Maninja wa Lipumba wavamia mkutano wa CUF Dar es Salaam

Written by  //  23/04/2017  //  Habari  //  Maoni 3

mvamizi

Pichani: Mtu aliyekumbana na nguvu ya umma miongoni mwa watu wanne waliyovamia mkutano wa ndani wa CUF na kuwajeruhi viongozi wake na waandishi wa habari jana katika Hoteli ya Vina Mburahati, Dar es Salaam.

Na Mary Geofrey – Nipashe Jumapili
23 Aprili 2017

WATU wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) – (anayetambuli na msajili wa vyama vya siasa), Ibrahim Lipumba jana walivamia mkutano wa ndani wa CUF na kuwapiga na kuwajeruhi viongozi wa chama hicho na waandishi wa habari.

Sakata hilo lilitokea katika hoteli ya Vina iliyopo Mburahati, Dar es Salaam wakati viongozi wa CUF Wilaya ya Kinondoni walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu mgogoro unaoendelea ndani ya chama kati ya pande hizo mbili.

Mwezi uliopita, Lipumba alitangaza rasmi kumwondoa Maalim Seif katika wadhifa wake wa Katibu Mkuu kwa madai ya kutohudhuria vikao muhimu vya chama.

Aidha, Lipumba alitangaza nafasi hiyo kuchukuliwa na Magdalena Sakaya, ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho upande wa Tanzania Bara.

PICHA ILIVYOANZA
Mnamo majira ya saa 5:30 asubuhi wakati Mwenyekiti wa CUF Kinondoni, Juma Nkumbi na viongozi wengine wa wilaya hiyo, wakiwaeleza waandishi wa habari kile walichowaitia, ghafla watu wanne waliokuwa wameziba nyuso zao kwa kuvaa soksi maalum za usoni, walivamia na kuanza kushambulia viongozi waliokuwa meza kuu kwa kuwapiga kwa mikanda na marungu.

Maninja’ hao walifika kwenye hoteli hiyo wakiwa na magari matatu aina ya Toyota Land Cruiser Prado yenye bendera za CUF na kuingia mapokezi na kujitambulisha kama wafuasi wa chama hicho na kuuliza eneo ambalo mkutano unafanyika.

Watu hao walifika mapokezi wakiwa wamevaa nguo za kiraia jambo lililowafanya wahudumu wasiwatambue kama ni wahalifu, hasa kutokana na magari yao kuwa na bendera za chama hicho.

Baada ya kuelekezwa wakati wakipandisha ngazi kwenda ghorofa ya nne, ndiko wanakodaiwa walivaa soksi maalum ili kuficha nyuso zao.

WALIVYOTINGA UKUMBINI
Wakati mkutano baina ya viongozi wa CUF wilaya ya Kinondoni na waandishi wa habari ukiendelea, ‘maninja’ hao wanne waliingia wakiwa wameshikilia mapanga, fimbo, mikanda na bastola na kwenda moja kwa moja meza kuu na kuanza kuwashambulia viongozi hao.

Taharuki hiyo iliwafanya viongozi waliokuwa meza kuu kusimama na kupambana nao kwa kuzuia kudhuriwa zaidi na silaha walizokuwa wameshika wenzao.

Katika hali isiyotarajiwa, mmoja wa ‘maninja’ hao alitoa bastola aliyokuwa ameihifadhi maungoni na kuinyooshea upande waliokuwa wamekaa waandishi wa habari ikiwa ishara ya kuwatishia kufanya kazi yao.

Kitendo hicho kilizua taharuki kwa waandishi na kusababisha baadhi yao kuumia kutokana na kukimbia bila tahadhari.

Kutokana na mazingira ya ukumbi huo kuwa mdogo na wenye mlango mmoja wa kutokea nje ya jengo hilo, baadhi ya waandishi walikimbilia mlango wa kwenda varanda ya ukumbi na kusababisha mmoja wao kutaka kujirusha, kitendo ambacho kiliwasababishia wenzake, kumvuta na kumuokoa.

Wakati wajumbe wa mkutano huo, wanaomuunga mkono Maalim Seif, wakiendelea kupambana, ‘maninja’ hao waliwashambulia kwa kuwapiga mateke na makofi huku, baadhi ya waandishi ambao baadaye walifanikiwa kutoka nje ya ukumbi kwa kupitia mlango mkuu.

WAANDISHI WAOKOA
Waandishi waliokuwa kwenye varanda ya ukumbi huo, walipiga kelele ambazo ziliwashtua watu waliokuwa chini ya jengo, ambao walijaa kutaka kujua nini kimetokea.

Baada ya kelele hizo, ndipo maninja hao walitoka na silaha zao na kushuka hadi eneo la mapokezi ambako huko walikutana na msimamizi wa hoteli, wahudumu na walinzi ambao walikuwa wamefunga mlango ili kuwazuia.

Kutokana na kitendo hicho ‘maninja’ hao waliwashambulia na kuwajeruhi maeneo mbalimbali ya mwili na kufanikiwa kufungua mlango na kutoka ndani ya hoteli.

WANANCHI WAWAKOMESHA
Baada ya kutoka kwenye jengo hilo walikutana na wananchi ambao walikuwa tayari wamejiandaa kuwakabili na wakati wakikimbilia kwenye magari waliyokuwa wamefika nayo hapo, wananchi waliwashambulia kwa mawe na kuvunja vioo vyote vya magari hayo.

Vipigo vya mawe kutoka kwa wananchi vilisababisha ‘maninja’ wawili kati ya hao walioingia ukumbini kuachwa na magari kukimbizwa na wananchi na wafuasi wa CUF na kufanikiwa kumkamata mmoja katika mtaa wa Mburahati Motomoto.

Mtu huyo alishambuliwa na wananchi na kujeruhiwa kwa kukatwa kwenye kisigino cha mguu wa kulia.

Akihojiwa na wananchi eneo la tukio, mtu huyo alidai kuwa si mfuasi wa CUF isipokuwa alishawishiwa na wenzake kwenda kufanya kazi hiyo ya uvamizi. “Jamani si mimi jamani nisaidieni mimi nimebebwa tu.

“Wamenaimbia nije nifanye hiyo kazi ila sijui chochote…Siyo mimi jamani, siyo mimi mmenikata mguu,” ilisikika sauti ya kijana huyo aliyekuwa katikati ya kundi la wananchi akijitetea.

Mmoja wa hudumu wa hoteli hiyo, alieleza kuwa hakufahamu kama ni wahalifu kutokana na kujitambulisha kuwa ni wanachama wa CUF.

KILICHOPONZA VURUGU
Kabla ya kuanza kwa vurugu hizo, Nkumbi aliwaeleza waandishi wa habari kuwa lengo la mkutano huo ni kuzungumzia tofauti zilizopo kati ya wafuasi wa Maalim Seif na Lipumba.

Aidha, alieleza kutokuutambua uongozi wa CUF wilaya ya Ubungo, ambao unamuunga mkono Lipumba kwa madai kuwa si kiongozi wa chama na hakuna kikao halali kilichowateua na hawatatoa ushirikiano kwa jambo lolote litakalofanyika.

Pia, walisema wanaunga mkono tamko lililotolewa na wanachama wa matawi 20 ya Mkoa wa Dar es Salaam la kumkataa Lipumba na kundi lake waondoke kwenye Ofisi za CUF za Buguruni.

Kuhusu Mtunzi

View all posts by

Maoni 3 katika "Maninja wa Lipumba wavamia mkutano wa CUF Dar es Salaam"

 1. salali 23/04/2017 kwa 4:31 um ·

  Bauce wa prof mzowa takataka ndembe ndembe mammamaye chezeya ukawa weweeee eeee.

 2. Elbattawi 23/04/2017 kwa 9:13 um ·

  Sifurahi kusikia vurugu za kupigwa na kuumizwa watu, lakini nashukuru sana angalau kuona uharamia uliyokuwa ukifanywa Pemba miaka ile baada ya uchaguzi mkuu wa 1995/2000 na kuendelea, umesambaa na kuhamia Tanganyika.

  Zamu ya Pemba kuteswa, kupigwa na kunyanyaswa tunashukuru imekwisha. Kwa upande wa Unguja, si haba kumetulia watu kupigwa na kujeruhiwa. MAZOMBI wako ‘holiday’.

  Ngoma ya MAZOMBI, kupiga na kujeruhi watu kwa maagizo ya serikali za CCM na mamluki aina ya Lipumba, imerejea kwao Tanganyika. Utawala wa kinafiki mwisho wake hukashifika kwa vitendo viovu kama hivi vya sasa.

  Wallahi, watawala akina Magufuli, Kikwete na wenzao wengine, bora kutawaliwa na punda au mnyama yoyote…wananchi wanaweza kuishi na kuendesha shughuli zao kwa amani na utulivu.

  Lazima tushangae, inakuwaje mtawala au niseme kiongozi wa nchi anaratibu vitendo vya uvunjifu wa amani kwa raia wake anao waongoza.

  Rais wa nchi anavunja sheria, Polisi wa nchi wanavunja sheria, anayejifanya kiongozi wa chama cha siasa anavunja sheria na mwananchi wa kawaida anakubali kutumwa kwenda kuvunja sheria.

  Nchi ya hatari sana, wala sijawahi kabisa kusikia kuwa duniani kuna nchi inayojigamba kuwa na utawala wa sheria, kuratibu vitendo vya kuvunja sheria, isipokuwa Tanzania.

  Wananchi wa Zanzibar, kwa muda mrefu hawakubaini kuwa uhalifu wa kuwapiga na kuwajeruhi wanachama na wafuasi wa CUF, unaratibiwa Tanganyika. Mungu, hafichi mnafiki sasa imenza kudhihirika.

  Pemba kuna msemo: ‘Tumbili akimaliza miti huja mwilini’ kwa msemo huo ndiyo hivi vitendo vinavyojiri sasa Tanganyika.

  Serikali kupitia Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kusimama kidete kumsaidia Ibrahim Lipumba katika vitendo vya kihalifu na matukio ya kuvunja sheria.

  Dunia imepata picha kuwa CCM imefilisika wala haikubaliki tena, viongozi wake wamepoteza dira na mvuto kwa wananchi na ndiyo maana wameacha siasa za kistaarabu na kugeuza mfumo wa siasa kuwa wa hatari na kijinga. Wamebaki katika kuendesha uhalifu.. 

 3. Jino kwa Jino 24/04/2017 kwa 4:37 mu ·

  Mimi sipendelei fujo lkn hali inapobidi kujitetea unatakiwa ujitetee bila ya woga na umuonyeshe adui wako kama weye shujaa wa kweli , inaonyesha CUF bado wako ktk usingizi mzito ni wazembe wa hali ya juu ni chama kisichojua mikakati hakina Vision wala strategy yyote vipi watu wanne wanakuja kuharibu mkutano mzima hamujui kwamba cuf muko katika vita sijui munafikiria nini, munafikiria mnacheza mdundikooo hamujui kama muna maadui wa ndani na wa nje kweli hivi ndio mmejipangaa kweli hivi ,naona hakuna dalili yyote wenzenu Kenya washabaduliasha tume ya uchaguzi kuna tume huru sasa ,na uchaguzi wa mara hii ama mbichi au mbivu lkn wapinzani washasema hawakubali tena ,sasa nyie cuf mmepewa lupumba tu anawatoa jasho kweli mutaiweza ccm Hebu jiulizeniiiiiii. Huyo Lupu kama ni nchi nyengine anagalikuwa tayari ni marehemu au yuko ICU pamoja na jecha >Mimi naona si rahisi bado CUF muko kama ndoto sana hta 2020 hamupewi serikali kwa maneno matupuuuuuu.Sera ya ccm hawatoi nchi kwa VIKARATASIIIIIIIII au Hamjuiiiiiii.

Comments are now closed for this article.