Pingamizi ya matumizi ya kidini yafutwa – Mfuko wa jimbo

Written by  //  13/04/2012  //  Habari  //  Maoni 3

jussa

Alghaithiyyah, Zanzibar

Hatimae Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeondosha kifungu cha sheria cha 16 (4) kilichokuwa kikitaka fedha za mfuko wa jimbo zisitumike kabisa katika shughuli za kidini na kisiasa.

Akichangia mswada huo wa mfuko wa jimbo Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu alisema hakubaliani kabisa na hatua hiyo ya serikali ya kuwaletea mswada amabo unakataza fedha za jimbo zisitumike katika shughuli za kidini bila ya kuzingatia utamaduni wa wazanzibari ambapo asilimia kubwa ni waumini wa dini hiyo.

Kifungu cha 16 (4) kinaelezea fedha za mfuko wa jimbo hazitatumika kwa shughuli za kidini wala kisiasa na kutumia fedha hizo itakuwa ni kosa kisheria ambapo Jussa alisema kisiasa ni sawa inaweza kuwacha lakini kutumika katika shughuli za kidini hilo haliwezekani kuepukwa.

Alisema “hilo mheshimiwa Spika sikubaliani nalo kuwa mfuko wa jimbo unakataza fedha zisitumike katika shughuli za kisiasa na kidini hilo halikubaliki maana kutokana na mazingira yetu suala la kuchangia shughuli za kidini ni muhimu …ujenzi wa msikiti na kuchangia madrasa ni muhimu na mfano madrassa zinatoa elimu kwa watoto wetu na kufundisha maadili mema kuliko hata skuli za kawaida” alisema Jussa.

Aidha aliwataka viongozi wa serikali na wajumbe wa baraza la wawakilishi kuwa makini na kutokubali kutumiwa na kwa kisingizio cha kutafuta haki na kukubali kila kinacholetwa na wageni na kuacha mila na utamaduni na hali halisi ya maisha ya wazanzibari.

“Mheshimiwa Spika suala hilo hapana na wala tuslionee aibu hili tunaambiwa hili kuwa nchi yetu ni haina dini lakini tusikubali kupangiwa madhali ni mifuko ya majimbo zikubaliwe katika maendeleo ya nchi yetu na sio kila kitu tunacholetewa tunakubali tu natoa wito kwa serikali kutokubali kila wanacholetewa tukitazame jee kina faida katika maisha yetu na watu wetu na jee hakiathiri mila na utamaduni wetu maana sisi ni waislamu”.

Jussa aliongeza kwa kusema kwamba “Viongozi wetu wanachangia misikiti sijasikia kuchangia kanisa na kwa nini wao wachangie lakini wawakilishi wasichangie wakati mwengine tusikubali na mambo kama haya tusijitishe lazima tuwe wakali katika hili wanananchi wetu ndio walipa kodi wa nchi hii kwa nini wasichangiwe hili siliungii mkono kabisa” alisema Jussa huku akikunja uso na kuinamisha uso wake chini.

“Mheshimiwa Spika Uingereza pamoja na kuwa serikali tunaambiwa inaendeshwa kisekular lakini haina dini lakini bado wanaheshimiwa madhehebu yao ya kiangalikan, na hilo linatambulikana na serikali kwa hivyo na sisi suala la kuwambiwa tusitumie katika shughuli za dini haiwezekani mazingira ya nchi yetu na watu wetu tunayajua” alisema Jussa.

Akiunga mkono kauli hiyo ya kutokubali kutumiwa kwa kisingizio cha kutotumia dini katika mfuko huo Mwakilishi wa Jimbo la Mkwajuni (CCM) Mbarouk Wadi Mussa (Mtando) alisema “Nakubaliana na Mheshimiwa Jussa kwamba wananchi wetu ni waislamu sasa inakuwaje tusiwajengee wanachotaka wakati mazingira ya nchi yetu kujenga madrassa ni sehemu ya shughuli za kijamii?” alihoji Mtando.

Alisema iwapo wananchi wenyewe watapendekeza kujengewa madrassa au kusaidiwa kujenga misikiti hawawezui kuingiliwa kwa sababu hayo ni mapenekezo yao na ni chaguo katika majimbo yao.

“Sasa Mheshimiwa Spika ikiwa wenyewe wananchi kipaumbele chao, kujenga skuli au nursey za tukawajengea lakini wengine wakisema sisi tunataka mchango katika madarasasa kwa nini tusiwape wakati mafunzo ndio yale yale?… hiki kifungu nashauri kiondolewe kabisa hakifai” alisisitiza Mwakilishi huyo.

Wakichangia katika mswada huo baadhi ya wajumbe wamesema kuwepo kwa utitiri wa kamati za maendeleo katika majimbo na vijiji kunasababisha vikwazo katika ufanikishaji wa mipango na malengo ya jumuia hiyo na kutopata ufanisi.

Wajumbe hao walieleza hayo jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi uliopo Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar walipokuwa akichangia mswada wa sheria ya kuanzisha mfuko wa maendeleo ya jimbo.

Akitoa mchango wake Mwakilishi wa jimbo la Ziwani (CUF) Rashid Seif Suleiman alisema mfuko huo uunganishe kamati za maendeleo ili utitiri wa kamati zilizopo hivi sasa katika majimbo ziondoke.

Alisema wingi wa kamati hizo, imekuwa kikwazo katika kuleta maendeleo ya jamii ambapo kwa kiasi kikubwa malengo na mipango ya kimaendeleo haifikiwi.

iwapo hakutokuwa na upembuzi yakinifu kuhusuiana na wingi wa kamati za maendeleo kwa kiasi kikubwa kutaleta vikwazo.

“Kuwepo kamati nyingi za maendeleo kutakwamisha utekelezaji wa mfuko, hivyo ni vyema kuangaliwa upya na upembuzi yakinuifu ufanywe”, alisema Mwakilishi huyo.

Aidha aliwataka wajumbe wenziwe wa Baraza hilo kuhakikisha kuwa fedha hizo wanatumia ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuandika ripoti ya matumizi na kupekeka sehemu husika.

Naye Mwakilishi wa Kiwani (CUF) Hija Hassan Hija alisema uanzishwaji wa mfuko huo ni jambo muafaka kwani utaharakisha maendeleo ya wananchi.

Akitoa mfano alisema nchini Kenya, ambako wanasheria ya mfuko kama huo, wananchi wameweza kupiga hatua za maendeleo kupitia fedha za mfuko kama huo, na kuimba serikali kuupa ridhaa mfuko huko.

Mapema akiwasilisha mswada huo, waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed alisema serikali imebuni mpango huo ili kuharakisha kazi ya uletaji maendeleo ya wananchi majimboni.

Waziri Aboud, aliwataka wajumbe wa Baraza hilo kuzitumia vizuri fedha hizo na kwa malengo yaliyokusudiwa baada ya sheria hiyo kuipitisha rasmi.

Aidha alisema ripoti ya matumizi ya fedha ndio kitu muhimu zaidi kwani itaaninisha maeneo ambayo fedha hizo zimetumika.

Kuja kwa mfuko huo kumeleta faraja kwa wawakilishi ambapo mfumo wanaoutumia hivi sasa wamekuwa wakipatiwa fedha hizo kupitia Wizara ya fedha zinzoingizwa shilingi milioni 5,000,000 kwa kipindi maalum baada ya kuanisha miradi ya maendeleo wanayotaka kuitekeleza majimboni mwao ambapo husimamiwa na serikali kuu.

Tayari mfuko kama huo umeanzishwa kwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano ambapo wamekuwa wakipatiwa fedha zinazotumika kwa ajili ya shughuli za maendeleo majimboni mwao.

Kutokana na kuwapo kwa hali hiyo serikali imeamua kuweka Mswada huo ambapo umeeleza lengo lake ni kutunga sheria itayoruhusu kuanzishwa kwa mfuko wa Maendeleo ya Jimbo wa Zanzibar, kwa ajili ya kurahisisha maendeleo katika majimbo ya hapa nchini.

Chini ya Mswada huo sheria hiyo ikiwa itapitishwa na kuwekewa saini na Rais, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi watapaswa kuamua hatima ya maendeleo ya majimbo yao kwa kushiriki katika uanzishaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mujibu wa vipau mbele vyao.

Kuhusu Mtunzi

View all posts by

Maoni yamefungwa.