kama anaujua uislamu, ni kweli amezaliwa katika uislamu, na a najua sura moja mbili tatu, laiti kama angeujua asingelithubutu kusema hayo.

  Jengine huyu amekosa heshima, heshima ambayo asie heshimu mkubwa wala mdogo, ndio maana amefika hapa alipo fika, hata hao makafiri, hawathubutu kumkufuru alie tuumba, kikubwa wataukataa uislamu na mtume wetu muhammad s.a.w) hii yote ni kutokujua na kupuuza na kukumbatia dunia.

  • Abdul Zakinthos 27/12/2016 kwa 9:15 um ·

   Abedi sisimizi anatoka kwenye chuo hasa ,sasa hivi yupo wapi? Watu wa aina hii tushakutana nao sehemu nyingi za ulaya.

   Nilikutana na Mnigeria mmoja ambae alikuwa muislam na sasa ameritadi na yeye ana sababu zake,lakini zaidi nadhani ni kufuata mwanamke Lakini sijamsikia kutokana.

   Bali nilikutana na Muigypt mmoja ambae anaishi USA sasa hivi, huyu huwezi kukaa nae hata dakika moja, maana huanza kutokana dini hadi mtume S.A.W humtokana na kumuita pedhophile kwa nin kamuoa Aisha RA umri mdogo na mambo kadhaa ,na akitoa ushahidi kuwa mtoto wa kike umri wake wa kuchipukia ni umri kadhaa..(licha ya kuwa mazingira ya wakati yanachania) huyu si muislam alikuwa ni Coptic Christian

   Pia nilikutana na Muiran nae alikuwa ni daktari na alikuwa muislam kwa mujibu anavosema maana tulishindana kwenye dini ,nae pia huwezi kukaa nae dakika moja.

   mi wala siwashangai watu wa aina hii kwa kuwa unapotaka kuwaelimisha basi hutokana wakakutoa kwenye mada kama hupo makini.

 6. MAWENI 27/12/2016 kwa 9:12 um ·

  Pengine huwo uraiya wake wa Uk. Ndio ulompa ujeuri , ushindani na ujuwaji.
  Hapo Unguja naamini makachero wanazo khabari zake zote.Hamuoni alivyo jisogeza kwa Mchimbi.
  Nchi ya Zanzibar na watu wake inapita kwenye mtihani mgumu sana ; kijamii, utamaduni, sisa , na kubwa zaidi kidini. Hayo hayakuanza leo. Lakini sasa yako wazi zaidi. Kwa kuwa wanaofanya hivyo ni kama vile mfumo wa ulimwengu hivi sasa unawalinda.
  Kwa kuazima maneno Chinu Achabe : THEY HAVE PUT A KNIFE ON THINGS THAT HOLD US TOGETHER AND NOW WE HAVE FALLEN APART.
  Matatizo ya ulimwengu wakiisalamu takriban yana lingana.Ukichunguza historiya ya Zanzibar kwa makini utaona tumeanzwa sisi ; tokeya alipo ingiya mkoloni Mrenu Afrika Mashariki . Kwa lengo la kueneza dini yao. Kama tunavyo hadharishwa kwenye Qura’an takatifu kuwa hawato rdhika na sisi waislamu mpaka tufuate mila zao. Hawo walo jiripuwa kama wasomali huko ugenini ;msifikiri kabisa wenye nchi yao hawawajui asili yao hasha!
  Kwa upande wetu ni juu yetu kuwailimisha chipukizi msingi ya dini ya ki islamu iliyo sahihi. Na wazee wawe mfano bora kwa watoto. Kuwaeleza historiya ya kiislamu sera ya Mtume (s.a.w) maswahaba zake . Kufundishwa quraan pamoja na tafsiri na hadith za mtume (s.a.w)
  Dini ya kiislamu ni ya Allah . Sisi waumini tufanye wajib wetu.
  Hiyo kuunda jopo la mulamaa kmuilisha huyo kijana na kumulekeza kwenye njia sahihi ni fkra nzuri. Na sikuzote watu kama hao ni kuwakabili sio kuwaogopa au kuwakimbiya. Wengine wamepata mitihani ya maisha wana changanyikiwa.

 7. Abdul Zakinthos 27/12/2016 kwa 9:22 um ·

  Mi nakwambieni huyu jamaa hafahamishiki hata kama akitoa video milioni kujidai kuomba radhi, taarifa zake nimezipata miaka mitatu nyuma ,hii video ya juzi imetokea kibahati mbaya tu lakini ukiwa nae karibu hutamka maneno machafu machafu zaidi kwa muda mrefu sasa nawatu washashindana nae sana.

  Kibaya zaidi ninavojua mimi huyu jamaa ameambiwa na Sheni aje afanye utaalamu Mnazi Mmoja, sasa ataendelea kuwepo mnazi mmoja na dada na mama zetu ndio wanapoenda kujifungua na yeye nasikia ndio daktari mkuu .. nilivosikia miaka hiyo..

  watu ambao Allah ameshapiga mihuri nyoyo zao wasifahamu ndio wenye dalili kama hizi ..

 8. mzeekondo 28/12/2016 kwa 1:00 mu ·

  Naomba mniruhusu na mimi kuleta masikitiko yangu kuhusu kauli chafu zilizotolewa na huyu Mzanzibari mwenzetu wa asili,mengi yamesha ongelewa hapa na waungwana wenzetu kuhusu hatua gani zichukuliwe dhidi yake,baada ya kufanyika uchunguzi wa kina kujua kwa nini mtu kama yeye anae ijua fika dini yetu,mila zetu,tamaduni zetu,ustaarabu wetu na miiko yetu mpaka kufika kutamka haya ambayo sithubutu kuyakariri hapa.

  Wengi tulijaaliwa na kubahatika kusafiri ndani na nje ya nchi au mipaka yetu, kusoma au kuwa na elimu kubwa,kidogo au kuwa kichwa kitupu, haikuwa sababu wala kisa cha kuanza kufikiri upya kama kuna Mungu wawili, au hakuna dini ya haki,haya ni maamuzi ya moyo wa muhusika, akisaidiwa na kichwa chake binafsi, kwa sababu, Dini ni Imani, na kama huna imani,utamaliza vyuo vyote vya elimu, vikuu na vidogo,iwe vya elimu dunia au akhera,lakini mwisho utaipata sababu uikatae dini yoyote, iwe umezaliwa nayo au umeiazima kwa wenyewe kisa hukuwa na IMANI tangu awali.

  Kutendewa wema/ukarimu na wasio amini dini yoyote kama ipo nyingine, zaidi ya ile ya haki yaani UISLAMU, sio kigezo cha kuanza kuyatafakari maasi yote unayo yajua, yanayo fanywa na waumini wa dini yetu, basi iwe ndio cheti cha wewe kuihama dini yetu/ yako kwa kuwa umefadhiliwa,dini ina mitihani yake mingi utakutana nayo katika uhai wako, ndio maana imani peke yake ndio itakayo kuongoza katika kufaulu safari yako hakuna kingine.

  Binafsi nimeyaona na kusikia mengi ya ajabu na kushtusha, yaliotoka vinywani mwa vijana wakati huo sote tukiwa nje na umri ndio huo ulio tupachika jina la ujana,sitosahau wakati tuko syria kuna sahib yangu mmoja mzanzibari kama mimi, tena muislamu baada ya siku hiyo dhiki kuishinda faraja, akaanza kuongea maneno ya kuudhi kama sio kutisha,alianza kwa kusema hakuna Mungu,kama hilo halikutosha, akaendelea kunena kuwa, kama yupo basi sisi watu weusi sote tutaingia peponi bure,hakuna kiingilio wala sababu ya kusali au hata kuwa na dini, kwa kuwa mateso tunayo pata hapa duniani, hawezi kutuhukumu kwani kila kiumbe humu duniani kinatubagua sisi.

  Huyu mwenzetu alikuwa hasali popote, wala haingii tena msikitini,nini kilimsibu mpaka akaamua kuwa na kauli hizi ugenini anakijua yeye, lakini mimi binafsi sikuchoka kumkumbusha kuwa kufuru sio jawabu ya matatizo yake,bali imani ndio itakayo mfanyia wepesi wa uzito ndani ya moyo wake,ilipita miaka zaidi ya ishirini sikuonana na muungwana huyu, lakini siku moja ghafla nikakutana nae Dare salaam pale clock tower,nika msimamisha, tulipomaliza kulicheza dansi{kukumbatiana}na kupeana salaam, tukaulizana mengi na wapi tulipopoteana.

  Kwa kuwa wakti wa sala ulikuwa hauko mbali, YEYE akaniambia, anakimbilia Msikitini, na mimi nikamwambia niko na usafiri pamoja wenzangu wawili, tutawahi kusali msikiti wa karibu na tunapo elekea,sikuthubu kumuuliza zile kauli zake za Syria vipi, bado ana msimamo ule ule, wa peponi na WATU WEUSI WATUPU,kwa kuwa jawabu ilikuwa wazi amerudi kwa Mola wake, na hilo ndio muhimu.

  Muhimu tukumbuke kuwa sisi sio watu wamoja katika kufikiri na kuwaza katika nyakati tofauti,mitihani tunayo kutana nayo hapa duniani, wengi tutateleza, na wengi tutanusurika INSHALAAH, muhimu kufundishana mema na kukatazana mabaya siku zote,sote tuta hukumiwa kwa mujibu wa viwango vya amali na dhambi zetu, wala asijinasibu mtu, hii ni himaya ya Mola,hatuwezi kuijua safari ya kila muumini,Subhana mwingi wa rehema, ndie mwenye kujua nani ataon’goka lini, au atateketea mpaka siku ya kuaga dunia na hatopata pumzi za kuendelea kukufuru siku gani.

  Tuchunge sana midomo yetu,ulimi mwepesi sana kurowa mate, ukishakuwa mbichi basi usiugeuze kama tairi lililojaa girisi, unateleza tu, mengine yatatushinda kuyarudisha kinywani yakisha toka.

  Nawashukuru waungwana.

 9. MAWENI 28/12/2016 kwa 8:35 um ·

  Ahsante Mzee Kondo.

 10. rasmi 28/12/2016 kwa 8:38 um ·

  Naomba kuchangia kwa upande wangu pia namna ninavyolionana hili suala la huyu Mr Gordon McGregory kutoka Scotland kama alivyojiita mwenyewe na kukataa kwamba yeye ni Abdullah.

  Hapa kuna suala hili la ELIMU na ni elimu gani utakumbana nayo ambayo inaweza kukujenga ama kukubomoa, niliwahi kusikia kwamba kama lilivyo tumbo, na akili pia inahitaji chakula, ila ni aina gani ya chakula utachokitia tumboni kikakusokota tumbo pia na akili kuna chakula ambacho ukikitia matokeo yake ni sumu ambayo itakusokota pia akilini maisha yako.

  Elimu ulimwenguni ipo nyingi, hakika unapotembea pia akili hailali bali inasoma mazingira iliyoizunguka, ni aina ya elimu ambayo huganda kichwani ama kupuuzia inachokiona, bali usidhani kupuuzia ulichokiona hakibaki akilini, matokeo yake ni matendo utayoyafanya bila kujijua kwamba ni matokeo ya hayo hayo uliyoyaona na akili kuyapokea.

  Kwa sisi tulio huku ughaibuni nakumbuka kipindi nafika katika maduka rafu ya juu kuna magazeti ya uchafu, ukiingia tu huwezi kuyakosa kuona, siku za mwanzo ilikua nastajabu kwamba watu wanaingia humo bila kutizama juu, bali nami ilifikia wakati nikiingia hata sijali tena kwamba huko juu kuna magazeti,kiukweli nimesahau hasa kwamba yapo! akili imeshajizoesha kupotezea, ila usifikiri imesahau!

  Tuliwahi kusikia watu wa enzi hizo wakipelekwa Urusi kusoma, wanaporudi huwa hawaamini Mungu tena, Je unajua ni aina gani ya elimu walipambana nayo!

  Ama wenzetu ambao walizaliwa katika imani ya Kisuni utu uzimani wakahisi ni bora Ushia. Je unajua ni aina gani ya elimu walipambana nayo!

  Walimwengu wanayo elimu ya kukutoa katika unachokiamini hatua kwa hatua, ni elimu kamili. Tizama kizazi tulichokuja nacho wakiwa wadogo katika nchi za ughaibuni tabia zao, Je unahisi ni sawa na sisi tuliokuja watu wazima?

  Ninachokikusudia kusema hapa ni hichi, dunia hii kuna elimu tofauti ambazo ni chakula kwa akili yako, utapopambana na elimu ambayo ni sumu kwa akili yako inategemea msingi uliopewa je ni imara, na huo pia kama maji yanavyokula ardhi pia ujue kwamba hata akili yako msimamo wako kullngangana na mazingira unabadilika bila hata wewe kujijua pia, ndipo nilipotoa mfano wa watoto wetu na sisi tulivyo tofauti zetu.

  Usidhani kwamba ukishuka tu katika nchi yenu kwamba watu hawatojua kwamba wewe ulikua hupo hapo muda mrefu, ama kwa kudhani kwamba kiswahili chako kiko sawa na wao bado!

  Huyu Dk amekula sumu ya kielimu, kama ilivyo kuwa ukila sumu tumboni ni bahati nasibu kupona basi na huyu pia sumu iliyo akilini mwake ni bahati nasibu kupona,

  Usiombe kukumbwa na elimu itayokuchanganya kwani hadi hii leo watu wanashindana je dunia ni duara ama tambarare! Daktari amejichanganya hapo, anahisi anaujua ukweli wa anachokitamka.

  Kama kilvyo kisu inategemea utakitumiaje kukusaidia ama kudhuria mtu, daktari ametumia akili yake kuuamrisha mdomo wake kudhuru.

  Kosa kubwa alilolifanya Iblisi ni kutakabari, unapofikia kiwango cha kujihisi unajua basi ni wakati wa kujua kwamba umerudi zero kama IBILISI. Kosa hili bado linaendelezwa na mfano wa akina daktari Abdallah.

  Natangulliza indhari kwamba mimi sijui, mjuzi zaidi ni yule aliyeniumba.

Comments are now closed for this article.