VIDEO- MANYANYASO YA POLISI KWA WANAKIJIJI WA KENDWA 2

Written by  //  29/12/2012  //  Habari, Vidio  //  3 Comments

About the Author

View all posts by

3 Comments on "VIDEO- MANYANYASO YA POLISI KWA WANAKIJIJI WA KENDWA 2"

  1. makame silima 30/12/2012 at 10:54 mu ·

    FUNDI MITAMBO/ MSAMARIA MWEMA YOYOTE NAOMA MUINGIZE HII NASAHA YA NDUGU YETU BI SALMA KWA JAMII YETU YA KIZANIBAR KATIKA DASBODI .

    Tutenganishe shughuli za serikali na CCM

    Salim Said Salim

    MUDA mrefu sasa pamesikika malalamiko mengi juu ya watumishi wa umma kuona wanawajibika zaidi kwa chama tawala cha CCM . Watu hawa wanaonekana kusahau au kudharau kuwa wanawajibika ili kuwatumikia wananchi wote kwa misingi ya usawa kwani wao ndio wanaolipa kodi zinazowapatia mishahara yao mwisho wa mwezi na kuwalipia petroli, posho na marupurupu wanapostaafu.

    Vilevile ni fedha za wananchi na si za CCM wala CUF au CHADEMA ndizo zinawalipia matibabu yao nje ya nchi wakati mwananchi wa kawaida huhangaika katika hospitali za serikali ambazo zina uhaba wa madaktari wataalamu, vifaa na dawa.

    Viongozi wa serikali wakiumwa kidogo tu haraka haraka wanapelekwa kutibiwa Ulaya, India au Afrika Kusini kama vile hospitali za hapa nchini ni za kuwahudumia wanyonge tu.

    Tusione watu wanakaa kimya, lakini hili linazungumzwa kwa masikitiko katika karibu kila baraza ya karata au kahawa na maskani za vijana. Hali hii haikubaliki katika mfumo wa utawala bora wa kidemokrasi inaonekana zaidi miongoni mwa baadhi ya viongozi ambao wanajifanya kama hawajui kwamba wao ni watumishi wa serikali na si vyama vya siasa.

    Hivi karibuni mwenendo huu hauonekani kukemewa na viongozi wa juu wa serikali, kama vile kufanya hivi ni sahihi na ndivyo wanavyotarajiwa kufanya. Ninaeleza hivi kwa sababu naona mwenendo huu wa kutotenganisha shughuli za serikali na za vyama vya siasa hausaidii kujenga demokrasi ya kweli na unachochea uhasama na watu ambao si wanachama wa CCM kuhisi na kuamini serikali yao haiwatendei haki na inawabagua.

    Matokeo yake ni kwa wananchi hao kupoteza imani kwa serikali yao na ili kuonesha hasira zao ndiyo maana hukataa kushirikiana nayo kama ilivyojitokeza katika zoezi la hivi karibuni la kuhesabu watu (sensa). Hivi karibuni lilifanyika zoezi la kukusanya maoni juu ya aina ya katiba ambayo Watanzania wanaitaka na katika baadhi ya maeneo kilichojitokeza ni vurugu tupu.

    Kwa upande mmoja viongozi wa vyama vya kisiasa walinyooshewa vidole kwa kuhusika na vurugu zilizosababisha baadhi ya mikutano ya kukusanya maoni kuvunjika. Ukweli ni kwamba viongozi wengi wa serikali hata baadhi ya mawaziri, walihusika kwa njia moja au nyingine kusababisha hizo vurugu.

    Waliojitokeza wazi kuonesha utashi mkubwa wa kisiasa na kufanya kazi kama makada wa CCM na si viongozi wa serikali ni baadhi ya wakuu wa wilaya. Katika zoezi hili la kukusanya maoni ya katiba wakuu wa wilaya ndio waliokuwa na jukumu la kuandaa na kufanya matayarisho ya kukusanya maoni katika wilaya zao.

    Badala ya kuifanya mikutano hii ni ya wananchi waliigeuza kuwa ya CCM. Kwa mfano, katika mikutano miwili, uliofanyika Michenzani na ule wa Mpendae, mjini Unguja, viti vilivyotumika vilikuwa na maandishi ya CCM nyuma.

    Hii ni kusema viti vile vilikodiwa au kuchukuliwa kwa hisani kutoka moja ya matawi au maskani za CCM. Hivyo kweli matukio haya ni ya bahati mbaya au ni kuonesha kile wana CCM wanachokiita jeuri ya chama chao?

    Tujiulize kwa nini haikutokea bahati mbaya ya kukodi viti vilivyokuwa na maandishi ya CUF, CHADEMA, NCCR-Mageuzi au chama kingine cha siasa?

    Afadhali kama viti vile vilikuwa na maandishi ya kikundi cha taarabu au klabu ya kandanda kwa sababu sehemu hizi zina wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa na imani ya dini.

    Utafiti wa haraka haraka unaonesha kitendo cha kutumia viti vilivyokuwa na maandishi ya CCM kiliwaudhi baadhi ya watu, wale wa vyama vya upinzani, na hali hii kuchangia kwa njia moja kutokea kwa vurugu zilizoshuhudiwa. Hapa tujiulize, hivi kupeleka viti vyenye maandishi ya CCM katika mikutano ya kukusanya maoni ya katiba kulikuwa na lengo gani kama si kuudhi baadhi ya watu na kuchochea vurugu?

    Ni vizuri kwa viongozi wa juu wa serikali kuitafakari hali hii kwa umakini na kuacha kuweka mbele utashi wa kisiasa na kulinda watu wanaovunja sheria kwa misingi iliyozoeleka ya kusema waliofanya hayo ‘ni wenzetu’ au ‘tumetoka nao mbali’. Kwa kweli hawa si wenzetu na kama tumetoka nao mbali basi wanapotupeleka ni mbali zaidi na hatukujui.

    Zanzibar, kwa kiasi fulani, imetulia tangu kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa licha ya hivi karibuni kuchomoza dalili za kutofautiana katika baadhi ya mambo kwa viongozi wa vyama vya CCM na CUF vinavyounda serikali hii.

    Ningelipenda kukumbusha mfano mzuri aliouonesha Rais mstaafu wa Awamu ya Tano, Dk. Amani Abeid Karume, ambaye hakuchelea kumfukuza kazi mkuu wa wilaya mmoja aliyeonesha kebehi kwa mpango wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

    Mara tu baada ya Rais Karume kuchukua hatua ile viongozi wengine wa serikali na hata wa CCM waliokuwa wanafanya kampeni za wazi wazi kupinga kuwepo serikali ya umoja wa kitaifa waliufyata baada ya kuona serikali isingevumilia mwenendo wao wa kutaka siasa za uhasama kuendelea Visiwani.

    Sielewi na sifahamu kwa nini viongozi wa serikali wanaotaka kuchafua hali nzuri ya hewa iliyoanza kustawi Zanzibar wanavumiliwa. Narudia kusema mwenendo wa baadhi ya hawa wakuu wa wilaya ni sawa na kupanda mbegu mbaya na mavuno yake yatakuwa mabaya.

    Viongozi wanaofaa kulindwa ni wale wanaofuata sheria za nchi na kufanya mambo yanayowaleta pamoja wananchi na si kuwagawa katika mafungu na kufanya mambo yenye ishara ya kutaka kuchochea siasa za chuki na uhasama.Viongozi wa serikali si tu wanapaswa kuelewa umuhimu wa kutenganisha shughuli za serikali na vyama vya siasa, lakini vitendo vyao vioneshe wanafanya hivyo.

    Vyinginevyo Zanzibar itajikuta inarudi hatua kadha mbele na watu wa Visiwani watapokuja kutanabahi na kujiuliza kulikoni watajikuta wamechelewa. Kitakachotokea ni majuto na kujilaumu kwa nini tuliwaachia mkono mrefu watu waliofanya mambo ya kuwarejesha nyuma watu wa Zanzibar.Tukumbuke wosia wa hekima na busara ya wazee wetu waliotuambia majuto ni mjukuu au usipo ziba ufa utajenga ukuta.

    Lakini hatari ninayoiona huko usoni ni kwamba huenda ikawa si ya kujenga ukuta tu bali ya kubaki na kiwanja chenye kichaka na kuanza upya kusafisha hicho kichaka na baadaye kujenga nyumba nyigine huku vifaa vya kuifanya kazi vikiwa haba au havipo kabisa. Nasema ‘aste aste’ Wazanzibari…mti na macho, mbele kuna kiza, kwahivyo ni vema tukawasha taa na kuona huko tunakokwenda!

    Chanzo tanzania Daima

  2. Makame Ame 30/12/2012 at 11:34 mu ·

    Ndugu zangu
    Tuwe na subira. Sisi wanchi hohe hahe (kama ndugu zetu wa Kendwa – waume , wake na watoto) pengine hatuna silaha ya kuonekana na kuwa na nguvu dhidi ya nguvu za dola. hilo lisitutishe. Baada ya kuona video hii imenipa moyo kwamba silaha yetu ambayo ni imani yetu kwa AQllah SWT tunayo na ina nguvu kuliko hizo bunduki na mabomu yao. Iko siku imani hii itasinda.
    Ya Rab taqabbal dua na uwalipe madhalimu hawa jazaa yao hususan kwa kuwapiga watu wasio na hatia. Ewe Allh unusuru Uislamu na Waislamu Amen.

  3. Zanzibar Moja 30/12/2012 at 12:19 um ·

    Nadhani makala ya hapo juu ni ya Salim Said na sio Bi Salma @ Makame Silima.

Comments are now closed for this article.