Lipumba amshambulia Maalim Seif na CHADEMA

Written by  //  09/04/2017  //  Habari  //  Maoni 3

lipumba+seif

By Bakari Kiango – Mwananchi
Sunday, April 9, 2017

Sarakasi zimeendelea ndani ya Chama cha CUF baada ya mwenyekiti wake anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kumshutumu Maalim Seif Sharif kwa madai ya kutaka kukiua chama hicho.

Lipumba alitoa tuhuma hizo jana, wakati wa kongamano la Jumuiya ya Vijana wa CUF (Juvicuf), lililofanyika kwenye ofisi za chama hicho Buguruni.

Akihutubia kongamano hilo alimtuhumu Maalim Seif kwa madai ya kubadili utaratibu wa vikao vya ushauri kwa kuzungumza na mkurugenzi mmoja mmoja badala ya kuwaweka pamoja.

Alisema kitendo hicho ni cha kumdhalilisha Naibu Katibu mkuu wa chama hicho Bara, Magdalena Sakaya.

“Sakaya amefanya kazi kubwa sana kukijenga chama hiki, lakini leo Katibu Mkuu (Maalim Seif) anamsimamisha uanachama Sakaya ili afukuzwe ubunge. Hivi tunajenga chama kweli hapa,” alihoji Lipumba na kujibiwa na wanachama wenzake kuwa chama kinabomoka.

Alisema huu ni wakati wa kukijenga chama na hakuna mwanasiasa Tanzania Bara aliyefanya kazi kubwa kuwatetea Wazanzibari kama yeye (Lipumba).

“Nasikia Maalim Seif anasema kutatokea machafuko endapo Rita wakifanya mambo yao. Maalim…hivi kukiwapo maandamano, kweli utakuwa mstari wa mbele, lini kulitokea ukawapo? Wakati maandamano yakifanyika unakimbilia Ulaya na habari unazipata huko huko,” alisema Lipumba.

Hata hivyo, Lipumba alisema amemsamehe Maalim Seif na yupo tayari kukaa naye meza moja ili kukijenga chama hicho ikiwamo kujenga uchumi utakaoleta manufaa kwa wananchi.

“Wakati wowote Maalim Seif njoo tuzungumze na turekebishe mambo,” alisema Lipumba.

Pia, Lipumba alikishutumu Chama cha Chadema kwamba kinamhadaa Maalim Seif na kinaweza ‘kumuuza’ kama kilivyofanya kwa Dk Wilbrod Slaa na kwamba hakina demokrasia kama kinavyotamba.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalim alisema chama hicho kinamtakia kila la kheri Lipumba na alimtaka akiache chama hicho kama kilivyo.

“Hata kama…hatuna demokrasia atuache kama tulivyo…lakini tunachojua hatumtambui yeye kama mwenyekiti wa CUF,” alisema Mwalim.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema Lipumba bado anaendelea kutapatapa na asitarajie yeye au Maalim Seif kufanya naye kazi pamoja.

“Umeniambia Profesa Lipumba amemsamehe Maalim Seif kwa kosa lipi? Hivi kati yake na Maalim nani kafanya kosa. Profesa Lipumba ndiyo anatakiwa kuomba msamaha Watanzania,” alisema Mazrui.

Alisema chama hicho kinafuata taratibu na hatua ya kumsimamisha uanachama Sakaya ilifuata kanuni kwa mujibu wa chama hicho.

Profesa Lipumba aliingia katika mgogoro na chama chake baada ya kuandika barua ya kujivua uenyekiti lakini baada ya mwaka mmoja wa nje ya uongozi alitengua kujiuzulu kwake.

Mkutano mkuu wa chama hicho ulikubali barua ya Lipumba ya kujiuzulu uongozi, lakini baadaye Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini iliandika barua ya kumtambua Lipumba kuwa ndiye mwenyekiti halali wa CUF, hali iliyokipasua chama hicho hadi sasa.

Kuhusu Mtunzi

View all posts by

Maoni 3 katika "Lipumba amshambulia Maalim Seif na CHADEMA"

 1. Abdul Zakinthos 09/04/2017 kwa 11:38 mu ·

  hihihi
  yule Mzee LIPU MBAA NAONA KAMA VILE HANA AKILI?

 2. mzeekondo 09/04/2017 kwa 4:29 um ·

  @ Abdul Zakinthos.

  Ndugu yangu Abdul Lipumba hana wazimu akili anazo, tatizo akili zake hazina maana na sisi, zina kila tija na wakoloni wenzake Tanganyika,huyu na kila Mtanganyika tunao shirikiana nao kwa sasa ni lazima tujue kuwa na wao siku ikifika wakihitajika kulinda maslahi ya Tanganyika na wao watafanya wajibu wao kwa taifa lao na huo sio usaliti.

  Usaliti tunao sisi Wazanzibari ambao hatuwezi,hatutaki na hatuna akili bado ya kujua haya mapema,tunadhani hawa wenzetu huyu hamjiulizi mwenyekiti wa ngapi wa cuf tangu kiundwe, anae kuja kuwaacha mkono baada ya kupewa amri na waliomtuma?mimi hata huyu Mtatiro mwenyekiti wa cuf kwa sasa upande wa maalim Seif, siwezi kumuamini hata dakika moja, naelewa wazi nae ukifika muda muafaka cuf wataisoma namba upya.

  Huu mpango wa kuwa na vyama kitaifa ninao upiga vita siku zote kuwa lazima mwenyekiti atoke bara,na lazima chama kiwe na wanachama bara kiasi fulani, ni mtego wa makusudi wa kuweza siku zote kupandikiza watu kama kina Lipumba, ili waje kuirudisha Zanzibar kwa Tanganyika kila tukijipapatua,hii sio bahati mbaya, huu ni mfumo wa makusudi ndugu yangu Zakinthos.

  Kosa limefanyika kwa cuf kuto kumkubalia barua ya kujiuzulu haraka Lipumba,japokuwa hakuna sheria inayo mruhusu Lipumba kujirudisha kwa mume baada ya kuomba talaka mwenyewe,sasa analitaka penzi kwa nguvu, kwa kuwa anajua hakupewa talaka, kwa hiyo bado yeye ni mke wa mtu.

  Maalim nae hamtaki kesha owa kwa kina Mtatiro,sasa huyu mke mkubwa analazimisha kugawa siku, hii ndio kesi iliyopo korti kwa sasa.

  Nakusalimia Abdul.

 3. zamko 11/04/2017 kwa 8:10 um ·

  @ Abdul Zakinthosh na @ Mzeekondo

  Ahsanteni kwa maoni yenu mazuri. hata mimi naona hivo hivo Huyu ni Lipu-Mbavuu.

  Leo napita tuu.

  isipokuwa nataka kuuliza.
  Kwani huyu Lipumba sio alishamfukuza Maalim Uwana chama na ukatibu mkuu?

  sasa anaposema maalim aje tukae meza moja tukijenge chama anakuwa anakusudia nini wakati yeye abaamini kwamba Maalim sio tena katibu mkuu wa CUF..

  Kutokana na usemi huu wa Lipumba, naweza kukubaliana na Watu Kwamba Lipumba hana Akili na ameishiwa KISIASA. Sasa amebakia kutapa tapa tuu mara kasema hivi mara vile..

  Msomi mzima anatumiliwa na GORILA lisilojuwa hata kuongea na WATU.. nalikifumbua Domo lake Jeusi kama Uso Wake basi litakuwa linahubiri Shari na Dhulma..

  Lipumba halijuwi afanyalo na sasa halbadiri za mbayana zamkumba.

  a

Comments are now closed for this article.