Tungejua tungeamua aina ya muungano kwanza: PINDA

Written by  //  06/08/2014  //  Habari, Kitaifa  //  Maoni 11

Dodoma. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema kama Serikali ingejua, ingeanza kwa kura za maoni ya wananchi kuamua aina ya muungano wanaoutaka, kabla ya kuendelea na mchakato wa Katiba.

“Tungejua kama hali ya aina hii itajitokeza, basi tungeanza na kura ya maoni, tungewauliza wananchi kama wanautaka muungano na kama ndiyo, basi uwe wa aina gani au serikali ngapi, mtu angesema moja, mbili, tatu na kadhalika,” alisema Pinda jana kwenye Viwanja vya Bunge mjini hapa.

Pinda alikuwa akijibu swali kuhusu hatima ya Bunge Maalumu kutokana na wajumbe wa Bunge hilo ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao hivyo wakishinikiza kile walichokiita kujadiliwa kwa rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na siyo vinginevyo.

Miongoni mwa mambo ambayo yamezua mvutano mkubwa ni muundo wa muungano wa serikali tatu uliopendekezwa na tume hiyo, pendekezo ambalo linaungwa mkono na wajumbe wa Ukawa ambao wamesusa Bunge, wakati upande mwingine wenye wabunge wengi wa CCM ukitaka muundo wa serikali mbili uendelee.

Pinda alisema baada ya kupata majawabu ya aina ya muundo wa muungano wanaoutaka wananchi kwa matokeo ya kura ya maoni, basi ungekuwa wakati mwafaka wa kwenda kukusanya maoni ya wananchi kuhusu mambo mengine katika Katiba.

“Lakini ndiyo hivyo, hatukuliwaza hili kwa hiyo ndiyo tunapata taabu yote hii kwa sababu kama mnavyoona bado hatujakubaliana, lakini wenzetu mpaka sasa hawajafika bungeni na mambo kama hayo. Lakini bado tuna imani kwamba busara zitatumika ili mchakato huu uwe wa maridhiano ya wote,” alisema Pinda na kuongeza:

“Katika kukusanya maoni ambayo tunayafanyia kazi sasa, Tume ya Jaji Warioba (Joseph, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba) ilikusanya maoni mchanganyiko na utakuta pengine suala hili la aina ya muungano halikuwa na mchango wa watu wengi.”

Alisema kama suala la aina ya muungano lingekuwa limetafutiwa suluhu mapema, mambo mengine yote yangejadiliwa na kuafikiwa kwa kuzingatia suala hilo ambalo linaonekana kuwa ni nguzo muhimu ya Katiba.

Alisema jitihada bado zinaendelea ili kuwashawishi Ukawa warejee bungeni na kwamba katika meza ya majadiliano hakuna kinachoshindikana.

“Ninaamini kwamba hizi tofauti zinaweza kuondoka kwa majadiliano, ni suala la kukubaliana kwamba ninyi chukua hiki na sisi tunabaki na hiki na hapo mchakato unaendelea,” alisema.

Alisema imekuwa vyema kwamba kanuni za Bunge Maalumu zimebadilishwa ili kuwezesha wajumbe kujadili maeneo mengine katika Rasimu ya Katiba ambayo hayana utata na kwamba suala la muungano linaweza kupewa fursa baadaye na wakati huo mwafaka unaweza kuwa umepatikana.

Na Neville Meena, Mwananchi

Posted Jumatano,Agosti6 2014 saa 9:38 AM

Kuhusu Mtunzi

View all posts by

Maoni 11 katika "Tungejua tungeamua aina ya muungano kwanza: PINDA"

 1. kiux 06/08/2014 kwa 2:02 um ·

  Hawa kina pinda wao siwanajisifu kuwa wanaweza kuamua lolote iweje aseme hivyo, kamakura yamaoni, waznz walidai sikunyingi wakapiga mabomu ya machozi na virungu, kama kweli wanania ya kupata katiba yenye mariziano livunje bunge la katiba turudi kwa wananchi waulizwe wanautaka muungano au hawautaki na kamawanautaka waseme niwaaina gani?

 2. sale 06/08/2014 kwa 2:50 um ·

  @kiux hata mi nakumbuka,,,

 3. Msemaji mkuu 06/08/2014 kwa 4:30 um ·

  Pinda anasema hayo akijua kwamba anazungumza unafiki. Suala la kura ya maoni kabla ya mchakato wa katiba lilipigiwa kelele sana na Wazanzibari kwamba ndio jambo muhimu la kufanywa .

  Walilikataa kwa kuogopa kwamba Zaznzibari wangeukataa muungano, jambo ambalo mpaka sasa linawatia woga.

 4. santorini 06/08/2014 kwa 6:26 um ·

  Pinda hodari wa kuchokonyoa,sasa na wailete kura ya maoni na ndipo tutakapoukataa muungano kwa kura si chini ya asilimia 70 kwani tunajua fika kama CCM tu ambao watataka serikali mbili na baadhi yao wataukataa kabisa.
  Viongozi wetu zanzibar walitupiga kila aina ya kipigo kwa kulazimisha mchakato wa katiba na kuikataa kura ya maoni , sasa katiba imeshatengenezwa kazi kujipara vichwa mpaka wametoka vipara na wengine wamevimba mashavu kwa safura kwa kukosha kula chakula cha siha .
  Karibu kura ya maoni , zanzibar kwanza ,muungano wa mkataba na CCM kifo cha mende miguu juu.
  Dua za mashekhe wetu zinawapa kiwewe hatutambuani,unafiq umezidi kutiliana wao kwa wao hata maskini msema kweli wamemtafutia njia ya kumdhibiti kinafiq ati anamiliki silaha kinyume chasheria .
  Bado dua hazitaishia hapo mpaka kila mnafiq ataadhirika duniani na akhera .
  Ukawa toeni somesho kwa ccm mpaka wajue kama ccm si wenye hati miliki ya kuiongoza nchi hii ,bali kila mwenye uwezo ,busara ,imani na wananchi wake ndie ataepata kibali cha kuiongoza kwa ridhaa ya wananchi wenyewe.
  UKAWA OYYYYYYYYYYEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEE

 5. best leader 06/08/2014 kwa 7:17 um ·

  Iyo Leo tena. Eti kama tungejua. Ama kweli pinda we we umepinda. Siku zote watu walipokua wakipiga kelele kua tupige kura ya maoni kuhusu muundo wa mungano kwanza mlikua viziwi au?
  Viongozi wengine bwana! Wapowapo tu hawajui mini wakisemacho wala wakitakacho.
  Hata firauna alisema maneno mfano wake kama hayo. Eti tungejua! Siasa za kinafiki tu na uongo ndio kazi yenu.hay a sasa mmeshajua leteni hio kura ya maoni tuamue kuhusu muundo wa mungano kabla kuendelea kujadili serikali zenu mbili.

 6. makunduchi 06/08/2014 kwa 8:31 um ·

  wee maluuni pinda amakweli umepinda wewe na mabunju wenzako.
  leo unasema kwamba kama mungelijua kama itakua hivi ni bora mungeli itisha kura ya maoni kwanaza na kuawauliza wananchi kama wanautaka muungano au hawautaki na kama wanautaka ni wa aina gani.ni hivi wazanzibari tuliamua zamani kushajihishana pamoja na kuawaamsha nyinyi mlio lala kuhusu muungano na kura ya maoni lakini muliamua kutoa maneno ya jeuri mukisaidiwa na Dr.shein na kusema kua nyinyi hamutaki kuamshwa kwani mumeamka zamani sasa leo kura ya maoni ya nini.endeleeni tu na kuwakamata mashekh zetu wa zanzibar maana nyinyi kazi yenu ni kuzulumu naomba muungu awalaani lana ya firiauni na awaue kama makafiri alivyowaua siku ya vita vya badri.amin.
  awazanzibari hatutaki kura ya maoni bali hatutaki laana hii ya muungano dhalimu hu wa kiyahudi.

 7. makunduchi 06/08/2014 kwa 9:03 um ·

  someni hii je haiendani na mazingira ya sasa
  ” ZANZIBAR imepata Kamishna mpya wa Jeshi la Polisi, Hamdani Omari Makame.

  Uteuzi huu uliofanywa karibuni na Rais Jakaya Kikwete umekuja muda mrefu tokea kuzuka shaka miongoni mwa baadhi ya watu juu ya uwezo wa kuliongoza jeshi hili Visiwani, wa aliyekuwa akishika nafasi hiyo, Mussa Ali Mussa.

  Sasa Mussa amehamishiwa makao makuu Dar es Salaam kuwa Kamishna wa Polisi Jamii na ninamtakia kila la kheri. Labda huko atawajibika kama anavyotarajiwa ofisa anayeongoza kikosi hiki.

  Kwa kweli kamishna mpya anaanza kazi akikabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo ile ya kurudisha imani ya raia wengi juu ya utendaji kazi wa jeshi hili katika kulinda usalama wa raia na mali zao.

  Inasikitisha kuona hata usalama wa mali za polisi ndani ya jeshi hili ulipotea katika utawala uliopita kutokana na kile unachoweza kukieleza kama aibu. Hii inatokana na kuibiwa upanga wa dhahabu uliokuwa mikononi mwa Jeshi la Polisi Zanzibar.

  Upanga huu ni mali ya Shirikisho la Wakuu wa Majeshi ya Polisi wa nchi za Kusini mwa Afrika (SARPCCO) na huwa mikononi mwa jeshi la nchi ambayo kiongozi wake huwa mwenyekiti wa shirikisho kwa kipindi cha mwaka mmoja.

  Upanga ulipoibiwa ulikuwa ni wakati Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania, Said Mwema, alipokuwa anamaliza muda wa uongozi wa shirikisho katika mkutano uliofanyika Zanzibar mwaka jana.

  Kwa mtazamo wa watu wengi, kashfa ya wizi wa upanga ule wenye thamani ya mamilioni ya shilingi ni kielelezo tu cha kile kinachoonekana kuyumba kwa muda mrefu Zanzibar kwa uongozi wa jeshi hili lililopewa dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao.

  Watu waliuliza baada ya kutokea wizi ule uliotia aibu nchi katika jumuiya ya kimataifa kama polisi hawawezi kulinda kilichokuwa mikononi mwao watawezaje kulinda kilichopo mikononi mwa wengine? Tunataraji aibu kama hii haitarudiwa. Hatajirudia.

  Mbali ya kashfa hii pamekuwepo na lawama kuwa ukereketwa wa kisiasa (sina hakika kama ni wa CCM, CUF CHADEMA au chama kingine) ulimsumbua kamishna Mussa na kuathiri utendaji wake wa kazi.

  Vikundi vya watu viliweza kuvuruga mikutano ya siasa ya vyama vingine na waliohusika hawakuguswa. Siku hizi wahuni hawa wanatukana viongozi hadharani na mikanda ya mikutano hiyo inaonyeshwa katika baadhi ya maskani za CCM. Wanaofanya hivi hawaguswi.

  Hii sio haki, na sheria za nchi yetu hazikubali hivyo, lakini kamishnna aliyepita alifumbia macho haya na kuonekana kuongoza jeshi kisiasa, badala ya kufuata sheria.

  Mifano mingine ni kwa polisi kufumbia macho na kutowawajibisha wahuni wanaokuwa na ujabari wa kutaka Unguja na Pemba zitengane. Kamishna aliyepita alifumbia macho uchochezi huu.

  Hivi karibuni tu watu hawa walibwabwaja matusi ya nguoni katika mkutano uliofanyika Mji Mkongwe na polisi walikuwepo hapo.

  Jeshi hili vile vile limekuwa likifumbia macho hata mabango ya matangazo ya hao wanaojiita “mabwana na mabibi wakubwa wa Zanzibar” ambao kazi yao kubwa ni kuandika maneno ya kukashifu watu.

  Baya zaidi ni ukosefu wa diplomasia wa kamishna Musa wa kutoa matamshi yaliyowashitua watu Visiwani na nje, na hata kutaka kuathiri sekta ya utalii ya Zazibar kwa wageni kuhofia kuja Visiwani.

  Ilikuwa kawaida kumsikia kamishna aliyepita pale panapotokea kitendo cha uhalifu kukurupuka kuwa vikundi vinavyodaiwa kuhusika na ugaidi vya Al Qaeda na Al Shabaab kuhusika na wafuasi wa makundi haya wapo Zanzibar.

  Sijui wapi kapata taarifa hizi, na anao ushahidi gani na kwanini hao anaowaita Al Qaeda asiwawajibishe kisheria au alikuwa anangojea yatokee kama tuliyoyashuhudia Kenya?

  Kauli hizi za hatari zilizusha vurugu na kuwa mada kubwa katika mitandao ya kijamii nchini na ya kimataifa. Baadhi ya mabalozi wa nchi za nje walifika hadi kuwaambia raia zao wawe na hadhari wakifika Zanzibar. Yote haya ametuzulia kamishna aliyepita.

  Ninakumbuka IGP Mwema alipochaguliwa kushika nafasi hiyo nilimuomba atende wema na aende zake na asingoje shukrani kwa vile nchi yetu bado mtu huhukumiwa kwa kosa analofanya na sio kwa wema wake (kama lilivyo jina lake).

  Sasa kazi kwako Kamishna Hamdani. Ni muhimu kama unafanya ihsani basi iwe ndani ya sheria za nchi na uelewe wapo waliojenga mazoea ya kuwa na haki ya kulielekeza Jeshi la Polisi namna ya kufanya kazi.

  Watu sio rahisi kuacha kuendeleza mazoea kwani mazoea yana tabu na hasa kama tabia (ukekereketwa) ukilingana.

  Lililo muhimu ni kutopenda au kumchukia mtu au kikundi cha watu, bali kuwapenda wanaoheshimu sheria.

  Kama ni kupata maelekezo ya utendaji kazi, basi ni katiba, sheria, vitabu Penal Code na Criminal Procedure Codes na maelekezo ya viongozi wa juu wa jeshi na nchi.

  Hakuna mwenye haki ya kukuingilia au kukufundisha kazi, na asiyeridhika na utendaji wako wa kazi apeleke malalamiko yake kwa wakubwa wako au afungue mashitaka mahakamani.

  Hili ni jeshi la Watanzania wote, wanaume na wanawake, vijana na wazee, wanachama wa vyama vyote vya siasa, taarab, kandanda na vyama vingine vilivyosajiliwa nchini.

  Hapana shaka jukumu hili ni zito na sio kama la kuuza karanga au muhogo wa kuchoma. “

 8. Alberta 07/08/2014 kwa 7:22 mu ·

  @ Pinda

  Kwani muheshimiwa mumeungana na nchi gani wakati tayari ulisha thibitisha kuwa Zanzibar sio nchi na ndoo munavyo ifanya hivyo sasa hivi kiongozi wenu wa Tanganyika yuko Marekani natumilia jina la Tanzania.

  huku mkitudhalilishia watu wetu mlio wapeleka Tanganyika

 9. Alberta 07/08/2014 kwa 7:22 mu ·

  @ Pinda

  Kwani muheshimiwa mumeungana na nchi gani wakati tayari ulisha thibitisha kuwa Zanzibar sio nchi na ndoo munavyo ifanya hivyo sasa hivi kiongozi wenu wa Tanganyika yuko Marekani natumilia jina la Tanzania.

  huku mkitudhalilishia watu wetu mlio wapeleka Tanganyika

 10. salali 07/08/2014 kwa 9:19 mu ·

  Hata tume ya maridhiano chini ya capten (moyo) walisema waulizwe wananchi kwanza ni Aina gani ya muungano iwapo watautaka wakafika kusema huko ni sawa na kutanguliza gari ya farasi kwanza.Leo Pinda anayaona,waliyoyaona kamati ya maridhiano miaka miwili na ushee nyuma,Huyu kama si waziri mzigo ni kitu gani?…..

 11. nuramo 07/08/2014 kwa 8:39 um ·

  Kama wewe Pinda unalijua hili sasa hivi sisi Wazanzibari tumelijua zamani ndio maana tukatoa maoni hayo tu ya Muungano wa Mkataba tunajua tukipata mkataba mambo mengine yanakuja automatic

  Kama sala inapokamilika na mambo mengine yanakamilika basi ndio hivo

Comments are now closed for this article.