Tanganyika kupata magari 58 kutoka WHO

Written by  //  15/12/2016  //  Habari  //  Maoni 3

Hizi ndio faida za muungano,japo gari moja itakuwa imeletwa zanzibar 😊😊😊 shaka hamdu upo? Wawakilishi wetu wa baraza la mapinduzi mupo?

Waziri Ummy Mwalimu

NA VERONICA ROMWALD– DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA), wameipa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto magari 58.

Who imetoa msaada wa magari 50 ya kubebea wagonjwa (Ambulance) na UNFPA imetoa magari manane ambayo yatatumika kuratibu shughuli za afya ya mama na mtoto.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya makabidhiano ya magari hayo, Waziri Ummy Mwalimu, alisema yatagawiwa katika mikoa sita iliyopo Kanda ya Ziwa.

“Tafiti zilizofanywa mwaka 2010 na tathmini iliyofanywa mwaka 2015 wakati wa kuandaa Mpango wa Matokeo Makubwa sasa (BRN), mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwamo Kigoma ilionekana kuwa na viashiria hafifu vya afya ya mama na mtoto,” alisema.

Akitolea mfano alisema mikoa hiyo ilionekana kuwa na utumiaji mdogo wa huduma ya uzazi wa mpango, wanawake wachache ndio waliojifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya na kuna idadi kubwa ya vifo.

“Wanawake wengi wanafariki dunia kwa uzazi nchini, hii ni changamoto kubwa kwetu, tumepambana kwa miaka 20 tumefanikiwa kuvipunguza kutoka vifo 580 hadi 432 kwa kila vizazi hai 100,000.

“Nia yetu ifikapo 2020 tuweze kupunguza tena idadi hiyo kutoka 432 hadi 292 sawa na asilimia 30 pamoja na vifo vya watoto wachanga kuvipunguza kutoka 54 ya sasa hadi 40 kwa kila vizazi hai 1,000,” alisema na kuongeza:

“Hivyo magari haya yatapelekwa katika mkoa wa Mwanza, Geita, Kigoma, Simiyu, Kagera na Mara.

Aliwataka waganga wakuu wa mikoa ambao watakabidhiwa magari hayo kuyakatia bima ya ajali ili yaendelee kudumu kutoa huduma kwa wananchi.

Mwakilishi Mkazi wa UNFPA-Tanzania, Dk. Hashina Begum, alisema magari hayo manane waliyoyatoa yana thamani ya Sh milioni 387.

“Tuna imani kwamba yatakuwa msaada mkubwa kwa Serikali katika kusimamia shughuli zote za uratibu wa afya ya mama na mtoto na hivyo kufikia lengo la kupunguza idadi ya vifo iliyotajwa,” alisema.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa WHO, Dk. Grace Saguti, alisema ambulance hizo zilizotolewa zitakuwa na huduma zote muhimu.

“Tumetanguliza hizi 50 zenye thamani ya Sh bilioni 5.9, lengo letu ni kuipatia wizara ya afya jumla ya ambulance 67,” alisema.

Kuhusu Mtunzi

View all posts by

Maoni 3 katika "Tanganyika kupata magari 58 kutoka WHO"

 1. jazba 15/12/2016 kwa 8:02 um ·

  na zanzibar tutapata magari mawili kutoka kwenye mgao wetu wa kisanii 4%,ingawa afya si jambo la muungano lakini kwa usanii na ulahgai ili tujione kama na sie tumo tutapewa gari mbili, moja tutapeleka pemba na moja unguja hio ndio haki yetu stahiki.

  Pengine ingelikuwa muungano ni wa haki tusingepata hata gari moja,au kama tungekuwa hatupo kwenye muungano huu pengine tungekuwa maskini wa kutupa lakini muungano unajitahidi kutueka sawa

 2. Asili haipotei 16/12/2016 kwa 11:46 mu ·

  koti lamuungano ilo walilojivisha watanganyika muungano huu uwende tu Tanganyika ndo Tanzania na tanzania ndo tanganyika nonsense

 3. Tengoni 16/12/2016 kwa 5:39 um ·

  Msiwagutushe smz hawaelewi chochote kinachoendelea kule Tanzania, mpaka kijitokeze ndani ya vyombo vya habari, hapo ndio huanza kudai asilinia nne yao, inakuwa ni usumbufu tu, kwani huwa weshachelewa javini. Hao kina Samia. Hussein mwinyi, Mbarawa na Masauni, wote wanajiona Watanganyika, hawana utamaduni wa kuibonyeza smz,wanafumba macho na kula kuku wao.hilo moja la magari limeonekana, kuna mia moja kila mwaka hayaonekani, wajinga ndio waliwao.

Comments are now closed for this article.