Stars yajipoza kwa Somalia

Written by  //  23/11/2015  //  Michezo  //  Maoni 3

Note: Hii taarifa nimeileta kisiasa zaidi

NA WAANDISHI WETU
23rd November 2015

o Yapata ushindi mnono katika mechi ya kwanza ya michuano ya Kombe la Chalenji

Hakika timu ya Taifa ya Bara ‘Kilimanjaro imewatoa kimasomaso Watanzania baada ya kupata ushindi wa bao 4-0 dhidi ya Somalia.

Mabao mawili mawili ya washambuliaji John Bocco na Elias Maguli yaliipa Kilimanjaro Stars ushindi mkubwa mbele ya Somalia katika Kundi A ya michuano hiyo.

Stars inayonolewa na kocha Abdallah Kibadeni, ilipata bao la kwanza kwa mkwaju wa penalti kupitia mshambuliaji wake, John Bocco katika dakika ya 11 baada ya Simon Msuva kuchezewa vibaya na beki wa Somalia.

Dakika ya 16, Elias Maguli alifunga bao la pili akimalizia pasi ya Msuva.

Baada ya mabao hayo, Stars iliendelea kutawala mchezo karibu idara zote uwanjani na kuwapa wakati mgumu Somalia.

Kipindi cha pili kilipoanza, Stars ilianza kwa kasi na dakika ya 53, Maguli alipiga bao la tatu akimalizia krosi ya nahodha Bocco.

Dakika ya 55, Stars ilihitimisha sherehe ya mabao baada ya Bocco kusukumia nyavuni bao la nne akiitendea haki pasi ya Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Baada ya mabao hayo, Stars iliendelea kucheza soka la kushambulia na kukosa mabao mengi ya wazi kupitia kwa Msuva na Bocco.

Baada ya mchezo, Kocha wa Somalia, Mbabazi Charles alisema kuwa wamefungwa kwenye mchezo huo kutokana na udhaifu wa mabeki.

Kocha Kibadeni alisema: “Tumepambana vizuri na kupata ushindi tuliostahili. Nitayafanyia kazi makosa niliyoyaona ili timu izidi kufanya vizuri.”

Nahodha wa Stars, John Bocco alisema ushindi huo hautawabwetesha, bali wataongeza juhudi ili washinde mechi zinazofuata.

Kilimanjaro Stars ilikuwa hivi;
Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Kelvin Yondani, Salim Mbonde, Himid Mao, Simon Msuva (Malimi Busungu), Said Ndemla, Elias Maguli, John Bocco na Deus Kaseke.

Wakati huohuo, mabingwa watetezi wa mashindano hayo timu ya Taifa ya Kenya (Harambee Stars) jana ilianza vyema baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Uganda (Cranes).

CHANZO: NIPASHE

Kuhusu Mtunzi

View all posts by

Maoni 3 katika "Stars yajipoza kwa Somalia"

 1. mohamed 23/11/2015 kwa 11:59 mu ·

  Binafsi habari za wabara sitaki kuzisikia, ni kwa sababu wao ndio wametufanya au wananifanya niwe hivyo.
  Kuna msemo”Samaki akionza mmoja huoza wote”.

 2. bokoboko 23/11/2015 kwa 6:09 um ·

  HIZI HABARI ZA MPIRA ZA STARS NA SOMALI HAZITUHUSU HUMU KWENYE WEBSITE SIS TUNATAKA MAMBO MUHIMU NA HABARI ZA SIASA MAMBO YANAENDAJE, HEBU MUANDISHI TUELEZE ULIKUWA NA MANTIK GANI KUTIA HABARI HIZO? KAMA HUNA HABARI BORA KAA KIMYA THAT ALL.

 3. Ashakh (Kiongozi) 24/11/2015 kwa 7:07 mu ·

  @ Bokoboko

  Ungesoma hiyo paragraph iliyokuwa highlighted ukafahamu. Hata hivyo nikufafanulie nilichokusudia.

  Tanzania ina timu tatu za Taifa, ambazo ni Taifa Stars, Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes kulingana na aina ya mashindano.

  Ila hapo kwenye hiyo para wenyewe hawataki utambuwe ni timu ipi kati ya tatu hizi. Para inasema hivi:

  “… timu ya Taifa ya Bara ‘Kilimanjaro imewatoa kimasomaso Watanzania..”

  Wakati sisi Wazanzibar tunayotimu yetu nayo inashiriki mashindano hayohayo.

  Bokoboko, mwishonikufahamishe licha ya kuwa wengi wetu ni mutribu kwa siasa, lakinimzalendo.net inajihusisha na nyanja zote za habari za nchi yetu. Iwe siasa, dini, utamaduni, mila, michezo, sanaa, kilimo, utafiti na kila unachokijuwa kikiwa na maslahi na faida kwa jamii yote kwa ujumla.

  Hivyo basi hapa utakutana na taarifa mchanganyiko. Ni wewe mwenyewe kuchaguwa ipi nataka nisome na ipi niiache. Kazi kwako.

Comments are now closed for this article.