Bunge, Maalim Seif wambana msajili mgogoro wa CUF

Written by  //  08/04/2017  //  Habari  //  Maoni 1

CUF+PICHAAA

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi  

By Boniface Meena na Sharon Sauwa – Mwananchi
Friday, April 7, 2017

Wakati Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Hamad akisema kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi anakivuruga chama chao, Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba imemtaka kuhakikisha anamaliza mgogoro wa chama hicho kuepusha kutia dosari Muungano.

Kauli hizo zimekuja siku moja baada ya Bunge kumtambua Naibu Katibu Mkuu wa CUF-Bara, Magdalena Sakaya kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho kwa maelezo kuwa Maalim Seif, anashindwa kutekeleza majukumu yake.

Bunge lilifikia uamuzi wa kutambua pande zote zinazopingana kwenye mgogoro huo baada ya msajili kumwandikia Profesa Ibrahim Lipumba kumweleza kuwa amekubali ombi lake la kutaka Sakaya atambuliwe kama Kaimu Katibu Mkuu, jambo ambalo linaonekana kuzidi kukigawa chama hicho.

Profesa Lipumba aliingia kwenye mgogoro na chama chake baada ya kuandika barua ya kujivua uenyekiti na kukaa nje kwa takriban mwaka mmoja kabla ya kurejea nchini na kuandika barua ya kufuta uamuzi wa kujiuzulu uenyekiti, jambo ambalo mkutano mkuu wa CUF ulilikataa na kuridhia kujiuzulu kwake.

Mgogoro huo umefanya kuwa na pande mbili; wa kwanza ukikubaliana na uamuzi wa mkutano mkuu wa kuridhia kujiuzulu kwa Lipumba, na wa pili ukikubaliana na kujirejesha madarakani kwa Lipumba.

Upande wa kwanza unaendesha shughuli zake kutoka Makao Makuu ya CUF yaliyopo Mtendeni, Unguja na upande wa pili ukiwa Ofisi Kuu zilizoko Buguruni, Dar es Salaam.

Jana, Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria ilimtaka Jaji Mutungi kuchukua jitihada za kuumaliza mgogoro wa CUF ili kuepusha athari kubwa zinazoweza kujitokeza katika Muungano.

Akisoma maoni ya kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka wa 2016/17 na ile ya 2017/18, mjumbe wa kamati hiyo, Joseph Mhagama alisema mgogoro huo unaweza kusababisha athari za Muungano.

“Katika mgogoro unaoendelea ndani ya CUF, Kamati inashauri Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuchukua jitihada za kutosha kusuluhisha mgogoro huo ili kuepusha athari kubwa zinazoweza kujitokeza katika Muungano,” alisema Mhagama.

Mhagama alisema kamati hiyo inaiagiza ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na weledi katika kusimamia utoaji wa ruzuku kwa vyama vya siasa na kuhakikisha kwamba taratibu hizo zinafuatwa katika utoaji ruzuku kwa vyama vya siasa.

Wakati wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Dimani na madiwani, msajili alitoa ruzuku ya zaidi ya Sh300 milioni ambazo zilichukuliwa na upande wa Profesa Lipumba ambao ulibadilisha majina ya watia saini wa akaunti iliyokuwa wilayani Temeke.

Oktoba mwaka jana, Bodi ya Wadhamini ya CUF, ilifungua kesi Mahakama Kuu dhidi ya Msajili, Profesa Lipumba na wanachama 12 waliosimamishwa.

Katika kesi hiyo, bodi inaiomba mahakama ibatilishe barua ya Msajili ya Septem 23, mwaka jana iliyotengua uamuzi wa Mkutano Mkuu wa kukubali kujiuzulu kwa Profesa Lipumba, imzuie Msajili asiendelee kufuatilia suala la kufutwa kwa uanachama wa Profesa Lipumba na pia azuiwe kuingilia mambo ya CUF.

Jana akizungumza na gazeti hili kuhusu uamuzi wa msajili kumtambua rasmi Sakaya kukaimu nafasi yake, Maalim Seif alisema, Jaji Mutungi ndiye chanzo cha matatizo ya chama hicho.

Alisema Profesa Lipumba si mwanachama wa CUF na pia si mwenyekiti wao kama anavyotambuliwa na Msajili.

“Tangu mwanzo msajili aliamua kuchukua upande na kuwa pamoja na Lipumba na ndiye mshauri wake…Wanashauriana kwa kila hali…lakini bado ukweli unabaki pale pale kwamba Lipumba si mwanachama kwa mujibu wa katiba ya CUF,” alisema Maalim Seif.

Maalim Seif alisema hata kama Profesa Lipumba angekuwa ni mwenyekiti, hana uwezo kumuengua katibu mkuu wa CUF.

“Chombo ambacho kina uwezo wa kuwashughulikia na kumsimamisha mwenyekiti, makamu mwenyekiti au katibu mkuu ni Baraza Kuu la Uongozi la Taifa…Halafu kama kuna kesi wanapeleka mkutano mkuu ambao unafanya maamuzi,” alisema Maalim Seif.

“Hata huyo Magdalena Sakaya mwenyewe naye kasimamishwa uanachama, si mwanachama. Mutungi ndiye anaendelea kulivuruga suala hili kwa mapenzi yake kwa Lipumba au sijui anapata instruction (maelekezo), sijui…Lakini Lipumba si mwenyekiti wetu, si mwanachama wa CUF.”

Alisema uchaguzi wa wabunge wa EALA umeharibika kwa sababu ya msajili kukubali waliyopendekezwa na Lipumba ambao si wanachama.

Katika uchaguzi huo uliofanyika Jumanne, Maalim Seif alipeleka jina la mgombea mmoja, wakati upande wa Lipumba ulipeleka majina matatu na ofisi ya bunge ikayapokea yote, ikayaweka majina hayo chini ya CUF “A” na CUF “B” kwa kuzingatia maelekezo ya msajili.

Maalim Seif alisema Habib Mnyaa, ambaye alichaguliwa kuwa mbunge wa EALA baada ya jina lake kuwasilishwa na Sakaya, alifukuzwa uanachama wa CUF na tawi lake na katiba yao inasema hawezi kurudi kuwa mwanachama wa chama hicho, hadi miaka miwili ipite.

“Yote haya Mutungi ndiyo kayachukua yeye ndiye anayevuruga na anaendelea kuvuruga,” alisema Maalim Seif.

Lakini jana, Jaji Mutungi alisema hatazungumzia suala hilo tena na vyombo vya habari, na kumtaka Maalim Seif asubiri uamuzi wa mahakama.

“Waandishi wa habari acheni kuendesha debate (mjadala) kuhusu suala hili kwa sababu liko mahakamani,” alisema Jaji Mutungi.

Jaji Mutungi ametoa onyo hilo wakati ameshtakiwa mahakamani lakini, ofisi yake ikimwandikia barua Profesa Lipumba kukubali uteuzi wake wa Sakaya kuwa Kaimu Katibu Mkuu. Hali hiyo inayonesha kibri kwamba msajili hashughulishwi na kesi inayomkabili mahakamani. 

Barua hiyo ya Machi 21 imesainiwa na Sisty Nyahoza wa Ofisi ya Msajili na inamweleza Profesa Lipumba kuwa itampa ushirikiano Sakaya katika majukumu yake ya kukaimu nafasi ya Katibu Kuu.

Kuhusu Mtunzi

View all posts by

Maoni Moja katika "Bunge, Maalim Seif wambana msajili mgogoro wa CUF"

 1. Elbattawi 08/04/2017 kwa 4:53 um ·

  Aibu aibu na fedheha kubwa kwa Tanzania kwa mambo yanayofanywa na vyombo vyake hasa vile vilivyopewa dhamana ya kutunga sheria na kuisimamia.

  Chombo, kama BUNGE ambalo ndilo linalotunga sheria za nchi ikiwemo sheria ya vyama vya siasa kweli linashindwa kuwa na uamuzi wa kukataa unafiki na kuendelea kutanua mgogoro unaendela ndani ya CUF.

  Hivyo, kweli Bunge halijui kuwa CUF kwa sasa kinakabiliwa na mgogoro na kweli bunge halijui kuwa Lipumba, alijiuzulu na baadaye kufukuzwa uanachama.

  Kwa nini Bunge kama linaendeshwa kwa kuzingatia maadili mazuri na uadilifu, lilikubali kuwapokea wagombea waliyoteuliwa kugombea ubunge wa EALA kutoka kambi mbili za CUF.

  Kwa nini halikuhoji kwanza uhalali wa wagombea hao kutoka chama kimoja lakini kambi tofauti za chama hicho hicho. Bunge la Tanzania ni zaidi ya KITUKO pamoja na SPIKA wake.

  Hivyo, kwa nini spika wa bunge, hakutaka maelezo zaidi kutoka kwa wabunge wa CUF, waliyomo ndani ya bunge kuhusu wagombea hao.

  Baadhi ya wabunge walipojaribu kuhoji uhalali wa Mohamed Mnyaa (Kambi ya Lipumba), spika alizuia na kupuuza hoja zao. Huku, ikifahamika kuwa Mnyaa, kafukuzwa uanachama wa CUF kutoka kwenye tawi lake.

  Nimejaribu kuwaza sana kitu hichi na kushangazwa na chombo kama Bunge la Tanzania, kuonekana lenyewe linavunja sheria na kupindisha haki za wananchi.

  Bunge linaongozwa ki-CCM limejaa siasa za dhulma na upendeleo. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, imekubuhu katika kukandamiza upinzani na upendeleo wa wazi wazi, hasa katika suala hili la mgogoro wa CUF.

  Kama alivyosema Maalim Seif kuwa, msajili ni tatizo kwa kuwa yeye ndiye aliamua kumuunga mkono Lipumba, kuanzisha mgogoro ndani ya CUF kwa maslahi yake binafsi, CCM na serikali zake.

  Kwa hali hii, ni wazi kuwa Tanzania inanuka dhulma katika taasisi zake zote na hali ikiendelea hivi hivi, kuna hatari kukumbwa na umasikini au ufukara kwa sababu haki haitendeki.

  Mwenyezi Mungu, huimiminia neema na baraka nchi na watu wake iwapo viongozi wake wanaheshimu maamuzi na haki za wananchi.

  Nchi bila ya viongozi wenye kupenda kutenda haki, waadilifu na wenye kuheshimu haki za raia, tabaan nchi hiyo itadidimia kwenye unyonge, ufukara, uonevu na majanga mengine, daima.

Comments are now closed for this article.