Sikukuu mwisho saa 12 kwa watoto – SMZ

Written by  //  19/08/2012  //  Habari  //  Maoni 28

Na Mwandishi wetu
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imesisitiza kuwa wakati wa sikukuu ya Edd- el fitri, sikukuu kwa watoto itaanza mchana hadi saa 12:00 jioni.

Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakary alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kwamba “Kwa watoto Sikukuu yao itakuwa wakati wote wa mchana hadi kufikia saa 12:00 jioni”

Waziri Abubakar alisema hatua za kisheria zitachukuliwa kwa mzee wa mtoto atakayemruhusu mtoto wake kukiuka utaratibu huo ambapo pia vyombo na taasisi zinazohusika zimeombwa kuchukua hatua za kisheria kwa atakakiuka utaratibu huo.

Mbali na suala hilo, serikali imewataka wazazi na walezi kuwavisha watoto wao nguo za heshima zinazoendana na mila na maadili ya Kizanzibari na sio zile nguo za kubana au zinazoondosha heshima na mila za Mzanzibari.

“Nawaombeni sana kuendeleza amani na utulivu uliopo nchini pamoja na kuendelea kufuata maelekezo ya serikali kwa faida yetu na kwa faida ya jamii yetu” , alisema Waziri Abubakar katika taarifa yake hiyo.

Aidha, serikali imeendelea kupiga marufuku wakati wowote disko toto. “Mambo kama ya disko toto bado tutaendelea kukemea vikali na kupiga marufuku kwa wakati wowote ule”, alisisitiza waziri huyo.

Waziri huyo aliwashukuru wananchi kwa kuitikia tangazo la serikali la muongozo juu ya namna ya kuheshimu mwezi wa Ramadhani katika kipindi chote cha kufunga pamoja na kupiga marufuku baadhi ya mambo katika sherehe za sikukuu.

“Napenda kuitaarifu jamii kwamba serikali bado inaendelea kuzingatia haja ya kuendeleza tabia hii nzuri ya kulinda heshima na tabia zetu katika jamii ya Kizanzibari kwa wakati wote”, alisisitiza Waziri Abubakar.

Kuhusu Mtunzi

View all posts by

Maoni yamefungwa.