Serikali itasimamia na kutekeleza matakwa ya wananchi katika kupata Katiba mpya

Written by  //  05/07/2013  //  Habari  //  Maoni 3

Na Miza Kona-Maelezo Zanzibar

Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar imeendelea na msimamo wake wa kuwahahakikishia Wazanzibari kuwa itasimamia na kuyatekeleza matakwa yao watayokubaliana katika Mabaraza ya Katiba ili kupata Katiba Mpya yenye kukidhi mahitaji yao.

Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar Abubakar Khamis Bakary ameyasema hayo wakati akisoma hotuba ya Makadirio ya Mapato na matumizi ya Wizara yake mwaka wa fedha 2013/2014 Katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Amesema jambo la msingi kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ni kufanya maamuzi ya kujua wanataka Muungano wa aina gani na Katiba ipi ili Wananchi watakapoenda kutoa Maoni yao katika Mabaraza ya Katiba wawe na hoja za msingi.

“Kwanza ni sisi wenyewe kujua tunataka Muungano upi na Katiba ipi kasha tuwaelimishe wananchi wetu”Alisema Waziri Bakary.

Amesema Wanachi wasiwe na wasiwasi na kwamba kupitia kwa Wawakilishi wao waijadili Rasimu ya Katiba na kuona kama inakidhi haja ya kuleta Maendeleo, Maisha mazuri na haki za Wazanzibar kwa kizazi kilichopo na kijacho.

“Tuhakikishe kuwa Katiba ijayo inafufua matarajio ya Wazanzibari kwa Zanzibar yetu ya leo na siku za usoni”alisema Waziri Bakary

Aidha Waziri Bakary ameitaka jamii kufahamu kuwa Katiba inayotakiwa itabadilisha sana Taifa kisiasa, kiuchumi na kijamii na kwamba Wananchi wanatakiwa kuwa imara na mazingatio ya mabadiliko hayo.
Alieleza kuwa mabadiliko yatakayotokana na Katiba Mpya yanaweza kuwa ya karibuni na mengine kuchukua muda mrefu hivyo wananchi wajitayarishe kukabiliana nayo

Katika hatua nyingine Waziri Bakary amesema Wizara yake kupitia Idara ya Mahkama imepanga kupunguza mrundikano wa kesi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki.

Aidha Majengo ya Mahkama ya Unguja na Pemba yanatarajiwa kufanyiwa matengenezo ili kuyapa hadhi ya kisasa.

Katika kutekeleza majukumu yake Waziri huyo ameliomba Baraza la Wawakilishi limuidhinishe jumla ya sh. 8,188,000,000.00 kwa matumizi ya kazi za kawaida.

IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

Kuhusu Mtunzi

View all posts by

Maoni 3 katika "Serikali itasimamia na kutekeleza matakwa ya wananchi katika kupata Katiba mpya"

 1. alwattan 05/07/2013 kwa 7:42 mu ·

  Mh!!!!!!, hivi?!, mbona rasimu hii ilipotolewa na warioba hatujasikia hata nyoko! wakati zaidi ya 64% ya wazanzibari walitaka serikali ya mkataba na matakwa yao hayakuingizwa kwenye rasimu?.
  mimi natilia shaka haya ya Abubakar na serikali yake

 2. Ghalib 05/07/2013 kwa 9:01 mu ·

  Inasikitisha kuona majengo kama mahakama yapo kama magofu, tena mahakama kuu za zanzibar inasikitisha sana, kama wakilishi mutafatilia huo ukarabati utakao gharimu, basi naweza kusema tunaweza kujenga majengo mapya na ya kisasa.

  Hebu angalieni huko tanganyika majengo ya serikali wanavyojenga ya kisasa ? hivi kwa nini tusiwe wachoyo wa maendeleo ? Mapinduzi munayo yasifia katika viriri ni mapinduzi ya maonevu ya wananchi kila vipindi vya uchaguzi au pale wanapodai haki zao na kuwapinga hayo ndo mapinduzi.

  Mapinduzi tunayotaka sisi na muyasifie ni maendeleo ya ukweli ambayo yatakayo tunufaisha kwa sisi sote na heshima kubwa kwa kuheshimiana baina ya wananchi na serikali, leo vikosi vya police vimekuwa haramia kuwabambikia kesi wananchi ambao wasikuwa na hatia.

  Katika suala la katiba mpya, wananchi wa zanzibar hawajatafuna maneno, Mh Abubakary unajua wananchi wanachokitaka, kama hujui basi waulize tume ya katiba ambao wamechukua maoni ya katiba, au kama pia unaona it is not enough for you, itisha kura ya maoni, tutakuwambia tunautaka muungano au hatuutaki, na kama tunautaka tutakuwambia wa aina gani.

  Mimi wa kwanza siutaki. EAC unatosha.

 3. mohamed 05/07/2013 kwa 9:16 um ·

  Asalam alaykum waungwana,naomba nifahamishwe hivi,
  Zanzibar kuna serikali ngapi? maana husikia SMZ na SUK. na kama ni mbili je zote anaongoza sheni au?

Comments are now closed for this article.