JK asema Bunge la Katiba litakutana Novemba 2013
Written by Ashakh (Kiongozi) // 01/01/2013 // Habari // 5 Comments
RAIS Jakaya Kikwete jana alitoa salamu zake za mwaka mpya kwa kuzungumzia mambo mbalimbali ya kitaifa, huku akibainisha kuwa Bunge la Katiba, litakaa Novemba mwaka huu kupitisha mapendekezo ya Katiba Mpya.
Katika hotuba yake hiyo, Rais Kikwete alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekamilisha hatua ya kwanza ya kukusanya maoni ya mtu mmojammoja nchi nzima na hatua inayofuata ni ya kukusanya maoni ya makundi maalumu.
“Kazi hiyo ya kukusanya maoni ya makundi maalumu, itaanza Januari 2013. Natoa wito kwa makundi hayo nayo kushiriki vizuri kwenye hatua hii muhimu. Baada ya hatua hiyo kukamilika, Tume itaandaa Rasimu ya Katiba ambayo wanategemea itakuwa tayari Mei, 2013.”
Rais Kikwete alisema Tume itatangaza muundo na namna ya kuwapata wajumbe wa Mabaraza ya Katiba na baada ya kuwapata rasimu hiyo ya Katiba itawasilishwa kwenye vikao vya Mabaraza hayo vitakavyofanyika kati ya Juni na Agosti, 2013.
“Baada ya kukamilika kwa vikao vya Mabaraza ya Katiba, Tume itakamilisha Rasimu ya Katiba ambayo itachapishwa kwenye Gazeti la Serikali kama yalivyo matakwa ya sheria. Aidha, itachapishwa katika magazeti ya kawaida kwa wananchi kusoma.
Novemba, 2013 rasimu hiyo itawasilishwa kwenye Bunge Maalumu kujadiliwa na kupitishwa. Baada ya Bunge Maalumu kupitisha itapelekwa kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho kupitia kura ya maoni,” alisema.
Rais Kikwete alieleza kama kila kitu kitakwenda kama inavyotarajiwa, Katiba Mpya iliyotokana na maoni na matakwa ya wananchi itapatikana ifikapo mwaka 2014.
“Mwaka huo Muungano wetu utakuwa unatimiza miaka 50, hivyo hiyo itakuwa zawadi ya tunu kubwa. Tukifanikiwa kupata Katiba Mpya wakati huo, tutafanya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa kutumia Katiba hiyo,” alisema.
Huduma za treni kusambaa Dar
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete amewaahidi wakazi wa Dar es Salaam kuwa Serikali itapanua usafiri wa treni kwa kuanzisha safari nyingine kutoka katikati ya Jiji kwenda maeneo ya pembezoni.
Alisema kazi hiyo iliyopangwa kuanza mwaka huu, inalenga kufikisha huduma za treni maeneo ya Tegeta, Kibaha na Mbagala Rangi Tatu, huku kukiwa na maboresho stahiki kwa treni zilizokwishaanza kazi
Rais Kikwete alisema tayari mshauri mwelekezi ameshateuliwa kufanya upembuzi yakinifu kwenye maeneo hayo… “Tunataka huduma hiyo iweze kufika Tegeta, Kimara, Luguruni, Kibaha Mbagala Rangi Tatu na Kongowe. Tuliamua kuanza na reli iliyopo lakini nia yetu ni kufanya vile hasa inavyotakiwa iwe kwa usafiri wa treni mijini.”



5 Comments on "JK asema Bunge la Katiba litakutana Novemba 2013"
Mi- niki-comments naambiwa natukana, tafadhalini Wazalendo toeni comments zenu kwa hii topic mpya.
Pambanua
Ziko comments nyingi umezitowa bila kuambia hivyo. Pale utakapofanya ndio unaambiwa. Hisi nani kakwambia.
Endelea kutoa comments wala usinune, almuhimu tu jiepushe na jazba, hamasa, lugha chafu. basiiiii
Kwa hali niliyojionea mimi kwenye ukusanyaji wa maoni ya znz watu wengi waliweka uzito katika suala la muundo wa muungano hivyo kusahau kabisa masuala mengine ndani ya katiba.
Kwa nguvu nyingi walizotumia smz na JMT dhidi ya wapinga muungano ni dhahiri kuwa tulipaswa tubalance maoni yetu yajikite pia katika masuala mengine yenye matatizo makubwa endapo tutafail kupata muundo wa muungano tuutakao.
hapa ni kuwa kila nchi itaongozwa na waziri mkuu na kuwa na raisi mmoja wa tanzania mfumo wa serekali 3 kwisha kabisa
@Abdul
Wee acha tu zije hizo serikali tatu, ndio hapo Waziri Mkuu wa Zanzibar na Waziri Mkuu watanganyika watakapokaa kujadili mustakbali wa muungano.
Tuombe Mungu Baraza la Wawakilishi liwepo.
Amma kwa upande mwengine ni nani mwenye mamlaka na uwezo wa kuifuta au kuibadilisha katiba ya Zanzibar?
Hata iwe si nchi wakati ina katiba yake vipi atapatikana Waziri Mkuu wa Zanzibar? Naomba uwelewesho